32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JE, TUMECHELEWA KUONGEZA TIMU?

 MARKUS MPANGALA NA ZAINAB IDD


LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuingia katika ushindani mpya kuanzia msimu ujao 2018/2019 ambapo timu zitaongezeka kutoka 16 hadi 20. Uamuzi huo ulitolewa  mwezi uliopita na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kwa hiyo mwishoni mwa msimu huu timu mbili zitashuka daraja ili kuzipisha mbili za kupanda pamoja na nne mpya zitakazoingia. Katika makundi hayo matatu zitatoka timu sita zitakazopanda Ligi Kuu Bara.

Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza ina timu za African Lyon, Ashanti United, Friends Rangers zote za Dar es Salaam; JKT Ruvu na Kiluvya United za Pwani; Mgambo JKT ya Tanga, Mvuvumwa ya Kigoma na Polisi Moro ya Morogoro.

Timu za Kundi B ni Coastal Union ya Tanga, JKT Mlale ya Ruvuma, KMC ya Dar es Salam, Mawezi Market ya Morogoro, Mbeya Kwanza ya Mbeya, Mufundi United ya Iringa na Mshikamano na Polisi Dar za Dar es Salaam.

Kundi C lina timu za Alliance School, Pamba na Toto African za Mwanza, Rihno Rangers ya  Tabora, Polisi Mara ya Mara, Polisi Dodoma ya Dodoma, Transit Camp ya Shinyanga na JKT Oljoro ya Arusha.

NDANI YA UWANJA

Idadi ya timu 16 zinaipa timu mechi 30 kwa msimu mzima wa Ligi. Hiyo ina maana raundi ya kwanza ya Ligi Kuu inakuwa na mechi 15, kisha raundi ya pili inakuwa na mechi 15 ambazo zinakamilisha 30 ili ligi hiyo imalizike.

Katika soka la ushindani mechi 30 za Ligi Kuu Bara kwa msimu mmoja ni chache sana. Hii ina maana idadi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ni sawa na Ligi Kuu ya Ubelgiji yenye timu 16 pia anayoshiriki nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta.

Kuna makundi mawili ya ushindani wa Ligi Kuu Bara. La kwanza linajumuisha timu za Yanga, Simba na Azam FC. Kundi la pili linajumuisha timu za Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Mbeya City, kwa mbali kuna Mbao FC ambayo ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita.

Zipo timu zilizopanda daraja msimu huu Lipuli, Njombe Mji na Singida United ambazo zimeonyesha ushindani katika mechi zao za kwanza.

Swali linaloulizwa sasa, je, ongezeko la timu za Ligi Kuu Tanzania Bara litakuwa na manufaa yoyote? Kama tulivyoona hapo juu kuwa wachezaji hugombania kushiriki mechi 30 za ligi, kisha yapo mashindano ya shirikisho ambayo bado idadi kubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza hutumika huko.

Ongezeko la timu 20 linamaanisha mchezaji atacheza mechi 38 za msimu kwa ujumla. Hilo litachangia wachezaji kuwa fiti zaidi. Kwamba raundi ya kwanza mchezaji atapigania kucheza angalau mechi 10 na raundi ya pili mechi 10 ili afikishe 20 kumweka fiti hata ikiwezekana zaidi ya hapo.

Mechi nyingi zinawasaidia wachezaji kuimarika zaidi, hivyo atakapocheza mashindano ya shirikisho yanakuwa ziada kwake kuongeza utimamu wa mwili. Hayo ndiyo mambo ya ndani ya uwanja iwapo timu zitaongezwa na yana manufaa kwa ushiriki mashindano ya kimataifa.

WADHAMINI

Upande mwingine inasemwa ongezeko la timu linachangia gharama kubwa kuanzia kwa timu zinazoshiriki, wadhamini wa ligi ambao ni Vodacom, Azam TV na wengineo. Faida ya mechi 20 wadhamini wa timu mbalimbali watafikisha habari za bidhaa zao mbali zaidi kuliko sasa.

