32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MANENTO: UTOAJI TAARIFA UNAKUZA DEMOKRSIA

Na LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento, amesema haki ya kupata taarifa ni kiashiria kimojawapo cha serikali yenye uwazi ambayo inathamini mchango na ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa taifa.

Alikuwa akizungumza Dar es Salaam jana  wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya upatikanaji wa taarifa.

Jaji Manento alisema haki hiyo ni ya kila mtu hivyo inapaswa kulindwa kwa nguvu zote.

“Lengo la maadhimisho haya ni kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya haki ya kila mtu kupata taarifa muhimu kwa maisha yao, zilizopo katika hifadhi ya serikali na kwingineko.

“Haki ya kufahamu namna viongozi waliowachagua wanavyotekeleza majukumu yao na namna fedha za walipa kodi zinavyotumika,” alisema Jaji Manento.

Alisema haki hiyo ya kupata taarifa ni mojawapo ya nguzo kuu ya tamko la Umoja wa Mataifa  kuhusu haki za binadamu la mwaka 1948 ambalo Tanzania pia ni mwanachama.

Alisema Tanzania iliridhia azimio la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu   baada ya kupata uhuru pamoja na mkataba wa haki za  raia na  siasa hivyo inawajibika kuutekeleza.

“Haki ya kupata taarifa na wajibu wa kutoa habari unaimarisha misingi ya utawala bora ikiwamo uwazi, ushirikishwaji, uwajibikaji na utawala wa sheria.

“Watendaji wa Serikali watafanya kazi zao kwa uwazi na wananchi kwa ujumla wao hata mmoja mmoja watashiriki na watendaji hao watawajibika kwa wananchi wao katika kila ngazi ya utendaji na hatimaye utawala bora utaimarika,”alisema Jaji Manento.

Aliitaka Serikali kuhakikisha inatunga kanuni na sheria ya haki ya kupata taarifa ya 2016  kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.

Jaji Manento aliwataka wadau wa habari wakiwamo waandishi wa habari na taasisi zisizo za kiserikali kuendelea kupaza sauti kudai haki ya kupata taarifa kwa sababu watoa taarifa hizo wanaweza kujisahau.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, mwandishi mkongwe ambaye pia ni mwanasheria, Jenerali Ulimwengu, alisema kucheleweshwa kutungwa   kanuni za sheria ya haki ya kupata habari iliyotungwa mwaka jana na kuidhinishwa na Rais kumesababishwa asasi za raia na vyombo vya habari kuendelea kufungiwa.

“Tunapojadili suala hili tuangalie uwezo tuliokuwa nao au tuliotarajiwa kuwa nao, je tunao au umeminywa kabisa?

“Tangu sheria hii ipitishwe haijachapishwa katika gazeti la serikali wala kutungiwa kanuni na tumeona magazeti yakifungiwa.

“Uhuru wa kujieleza ndiyo mama wa uhuru wote, kama huna uhuru wa kusema nina njaa, uhuru wa kupata chakula, utatoka wapi?” alihoji.

Naye Mkurugenzi wa Sikika, Irenei Sungura, alisema ukimnyima mtu nafasi ya kujieleza unampa nafasi ya kufikiria zaidi hata yale ambayo asingeweza kuyafikiria kama angepewa uhuru.

“Sasa unapolifungia gazeti ambalo limechapisha taarifa ambayo ilikuwa imeenea kwenye mitandao, je unapozuia mtoa taarifa sisi wananchi tunaopokea taarifa hizo tuajua kuzichakata kujua ipi sahihi?” alihoji.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, Absalom Kibanda alisema mapambano dhidi ya sheria kandamizi kwa vyombo vya habari hayajaanza leo, kwa sababu  yamekuwapo kwa muda mrefu.

“Tatizo tunaongozwa na chama kile kile na watu wale wale na wenye mitazamo ile ile, hata akizaliwa  Waziri Mkuu mpya, Makamu wa Rais Mpya japo atakuja na staili mpya  ataendeleza yale yale.

“Kwa sababu ilianza wakati wa Mkapa (Benjamin) alipoandikwa akiwa kule Tabora aliwatisha wamiliki wa vyombo vya habari kuwa wataeleza wanakotoa mitaji, akaja aliyefuata Kikwete akajionuesha ana urafiki na vyombo vya habari kwa kutaka kuonekana,” alisema Kibanda.

Alisema kwa sasa Tanzania imekuwa na idadi kubwa ya watu wajinga kuliko ilivyokuwa zamani kutokana na kuminywa kwa uhuru wa kupata taarifa ikiwamo Bunge kutooneshwa  mubashara (live) na kuchaguliwa baadhi tu ya matukio ya kuonyeshwa.

Kuhusu mashambulio mbalimbali likiwamo la hivi karibuni dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema si geni bali ni mwendelezo wa matukio hayo tangu awamu zilizopita.

Mwakilishi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, alisema kwa sasa haki hiyo imeshuka sana na jamii wakiwamo waandishi wa habari wamejawa woga wa kuhoji mambo mbalimbali yanayohusu jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles