Na Bakari Kimwanga, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna mstaafu Alfred Tibaigana, amesema umefika wakati wa wanaharakati kwenda mahakamani kupata tafsiri ya kisheria juu ya mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa kwenye rasimu ya Katiba Mpya na Bunge Maalumu la Katiba.
Amesema kutokana na malumbano yanayoendelea nje ya Bunge kati ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kundi la Tanzania Kwanza linaloundwa na wajumbe kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuna hatari Watanzania wakakosa Katiba.
Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana katika mahojiano maalumu, Tibaigana alisema ili kunusuru mchakato huo ambao unaonekana kuyumba na hata kutishia kutopatikana kwa Katiba Mpya, wanaharakati wanapaswa kwenda mahakamani kupata tafsiri ya kisheria.
“Kuhusu suala la Katiba Mpya kwa namna lilivyo sasa linaonekana kuelekea kukwama, nimefuatilia kauli za viongozi wa dini na hata Serikali, bado kuna kila dalili Bunge Maalumu la Katiba kukwama tena.
“Kwa maoni yangu ni vema wanaharakati waende mahakamani wafungue kesi ili kuweza kupata tafsiri ya kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, maana hivi sasa kila kundi limekuwa likivutia upande wake, kuna wanaopinga rasimu ya Tume ya Jaji Warioba isifumuliwe ila ijadiliwe na wengine wanataka kuifumua ili waingize na hata kuondoa baadhi ya vifungu,” alisema Tibaigana.
Alisema kama mahakama itaweza kutoa tafsiri, Watanzania wataweza kuelewa kama Bunge Maalumu la Katiba lina haki ya kubadili vifungu vya Rasimu ya Katiba ama la kuliko ubishani unaoendelea sasa.
“Ikiwa tafsiri itatolewa na mahakama na kila kundi kuweza kujua wanatakiwa kusimamia wapi na hii itatusaidia hata sisi tuliokuwa nje ya Bunge kujua nani mkorofi,” alisema.
Hivi sasa Tibaigana anajishughulisha na masuala ya ujasiriamali, ingawa mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu alijaribu kugombea ubunge katika Jimbo la Muleba Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujikuta akibwagwa wakati wa kura za maoni.