Hata hivyo jambo la kuzingatia ni kwamba ongezeko la timu za Ligi Kuu Bara limewahi kuzua malumbano makali mfano halisi ikiwa ni Ligi Kuu Kenya, ambapo kituo cha Televisheni cha Supersport kililazimika kujitoa. Kwenye udhamini baada ya Shirikisho la Soka Kenya kutangaza kuongezeka idadi ya timu na kufikia 18.

Maana yake gharama za kuonyesha ligi hiyo zinaongezeka kuanzia wadhamini wakuu Vodacom, ambao watakuwa na mabadiliko katika mkataba wao wa miaka mitano kuwa na majukumu ya kuongeza fedha kwa ajili ya timu nne zitakazoongezeka.

WACHAMBUZI NA MAKOCHA WATOA NENO

Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, kocha wa zamani wa Mwadui FC ambaye kwa sasa afundisha Dodoma FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, anasema si jambo baya kuongeza idadi ya timu katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa maslahi ya timu ya taifa. Julio anasema ilibidi kwanza kuwe na mfumo mzuri wa kupandisha timu kutoka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwenda Ligi Kuu (VPL).

“Sio jambo baya kwani lengo ni kufanya kuwe na changamoto kwa wachezaji na hata timu husika lakini lazima iangaliwe, je, mfumo wa kupandisha timu kutoka FDL kwenda VPL upo sawa kwa maana yakuwa wanaopata nafasi wanapanda kwa haki.

“Tunaweza tukawa na timu 20 na zaidi lakini VPL ikawa na timu za hovyo kutokana na wengi wao kupanda daraja kwa kushika mkono jambo linalopunguza ladha ya Ligi Kuu Bara,” anasema.

Kennedy Mwaisabula’ Mzazi’ ni kocha mzoefu na mchambuzi wa soka nchini ambaye anasema kabla ya kuongeza idadi ya timu, TFF ilipaswa kuboresha ligi kwa kutafuta wadhamini wengine ili kuongeza fedha kwa timu.

“Tunafahamu hali ngumu iliyopo kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara hivyo ni vema wakapatikana wadhamini watakaoongeza dau la fedha kwa timu shiriki, kuweka miundombinu mizuri, kuwa na waamuzi wenye kutafsiri sheria 17 za soka kiufasaha kisha ndipo idadi ya timu ziongeze, lakini ongezeko hilo sio baya iwapo kama kutakuwa na maboresho katika ligi husika,” anasema.

RAIS TFF AFUNGUKA

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzanai (TFF), Wallace Karia anasema kuwa suala la Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na timu 20 lilijadiliwa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji miaka mitatu iliyopita isipokuwa zilitakiwa kuanza timu 18 msimu uliopita kabla ya kufika 20 msimu ujao.

“Miaka iliyopita lilijadiliwa hili na kamati ya utendaji na ikakubaliwa lingeaanza na timu 18 msimu uliopita kabla ya unaokuja kufika 20 lakini ilishindikana kwa kuwa tulihofia wadhamini wetu wakuu huenda wangeshindwa hivyo tukasubiri mkataba wao umalizike ndipo tuliweke wazi,” anasema.

Karia anasema: “Kwa upande  wadhamini wetu Azam TV hakuna tatizo kwani mkataba wao unaruhusu ligi kuwa na timu 20, hivyo hakukuwa na budi kusubiri umalizike mkataba wa Vodacom ambao msimu huu ukimalizika nao mkataba wao umefika mwisho.”

Anasema iwapo kama Vodacoma au kampuni nyingine itahitaji kuidhamini Ligi Kuu Tanzania Bara hawana budi kujua zipo timu 20 na sio 16 kama ilivyokuwa, hii yote ni kutaka wachezaji wacheze mechi nyingi zaidi.

“Lengo kubwa la kuongeza idadi hiyo ya timu katika VPL ni kutoa nafasi kwa wachezaji kucheza angalau michezo 40 ya kwa msimu, lakini pia kuongeza uzoefu kwa waamuzi wetu, nina hakika hakutakuwa na tatizo mara baada ya kuanza jambo hilo msimu ujao,” anasema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles