NA SHARIFA MMASI-DAR ES SALAAM
CHAMA cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), kimesema timu yoyote itakayoshindwa kufuata ratiba za michezo ya robo fainali ya Ligi ya RBA iliyoanza jana bila sababu ya msingi itachukuliwa hatua.
Hatua hiyo ni pamoja na timu pinzani kupewa ushindi wa mezani.
Kauli hiyo kutoka kwa Rais wa BD, Emesu Okare, ilikuja baada ya kusambaa kwa nakala kutoka kwa umoja wa vilabu, wakidai kugomea mechi za robo fainali hadi hapo uongozi wa mkoa wao utakapotekeleza makubaliano ambayo waliafikiana kupitia vikao mbalimbali.
Okare aliliambia MTANZANIA kuwa, mgomo huo unasukumwa na baadhi ya viongozi wa klabu wenye nia ya kurudisha maendeleo ya mchezo huo nyuma.
“Ni kweli nimeona taarifa zikizagaa mitandaoni kuwa timu zilizopangiwa kucheza leo (jana) hatua ya robo fainali, zimegoma.
“Nitoe kauli hii nikiwa kama Rais mwenye dhamana, michezo itakuwepo kama kawaida, timu zitakazojitokeza zitaendelea na ratiba na kwa zile ambazo zinadai kugoma basi zitawasababishia wapinzani wao kupata ushindi wa mezani,” alisema Okare.
Miongoni mwa mahitaji hayo ni pamoja na BD kuwalipa waamuzi madeni yao ya nyuma ambayo ni kiasi cha Sh 2,080,000, lakini hadi sasa fedha zilizotolewa ni 700,000 tu.