32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

BABU WA MIAKA 60 AFARIKI DUNIA AKIONGEZEWA NGUVU ZA KIUME KWA MGANGA WA KIENYEJI

 

Na KADAMA MALUNDE-Shinyanga


MZEE    Joseph Sahani (60), mkazi wa Kijiji cha Nzonza wilayani Shinyanga,  amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu ya kuongezewa nguvu za kiume kwa mganga wa kienyeji.

Sahani alifariki dunia baada ya mganga huyo wa kienyeji kumjaza dawa kwenye tundu la uume kwa kutumia pampu ya kujazia upepo baiskeli.

Akizungumza na waandishi wa habari   mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simoni Haule alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni.

Kamanda alisema  mzee huyo alikuwa akipatiwa matibabu ya kuongeza nguvu za kiume kwa mganga wa kienyeji,   Robert Nkoma (58).

Alisema mzee huyo alibaini kuwa ana tatizo la nguvu za kiume hivyo aliamua kwenda kwa mganga huyo ili atibiwe ndipo mganga alipomuingiza unga unaosadikiwa kuwa ni dawa ya kienyeji, kwenye tundu la uume kwa kutumia pampu ya baiskeli.

“Mganga alianza kuingiza dawa hiyo kwenye tundu la uume akitumia pampu ya baiskeli.

“Akawa anapampu kama anajaza upepo na kusababisha mzee aishiwe  nguvu na kutoka damu nyingi kwenye uume hali iliyosababisha kifo chake,” alisema Kamanda Haule.

Alisema   mganga huyo ametiwa nguvuni huku uchunguzi ukiendelea na utakapokamilika mtuhumiwa  atafikishwa mahakamani kwa hatua za sheria.

“Natoa wito kwa wananchi wenye matatizo ya afya  kuacha tabia ya   kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba, bali waende kwenye vituo vya afya au hospitali kufanyiwa uangalizi na kupewa matibabu sahihi,” alisema.

Katika tukio jingine, polisi wanamsaka mkazi wa Kitongoji cha Mwakakongoro wilayani hapa,  Masesa Sesaguli, kwa tuhuma za kumuua binti yake, Nshoma Masesa (16).

Binti huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Buhongwa  Mwanza, inadaiwa   aliacha masomo na kwenda kuolewa wilayani Kahama.

Inaelezwa kuwa mwanafunzi huyo aliuawa juzi kwa kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi.

Kamanda Haule  alisema chanzo cha mauaji hayo ni mwanafunzi huyo kutoroshwa shuleni na kupelekwa Kahama ambako alikuwa akiishi maisha ya ndoa na mwanamume aliyemtorosha.

Haule  aliwashauri wazazi kutokuwa na hasira wanapowaadhibu watoto wao.

Vilevile aliwaasa wanafunzi kujikita zaidi katika masomo na kuacha tabia ya kujiingiza katika mapenzi wakiwa katika umri mdogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles