33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

UCHUMI KITANZINI WATAALAMU HAWASHTUKI

Na Shermarx Ngahemera

UCHUMI wa Tanzania ni kitendawili kwani umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia saba kwa miaka kadhaa sasa lakini hakuna cha kuthibitisha kwa wengi.

Kiwango hicho ni juu ya wastani wa nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA). Malengo ya kisera ni uchumi kukua kwa wastani wa asilimia nane au zaidi kwa mwaka na kutoboa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Kama ilivyo kawaida duniani, ukuaji huo  Tanzania unatofautiana kutoka sekta moja hadi nyingine. Zipo sekta zinazokua kwa wastani mkubwa na zinazokuwa kwa wastani mdogo.

Taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inasema katika robo ya kwanza ya mwaka 2017, ukuaji wa uchumi umeshuka kutoka asilimia 6.8 za kipindi kama hicho mwaka jana mpaka asilimia 5.7. Hii ni sawa na anguko la asilimia 1.1. Mambo mengi yanaweza kuchangia anguko hili na hivyo kuweka dhamira ya kweli ya kutaka kujua kwanini. Serikali imetulia tuli na kuacha kuzungumzia. Kuna haja ya kufanya utafiti wa kubaini sababu na namna ya kubadili mwelekeo huu ambao si mzuri.

Lengo la uchumi mpana ni kufikia ukuaji wa asilimia saba katika mwaka wa fedha 2017/18 na pengine tusipoangalia  mwaka huu katika kipindi cha pili kama uchumi utaendelea kupungua au kusimama ndio tunaweza kuanza kuwa na kupumbaa kwa uchumi (recession) hii ni hali kwa mfululizo wa vipindi viwili uchumi ukisinyaa.

Lakini dalili zote zipo na hivyo kusubiria wenye mamlaka kutangaza kwanini mambo yameanza kudorora. Kwani uzalishaji viwandani uko chini, migodi ya dhahabu hakuna anayejua kinachoendelea na uagizaji wa mitambo umenywea kulikoni? Watu wanahoji na kuhofu kuhusu lengo la asilimia 7 kwani linaonekana kutofikika kwa mwaka wa fedha uliopita. Inaweza kuwa kazi kubwa kufikia lengo hili la kisera. Ukuaji unatakiwa uongezeke kwa asimilia 1.3 ili kufikia lengo la asilimia saba. Suala la msingi ni kujua chanzo kikuu cha kushuka ukuaji na namna ya kurekebisha hali hii.

Ajira haijapanuka

Ajira ni kigezo kikubwa cha ukuaji uchumi lakini kwa hali iliyopo na mazingira yanayotawala ukuaji huo hapa nchini hauendani na hali halisi ya ajira kwani inaonekana kusinyaa ingawa matoleo mengi ya Serikali inaonesha azma sahihi ya kutaka kuajiri.

Ukuaji wa uchumi wetu hauleti ajira kwa wingi ni kwa sababu sekta zinazokua ni zile zinazotumia mitambo na mashine badala ya watu wengi kama kwenye kilimo au uvuvi.

Hivi sasa kazi ya watu wengi hufanywa kwa ufanisi mkubwa na watu wachache wakisaidiwa na au wakizisaidia mashine na mitambo ya hali ya juu. Matokeo yake, ni ukuaji mkubwa wa sekta husika bila kuajiri watu wengi na hatujajifunza namna ya kuishi na mashine na hivyo tunaelekea kukwama kwani usasa umetamalaki kila uwanda wa uchumi.

 Usasa uko kwenye viwanda vya kisasa, bandarini, migodi ya kisasa hutumia mitambo mikubwa na si watu kwenye uchimbaji na uchakataji, ujenzi wa ‘flyovers’, hata mashamba ya kilimo biashara (green house technology) kunatumika mitambo na mashine badala ya watu.

Usiseme kwenye mawasiliano ambayo imefanya posta kufungwa na watu wengi kukosa ajira na watu wa miamala hufanya wakala mmoja kwa kampuni zaidi ya 5 na hivyo ajira kunywea badala ya kukua. Mitandao ya jamii inaua magazeti.

Matumizi ya kompyuta yameleta faida lakini yamefukuza kazi watu na badala yake kompyuta moja huchukua nafasi za watu 10 hivi kwani utafiti kamili haujafanyika.

Umasikini kipato

Mara nyingi swali linaloulizwa ni kuwa kama uchumi umekua mbona fedha mifukoni haziko? Hili ni swali ng’ang’anizi kati ya malalamiko na maswali yanayoibuka. Yaani umasikini wa kipato.

Sababu za hali hii ni pamoja na sekta zinazokua kwa kasi kutokuwa na watu wengi na nyingi zinatumia mitambo. Hivyo basi walio nje ya hizi sekta hawafaidi ukuaji wake yaani kinachokua ni thamani na si ukubwa wa bidhaa au kwa maneno mengine si udhalilishaji na hivyo kukosa mwingiliano na sekta nyingine na hivyo haziweki msingi wa maendeleo ya sekta nyingine kama ingekuwa kilimo au uvuvi (synergies). Yaani lazima kuwe na kuwezeshana ndio pale tija itakuwa bayana.

Kwa mfano sekta ya madini inaweza kukua kwa kasi Kanda ya Ziwa, lakini sekta ya uvuvi, kilimo na ufugaji isifaidi ukuaji huo kwani hauna uhusiano (complimentarily). Hii itatokea kama ukuaji wa madini unatumia bidhaa za kilimo, uvuvi na mifugo kutoka nje badala ya ndani ya nchi kama ilivyo Tanzania.

Wakati mwingine, sekta zinazokua zinaweza kuwa chini ya umiliki wa kampuni za nje zinazoruhusiwa kuhamisha faida, mapato hata mtaji kwenda kwao. Hata kutokulipa kodi hakupo. Hapa kinabakia kiasi kidogo tu au kiduchu na si vinginevyo.

Hivyo basi kama sehemu iliyokua haitawekezwa nchini ukuaji huu hautafika mifukoni mwa wasio katika umiliki wa kampuni hizi kutokana na gawio la yatokanayo na ukuaji huu haliko nchini na hivyo kuona kitendawili tu.

Vile vile sera za uchumi huathiri matokeo ya uchumi husika kwani kama uchumi utakua lakini kodi na ruzuku zikawa zimepandishwa kwa masikini, basi umasikini hautapungua kwani utiririkaje wake uchumi huu hautakuwa mkubwa na endelevu ila utamilikiwa na Serikali yenyewe ambayo kimsingi si zalishaji.

Fikra za utawala bora na uwabikaji nazo huathiri mtazamo ikiwa ni pamoja na masuala ya haki za binadamu na maadili ambayo hudai au kuongeza gharama za utendaji na hivyo kuzuia ajira ikiwa ni kwa usalama wake au mahitaji maalumu.

Isitoshe mazingira na tabia nchi ni msingi mpya wa utendaji ambao huhakikisha kuwa mazingira hayaharibiwi katika mimbari ya ukuaji wa uchumi  husika na hivyo ni gharama ya ziada. Kwani ukuaji haupaswi kukinzana na haki za binadamu wala kutumikisha watoto au njia yoyote isiyoakisi utawala bora na maadili ya mwenendo wa umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles