NA RAMADHAN HASSAN – DODOMA
SERIKALI imesema zaidi ya vibali vya ajira 10,000 vimesainiwa, huku 4,816 vikiwa katika taratibu za kutolewa ili kuziba mapengo yaliyojitokeza baada ya wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi kuondolewa katika ajira.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susanne Masele.
Katika swali lake, Masele alitaka kujua kauli ya Serikali kwa watumishi wa umma waliokuwa wamesaini mikataba ya ajira na baadaye Serikali ikasitisha ajira ili kupisha ukaguzi wa watumishi hewa.
Aidha, alitaka kujua kama Serikali inatambua kuwa watu hao tayari walikuwa watumishi na mchakato wa kuwaingiza kwenye orodha ya malipo ya mishahara ulishaanza, lakini ukasitishwa ghafla na sasa wako mtaani na hawajui hatima yao.
Mbali na hilo, mbunge huyo alihoji ukweli wa kauli ya kuwa Serikali haiwezi kuajiri watumishi kutokana na ukosefu wa fedha.
Akijibu maswali hayo, Kairuki alisema Serikali ina uwezo wa kuajiri na tayari vibali 10,000 vimesainiwa huku 4,816 vikiwa mbioni kutolewa.
Alisema mishahara mwaka huu hawakupandisha kwa sababu bado wanaendelea kuangalia hali ilivyo, ikiwamo hali ya kiuchumi.
“Kilichofanyika ni nyongeza ya mwaka ya mishahara na wakati wowote kuanzia sasa nyongeza hiyo itaanza kutekelezwa,” alisema Kairuki.
Kwa upande wa madaraja, Waziri Kairuki alisema tayari fedha ilishatengwa na zaidi ya Sh bilioni 660 zimeongezeka katika bajeti ya mwaka huu ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana.
Alieleza kuwa bajeti ya mwaka jana ilikuwa Sh trilioni 6.6, lakini mwaka huu wametenga zaidi ya Sh trilioni 7.205.
“Fedha hizi zitasaidia kulipa madeni ya watumishi, pia kupandisha watumishi zaidi ya 193,166 na wakati wowote zitaingizwa na watumishi watazipata,” alisema Kairuki.
Kairuki aliliambia Bunge kuwa watumishi wote waliositishwa kuingizwa katika orodha ya malipo ya mishahara Mei mwaka jana kupisha uhakiki wa watumishi, kwa sasa wamesharudishwa na wanaendelea na kazi na kulipwa mishahara yao kama kawaida.
Aidha, alisema watumishi hao wanatambuliwa kama watumishi wengine wa umma.