Na Neema Mathias
-MAELEZO
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imekamilisha awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule 10 kongwe za Serikali, ili kusaidia miundombinu bora ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuongeza nafasi za wanafunzi kupata elimu.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Sylvia Lupembe kuhusiana na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa shule hizo za sekondari unaotekelezwa na Serikali kupitia TEA.
“TEA inakarabati shule kongwe 17 kati ya 87 na tumeanza ukarabati wa shule 10 katika awamu ya kwanza unaogharimu Sh bilioni 10. Hadi sasa ukarabati huo umefikia asilimia 80 na ifikapo Oktoba utakuwa umekamilika,” alisema.
Alizitaja shule zinazokarabatiwa kuwa ni Mzumbe na Kilakala (Morogoro), Msalato (Dodoma), Mwenge (Singida), Pugu (Dar es Salaam), Ilboru (Arusha) na Same (Kilimanjaro).
Nyingine ni Tabora Wavulana na Tabora Wasichana zote za Tabora na Shule ya Sekondari ya Wasichana Nganza iliyopo Mwanza.
Alisema ukarabati wa awamu ya kwanza umehusisha miundombinu ya majengo ikiwemo mabweni, madarasa, majengo ya utawala, kuboresha mifumo ya maji safi na maji taka na mifumo ya umeme.
“Tayari makabidhiano ya awali yamefanyika kwa baadhi ya majengo hususan mabweni na madarasa katika shule za Msalato, Mwenge na Mzumbe,” alisema.
Lupembe alibainisha kuwa mafanikio kutokana na mradi huo yameanza kuonekana kwani ari ya wanafunzi kusoma imeongezeka na idadi ya usajili wa wanafunzi imeongezeka katika shule ya Mwenge na nyingine zilizokarabatiwa.