Na JANETH MUSHI-ARUSHA
WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema wa Arusha Mjini na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki, wameweka hadharani ushahidi wa video unaoonyesha jinsi baadhi ya madiwani wao walivyoshawishiwa kukihama chama hicho na kujiunga na CCM.
Wabunge hao walibonyeza kitufe jana mbele ya waandishi wa habari kama walivyoahidi Jumapili iliyopita, kwamba wangeanika ushahidi huo hadharani kuonyesha mbinu walizoziita chafu, zilizofanywa na viongozi wa Serikali kwa madiwani wao.
Katika ushahidi huo, madiwani hao wanaonekana kwa nyakati tofauti, wakizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, Katibu Tawala, Wilaya ya Meru, Timotheo Mzava na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri.
Mazungumzo kati ya viongozi hao wa Serikali na madiwani hao, yanahusu kuhama kwa madiwani hao na ahadi walizotakiwa kupewa baada ya kutimiza nia hiyo.
Katika video ya kwanza inayoonekana kuchukua dakika zipatazo 30 baada ya kurekodiwa Agosti 28, mwaka huu, Mzava anaonekana akiwa ofisini akizungumza na mmoja wa madiwani wa Chadema kwa kumshawishi ahamie CCM.
Katika mazungumzo hayo, diwani huyo anaomba kabla hajajiuzulu, atekelezewe miradi miwili ya soko na barabara iliyopo kwenye kata yake.
Diwani huyo anasikika akisema ana nia ya kuhama ila ana mashaka na madiwani wengine waliokwisha kuhamia CCM ambao anasema yeye ni tofauti na madiwani hao.
Kwenye video hiyo hiyo, inaonekana siku diwani huyo huyo akizungumza na Mkuu wa Wilaya (Mnyeti), Mkurugenzi Kazeri.
Katika video hiyo, diwani huyo anaonyesha wasiwasi wa kuhama akisema anahofia kutolipwa fedha hizo baada ya kuhama.
Katika mazungumzo hayo, Mkurugenzi Kazeri anasikika akisema tayari wamekwisha kupiga hesabu ya idadi ya vikao walivyobakiza madiwani hao kabla ya kumalizika kipindi chao cha uongozi mwaka 2020.
Pia, Kazeri anasikika akimwambia diwani huyo kwamba ni vema akaangalia mwelekeo wa maisha yake na akimsisitizia diwani huyo kwamba ameshampa maelekezo mweka hazina wa halamshauri yao namna ya kuwalipa kiinua mgongo chao cha miaka mitano pamoja na posho zote ingawa wamekuwa madarakani kwa mwaka mmoja na nusu.
Mnyeti pia anasikika akimweleza diwani huyo kwamba akishaandika barua ya kujiuzulu na kuhamia CCM, atatafutiwa ajira
zitakapotangazwa na kwamba kabla ya ajira rasmi, diwani huyo atakuwa akifanya kazi za kujitolea akisubiri ajira rasmi.
Mnyeti anasikika akisema yeye hafanyi uamuzi lakini ana ushawishi na kwamba Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alishachukua wasifu wa madiwani hao (CV).
Vilevile Mnyeti anasikika akisema kwa mamlaka aliyonayo, atashughulikia suala hilo na alimsisitizia diwani huyo kwamba Rais Dk. John Magufuli, anatarajia kutembelea mkoani Arusha baada ya wiki tatu kuanzia siku waliyokuwa wakizungumza.
Mnyeti anaonekana akimshawishi diwani huyo ahame kwa kuwa Rais Dk. Magufuli atakapokuwa Arusha watapelekwa wakaonane naye usiku.
Kwa mujibu wa video hiyo, Mnyeti akiwa nje ya ofisi yake anaendelea kusema madiwani wengine wawili wameshatafutiwa ajira katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na katika ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mnyeti anazidi kumtaka diwani huyo aandike barua ya kujiuzulu na hata kama hana ajira, yeye yuko tayari kumlipa mshahara aweze kutunza familia yake.
Video hiyo pia inamuonyesha diwani huyo akilalamikia mgao wa Sh milioni mbili alizoahidiwa kupewa kama kianzio huku Mkurugenzi Kazeri akisikika akisema hakuna diwani aliyepewa zaidi ya kiasi hicho cha fedha.
Pia Kazeri anasikika akimwahidi diwani huyo kwamba atatekeleza miradi katika kata yake ili akigombea udiwani kupitia CCM wakati wa uchaguzi mdogo aweze kuchaguliwa kwa urahisi kwa kuwa ameshatekeleza ahadi kwa wapiga kura wake.
VIDEO NYINGINE
Video nyingine inaonyesha aliyekuwa Diwani wa Makiba, Emanuel Mollel, akizungumza na diwani mwenzake akimshawishi mwenzake ambaye haonekani vizuri kwenye picha, kwamba ahame kwa sababu hata Diwani wa Maroroni, Bryson Isangya, alipokuwa akioa, Mzava ambaye ni Katibu Tawala, ndiye aliyekuwa mratibu wa harusi yake.
Diwani huyo anasikika akisema kwamba Kazeri amewahakikisha kuwa uchaguzi mdogo ukirudiwa watampigia kura ya kutokuwa na imani Mwenyekiti wa Halmashauri, Willy Njau.
Katika video hiyo, mkurugenzi huyo anasikika akisema kwamba katika uchaguzi wowote utakaoitishwa, hakuna mgombea wa Chadema atakayetangazwa hata kama atakuwa ameshinda.
Mbali na video hizo, Lema na Nassari walionyesha sauti iliyorekodiwa ambako mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mnyeti, akizungumza na mmoja wa madiwani aliyejiuzuru jimboni kwa Nassari.
Katika sauti hiyo, Mnyeti anasikika akimuuliza kama wakati wa vikao vyao kuna mtu alikuwa anawarekodi, lakini mtu huyo anasikika akisema hakukuwa na mtu aliyekuwa akiwarekodi.
NASSARI
Akizungumza baada ya kuonyesha ushahidi huo ambao nakala zake alizigawa kwa waandishi wa habari kupitia flash, Nassari alisema
kufanya siasa na kuongoza wananchi hakuhitaji nguvu bali kunahitaji akili.
“Nilishasema sina shida ya diwani kuhama chama, nina shida na watu wanavyohama chama halafu kwa kumtaja rais, hii ni aibu kwa taifa, dola na Serikali kwa ujumla.
“Mmeona aina ya rushwa, rushwa ya fedha, ajira, ulinzi, makazi,
kiinua mgongo na posho ya miaka mitano ambayo mtu hajaitumikia, lakini anaahidiwa kupewa.
“Rais amejipambanua kwamba ni kiongozi anayesimama na kupinga rushwa kwa vitendo.
“Katika hili, sikutaka kuiabishia Serikali ndiyo maana nilitaka kukutana na rais nimpe ushahidi ili achukue hatua, lakini kwa kuwa Polepole ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM amejitokeza na kututaka tuwe wazi, na sisi tumeamua kueleza kila kitu.
“Juzi niliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kupitia ujumbe wa maandishi nikimuomba nikutane naye kumpa ushahidi wetu.
“Kwa hiyo, kesho asubuhi (leo), tutakwenda Takukuru Dar es Salaam kupeleka ushahidi kwa sababu kuna ushahidi mwingine hatujauonyesha kwa sababu ni aibu kwa Serikali.
“Kwa kifupi, tunao uchafu mwingi ambao tukiuachia hapa, ni aibu kwa dola na hata kwangu mbunge. Kwa hiyo, tunawaomba wachukue hatua , hii ni tamthilia kama Isidingo, yaani hii ni sehemu ya kwanza,” alisema Nassari.
LEMA
Naye Lema alisema watendaji wa Serikali waliohusika katika matukio hayo hawastahili kuwa kwenye ofisi za umma kutokana na makosa waliyoyafanya.
“Gharama za kurudia uchaguzi katika kata moja ni kati ya Sh milioni 250 hadi Sh milioni 300. Kwa hiyo, katika kata zote zitakazorudia uchaguzi, zitatumika zaidi ya Sh bilioni 4.5 ambazo zingeweza kujenga kilomita tisa za barabara.
“Sina hakika kama kuna hatua zitachukuliwa dhidi ya watu hao, lakini uhakika nilionao ni kwamba tumetekeleza wajibu wetu.
“Lakini tutakenda Takukuru, nyie tumewapa kidogo, wao tunawapa mziki wote waangalie na mambo ambayo tumeogopa kuwaonyesha hapa wajue sisi tuna busara,” alisema Lema.
Alisema anaamini Takukuru watachukua hatua dhidi ya watumishi hao kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa watu wengine wanaohusika na rushwa.
MNYETI
Akizungumzia madai hayo, Mnyeti alisema atazungumzia tuhuma hizo leo saa 2.00 asubuhi mbele ya waandishi wa habari.
Mkurugenzi Kazeri alipopigiwa simu, alimtaka mwandishi wetu ampigie baadaye na alipopigiwa tena, simu yake haikupatikana.
Viongozi wengine waliotajwa kwenye ushahidi huo wa video akiwamo Gambo, Katibu Tawala Mnzava Mollel, hawakupatikana kupitia simu zao za mkononi.