30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA BADO WABABE KWA AZAM

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

TIMU ya Azam FC na Simba SC zinatarajia kukutana leo katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

Azam itakuwa mwenyeji katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa kwanza kwa timu hiyo kucheza kwenye Uwanja wa Chamazi dhidi ya timu za Simba na Yanga, fursa hiyo imekuja siku chache baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufanya mabadiliko ya ratiba katika michezo ya ligi kuu.

Mchezo huo utakuwa na msisimko mkubwa kutokana na timu hizo kuanza vizuri katika michezo yao ya awali msimu wa 2017/2018, kutokana na timu zote hizo kuibuka na ushindi.

Simba iliufungua msimu kwa kupata ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, huku Azam ikianza kwa kushinda bao 1-0 walipocheza na Ndanda FC.

Utamu wa mchezo huo unatokana na upinzani uliopo baina ya timu hizi, kwani katika msimu uliopita timu hizo ziligawana pointi tatu kutokana na kila mmoja kushinda mchezo mmoja kwenye Ligi Kuu.

Simba ilishinda mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa bao lililofungwa na Shiza Kichuya, kabla ya Azam kulipa kisasi kwa kushinda mechi ya mzunguko wa pili huku bao likiwekwa kimiani na  aliyekuwa nahodha, John Bocco ‘Adebayor’, ambaye kwa sasa amejiunga na Wanamsimbazi hao.

Ukiachilia mbali Ligi Kuu, timu hizo zilikutana katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi, Simba ilikubali kufungwa 1-0, bao lililofungwa na kiungo, Himid Mao, lilitosha kuipa Azam ubingwa wa michuano hiyo.

Simba ilifanikiwa kulipa kisasi katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ‘FA’, ambapo bao la kiungo, Mohamed Ibrahim ‘Mo’, lilitosha kuing’oa Azam katika michuano hiyo, huku wao wakinyakua taji hilo.

Licha ya rekodi hizo za msimu uliopita kuonyesha jinsi mchezo utakavyokuwa na upinzani, mvuto zaidi katika mchezo huo utakuwa ni pale wachezaji; Erasto Nyoni, Aishi Manula na Bocco watakapoikabili timu yao ya zamani.

Uimara wa vikosi 

Timu zote zina utajiri mkubwa wa wachezaji wanaocheza eneo la katikati ya uwanja, ambapo kila timu imesheheni mafundi wa kuuchezea mpira.

Safu ya kiungo ya Azam inaongozwa na nahodha, Himid Mao, Salum Abubakar ‘ Sure Boy’, Frank Domayo, Stephen Kingue, huku Simba ikiwa na James Kotei, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Haruna Niyonzima na Mo Ibrahim katika eneo hilo.

Mchezo unaozikutanisha timu hizi umekuwa na kawaida kuwa na matumizi wa viungo wengi kwa kila upande, hivyo mara nyingi mechi za Azam na Simba mpira huchezwa katikati ya uwanja.

Simba inajivunia kuwa na wachezaji ambao wanaweza kuamua matokeo kama Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na John Bocco, huku kwa upande wa Azam kukiwa na Yahya Mohamed, Ramadhani Singano na mshambuliaji wao mpya, Mbaraka Yusuph.

Udhaifu wa vikosi

Timu zote hizo zimekuwa na changamoto kubwa kwenye maeneo ya ulinzi, kocha wa Azam Mromania, Aristica Cioaba, ana mtihani wa kujenga  upya kikosi chake kufikia uimara uliokuwapo misimu mitatu iliyopita chini ya Stewart Hall.

Baada ya kuondokewa na wachezaji wake muhimu, Cioaba atakuwa na mtihani wa kuwaunganisha nyota wake wapya waliosajiliwa msimu huu, wakiwamo Salmin Hoza, Mbaraka Yussuph na  Wazir Junior.

Simba imesajili wachezaji mahiri kwa ajili ya kuimarisha eneo lao la ulinzi, changamoto kubwa kwao inakuja pale wanapomkosa Mzimbabwe, Method Mwanjale, katika kikosi.

Mwanjale anapokosekana  safu hiyo ya ulinzi huwa shakani licha ya kuwapo mabeki imara kama Mganda Jjuuko Murushid na Salim Mbonde, Mwanjale amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu hiyo kutokana na uwezo wa kuongoza wenzake.

Wakati mamilioni ya wapenzi wa soka nchini wakisubiri kwa hamu mpambano huo wa kukata na shoka kati ya Simba SC na Azam FC, rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 24 katika mashindano mbalimbali tangu 2008.

Katika michezo hiyo, Simba imeshinda mara 10, imepoteza 9, sare tano, huku Azam ikishinda michezo tisa, kupoteza 10 na sare tano.

Ligi Kuu Tanzania Bara 

Mechi: 17 (2008-2017)
Azam: Ameshinda 5, amepoteza 8, sare 4
Simba: Ameshinda 8, amepoteza 5, sare 4

Kombe la Kagame

Mechi: 1 (Julai 2012) katika robo fainali
Matokeo: Azam FC 3-1 Simba

Kombe la Mapinduzi

Mechi: 2 za nusu fainali
Matokeo: Azam FC 2-0 Simba (2012), Azam FC 2-2 Simba (Azam akashinda kwa penalti 5-4).

Kombe la Urafiki

Mechi: 1 (Julai 2012) katika fainali
Matokeo: Azam FC 1-3 Simba

Kombe la Benki ABC

Mechi: 1 (Agosti 2012) katika nusu fainali
Matokeo: Azam FC 1-2 Simba

Kombe la FA

Mechi: 1 (Aprili 2017) katika nusu fainali

Matokeo: Simba 1-0 Azam FC

Kombe la Mapinduzi

Mechi: 1

Matokeo: Azam 1-0 Simba.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles