Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
NJOMBE Mji imesisitiza bado haijapotea njia na kilichotokea kwenye mechi zao mbili zilizopita ni upepo tu lakini hali itakuwa tulivu.
Njombe Mji imevurunda mechi zake zote mbili za Ligi Kuu msimu huu, ikianza kwa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Prisons kabla ya kubanduliwa bao 1-0 na Yanga wikiendi iliyopita.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Njombe Mji, Erasto Mpeka, alisema licha ya kupoteza michezo yote waliyocheza mpaka sasa, hali hiyo haijawakatisha tamaa badala yake wanajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Malengo yetu ni yale yale toka mwanzo ya kumaliza nafasi tatu za juu, kama tukishindwa kabisa basi tusikosekane kwenye 10 bora,” alisema Mpete.
Hata hivyo, alisema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa hasa ya kifedha lakini wanapambana kusaka wadhamini ili kuzitatua.
“Kuna changamoto kadhaa hasa katika gharama, lakini tunajitahidi kwenda nazo sawa, tunategemea sapoti kubwa sana ya wapenzi wa soka hapa Njombe,” alieleza mwenyekiti huyo.
Njombe Mji itashuka dimbani Jumapili kuumana na Mbeya City katika pambano la ligi hiyo litakalopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.