Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MTOTO wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, John Nyerere, anatarajiwa kuzikwa Jumatano hii kijijini kwao Mwitongo wilayani Butiama mkoani Mara, baada ya kukamilika kwa taratibu za mazishi.
John alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipokua amelazwa baada ya kuugua maradhi ya mapafu na kisukari yaliyosababisha kifo chake.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwao marehemu Msasani jijini Dar es Salaam, mjukuu wa Mwalimu Nyerere, Moringe Magige, alisema mwili wa marehemu John utaagwa leo Msasani kuanzia saa 7 mchana na baada ya hapo utasafirishwa kesho kuelekea wilayani Butiama kwa mazishi.
“Baada ya kuwasili mwili saa 7 mchana kutakuwa na ibada maalumu ya kumuombea marehemu itakayochukua muda wa saa moja,” alisema Moringe.
Aliongeza baada ya kumalizika kwa ibada, mtoto wa marehemu, Charles Makongoro, atasoma wasifu wa marehemu na kwamba akimaliza watatoa heshima ya mwisho.
Katika msiba huo viongozi mbalimbali wa chama na Serikali walihudhuria kutoa rambirambi kwa familia ya Mwalimu Nyerere wakiongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Mkuu Pinda, alisema wanashirikiana na familia katika msiba huo huku akiahidi kutoa taarifa kwa viongozi wa nchi za Ukombozi wa Afrika ili nao waweze kujumuika katika msiba huo.
Viongozi wengine waliohudhuria msiba huo ni pamoja na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Nape Nnauye.