29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

GINIKI: MEDALI IMENIPA MZUKA WA KUPAMBANA

NA WINFRIDA MTOI

KWA miaka mingi Tanzania ilikuwa imepotea kwenye ramani ya dunia katika mchezo wa riadha kutokana na kufanya vibaya kwa muda mrefu, lakini kuna mwanga umeanza kuonekana.

Ndani ya mwaka mmoja na nusu riadha imekuwa na mabadiliko tofauti, baada ya baadhi ya wanariadha kuchanua kwenye mashindano ya kimataifa na kutwaa medali.

Miongoni mwa wanariadha wanaokuja juu hapa nchini ni Emmanuel Giniki, ambaye wiki iliyopita alifanikiwa kutwaa medali ya dhahabu kwenye mashindano ya majeshi ya nchi wanachama wa Afrika Mashariki katika mbio za nyika za mita 10,000.

MTANZANIA Jumapili imezungumza na Giniki kuhusu mafanikio hayo, hasa baada awali kukosa medali katika mashindano ya dunia yaliyofanyika London, Uingereza, iliyosababishwa na kupata majeraha njiani wakati wa fainali ya mbio za mita 5000.

Akizungumzia ushindi huo, mwanariadha huyo anasema amefurahi kwa sababu ameweza kuwazidi wale waliokuwa wanamsumbua kwa muda mrefu wanapokutana kwenye mashindano mbalimbali.

“Nimefurahi kushinda kwa kweli, mashindano yalikuwa magumu kwa sababu kila mmoja alikuwa amejipanga kushinda, nashukuru Mungu ameweza kunitetea katika kufanikisha ndoto na kuitangaza nchi yangu vizuri.

“Ugumu wa mashindano hayo unatokana na uwepo wa wanariadha wengi wakali, lakini nilikomaa hadi dakika ya mwisho sijakubali kushindwa kirahisi. Medali hii ni ishara nzuri kwangu, inaonyesha jinsi gani ninazidi kupanda na sitarudi nyuma,” anasema.

Anaeleza siri ya ushindi wake kuwa kabla ya kuanza mbio alijiandaa kisaikolojia mwenyewe kwa kujiweka tayari kwa matokeo yoyote na changamoto atakazokumbana nazo wakati akikimbia.

“Kabla ya kuanza mbio lazima ujipange ukubali hali utakayokutana nayo, hivyo kitu cha kwanza kabisa nilitambua katika michezo kuna kushinda na kushindwa, lakini pia lazima upambane ili kushinda, vyote hivyo vilikuwa kichwani mwangu.

“Nilijua fika nakimbia na wanariadha kutoka nchi tofauti, ikiwamo Wakenya, ambao siku zote wanajiamini kwamba ndio washindi, ila nilikomaa mwisho wa siku nikawashinda,” anasema.

Anasimulia miongoni mwa wanariadha aliowamwaga siku hiyo mmojawapo ni Ezekiel Kimboi wa Uganda, ambaye kwa muda mrefu alikuwa anamsumbua wanapokutana kwenye mashindano mbalimbali.

“Ujue kwa sasa Afrika Mashariki katika mbio ninazokimbia kuanzia 5,000 na ‘Half Marathon’, ni wanariadha wawili  tu ndio ambao wananisumbua nikikutana nao, lakini Kimboi tayari nimemshinda na  aliyebaki ni Mkenya Michael Kororo, endapo siku moja nitakutana naye na nikamshinda itakuwa hakuna wa kunipa shida tena katika ukanda huu.

“Hivi sasa nafanya mazoezi sana kwa sababu ndiyo silaha kubwa ya ushindi, siwezi kujibweteka. Naamini ipo siku nitamshinda Kororo kwa kuwa unapowapita wanariadha wanaokusumbua  na kuvunja rekodi zao, inakuongezea morali na kuendelea kufanya vizuri kushinda,” anasema.

Giniki mara nyingi mashindano yake ya nje anapenda kwenda China, hapa anaeleza siri ya kupenda kushiriki mbio za huko kuwa ni kutokana na mfadhili wake ni raia wa nchi hiyo na ana mchango mkubwa katika mafanikio yake.

“Mimi nimefika hapa nyuma yake pia kuna mtu anayenisaidia, hivyo nawashauri wanariadha wenzangu wajitahidi kutafuta wafadhili kwa sababu wanasaidia  mambo mengi na kukufanya upate mashindano mengi ya kimataifa ili kukujenga kiushindani na kukutangaza.

“Kwa mfano, sasa hivi nimerudi kutoka Burundi kwenye mashindano ya majeshi, lakini tayari nimeanza mazoezi kwa kuwa natarajia kwenda China kushiriki mashindano ya nusu marathoni mwezi ujao, baada ya hapo nitarejea kujiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola,”  anaeleza.

Anasema matatizo yaliyotokea kwenye mbio za dunia huko London ameshasahau, kwa kuwa ni jambo la kawaida katika michezo, kwa sasa anasonga mbele kuhakikisha anakuwa na rekodi kubwa zaidi.

Anaeleza kuwa, majeraha ni moja ya changamoto alizokumbana nazo katika safari yake ya riadha hadi kumfanya akate tamaa ya kuendelea na mchezo huo, lakini alijipa matumaini na kurejea tena baada ya kupona.

Katika mashindano ya London, Giniki aliumia mguu wakati wa fainali ya mbio za mita 5,000, zilizoshirikisha wanaridha 21, akiwamo mwanariadha maarufu, Mo Farah na kuambulia nafasi ya 13.

Mashindano mengine ya kimataifa aliyoshiriki

Giniki, ambaye ni mzaliwa wa Kateshi, Wilaya ya Hanang, Manyara, mwaka huu ndipo jina lake liling’ara zaidi baada ya kufanikiwa kushinda medali tatu za dhahabu katika mashindano matatu tofauti yaliyofanyika China.

Medali ya kwanza alichukua Aprili 27, kwenye michuano ya ‘Shanghai Half Marathon’, akitumia muda wa saa 1:01:36, Mei 7, aliibuka kidedea katika mashindano ya Naijing Xianlin Half Marathon kwa muda wa saa 1:02:00 na Mei 16 mbio za  ‘Jurong Half Marathon’ alitumia 1:04:00 .

Mashindano mengine aliyoshiriki ni ‘Jinjiang inter Half Marathon’ mwaka 2015, ikiwa ni mara yake ya kwanza kukimbia nje ya nchi na alifanikiwa kushinda katika nafasi ya kwanza akitumia dakika 62:36.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles