Mnamo Julai 20 mwaka jana, Rais Robert Mugabe aliwaambia maseneta wa Marekani kuwa “mtakiona” iwapo Trump akishinda urais. Mugabe aliwaambia maseneta wa Marekani waliozuru taifa hilo kwamba watajutia kutofanya urafiki naye iwapo Donald Trump atachaguliwa kuwa rais.
Maseneta hao, Chris Coons na Adam Schiff, waliliambia gazeti la Politico nchini Marekani kwamba, walikuwa katika taifa hilo kuzungumzia usafirishaji wa wanyama mwitu na kwamba waliomba kukutana na rais huyo na wakashangaa kwamba alikubali kuonana nao.
Maseneta hao walisema kuwa Mugabe aliwataka kuelezea kwa nini Marekani inaliwekea vikwazo taifa hilo ambapo walitoa sababu kadhaa. Ni wakati huo ambapo Mugabe aliwaambia: ”Wakati Trump atakapokuwa rais mtatamani mngefanya urafiki nami”.
Februari 20 mwaka huu, Mugabe alikubaliana na sera ya Rais Donald Trump kwamba “Marekani iwe ya Wamarekani”. Mugabe alizungumza kwa mara ya kwanza juu ya utawala wa Trump, ambapo alibainisha kushangazwa na ushindi wa kiongozi huyo wa Republican.
Hata hivyo, hakutaka mgombea wa chama cha Democratic “Madam Hillary Clinton ashinde”. “Lakini vilevile, ukija kwa Donald Trump ambapo anazungumzia uzalendo… Marekani iwe ya Wamarekani – katika hilo, nakubaliana naye. Zimbabwe iwe ya Wazimbabwe,” alikaririwa na gazeti la serikali la The Herald.
Aidha, kipindi hicho Mugabe alisema Trump anafaa kupewa muda wa kudhihirisha uwezo wake. “Sijui. Mpeni muda. Trump huenda hata labda ataangalia upya vikwazo vilivyowekewa Zimbabwe.”