BARAZA la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameomba nafasi ya uwakilishi wa wazee bungeni kama ilivyo kwa kada nyingine kama wanawake au walemavu.
Wazee hao wamemuomba rais kiatika nafasi 10 za uteuzi kukatiba kumteua mwakilishi wa wazee walau nafasi moja.
Katibu Mkuu wa baraza hilo, Roderick Lutembeka amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya wazee duniani ambapo pia pamoja na hilo, baraza hilo pia limemwomba Rais John Magufuli kukutana na wazee ili kujadiliana na kupata ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.
“Sera ya wazee inataka, wazee wawakilishwe katika ngazi zote za maamuzi lakini pamoja na sera kutamka wazi bado wameshindwa kutumia nafasi hiyo kuteua nafasi ya mwakilishi wa wazee.
“Ila wapo wawakilishi wa vijana, wanawake na walemavu. Hali hii inawafanya wazee washindwe kuwa na mtu wa kuwasemea katika vyombo hivi muhimu vya kufanya maamuzi ya nchi,”amesema Lutembeka.
Aidha, amesema endapo Serikali haitafanya hivyo, wawakilishi wa wananchi ambao ni wabunge watumie kanuni ya Bunge kuwasilisha muswada binafsi kuhusu sheria ya wazee nchini.