Na JANETH MUSHI -ARUSHA
WAZIRI Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, amelaani kukamatwa kwa Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) na kudai kuwa vitendo hivyo vinaweza kuligawa taifa kwa ubaguzi wa kisiasa miongoni mwa jamii.
Kutokana na hali hiyo amewaomba viongozi wa dini wakiwamo maaskofu, wachungaji na masheikh nchini kukemea ukiukwaji wa misingi ya Katiba na sheria ikiwamo manyanyaso na udhalilishaji unaoendelea nchini dhidi ya viongozi wa upinzani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa Lema alisema hatua ya kukamatwa kwa mbunge huyo na Jeshi la Polisi sambamba na kumsaka Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ni wazi kuna dalili mbaya ambayo inaweza kuzaa chuki za kisiasa miongoni mwa jamii ya Watanzania.
Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chadema, alisema hatua ya kukamatwa Bulaya kwa amri ya Mkuu wa Wilaya kwa tuhuma za kufanya mkutano wa hadhara nje ya jimbo lake ni jambo la ajabu ambalo ni wazi linakwenda kuua demokrasia nchini.
“Nimewaita kulaani vikali kitendo cha Bulaya kukamatwa kwa amri ya DC huku Heche akiendelea kuwa mafichoni kwa sababu anatafutwa kwa kosa ambazo hata kwenye Katiba ya nchi hazipo.
“Kosa la Bulaya halipo hata katika sheria hakuna na hata kama sheria itafanyiwa marekebisho gani huwezi kutunga sheria ya kumzuia mbunge au mtu yeyote kuongea katika mipaka ya Taifa lake.
“Mimi kama mbunge na waziri kivuli nimepata madhila ya kukamatwa na polisi, hili jambo linaumiza na kusikitisha sana. Mbunge kukamatwa kwa kuwa amekwenda kwenye mkutano kwenye jimbo jingine, hii ni hatari sana kwa nchi na inaendelea kuligawa Taifa…. maana yake huko tunakoelekea kuna siku wasukuma watasema hawawataki wachaga katika mikoa ya usukumani.
“Kuna siku watu wa Morogoro watasema hawawataki wamasai kwao, hii mbegu siyo tu inaua demokrasia bali inaua uhuru wa kutoa maoni na haki ya kutembea popote,,” alisema Lema
Kutokana na hali hiyo alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro kuwaelekeza askari wake kote nchini ili waache tabia ya kufanya kazi kwa kufuata maelekezo ya viongozi wa kisiasa.
Alitolea mfano kukamatwa kwa Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro (Chadema) na viongozi wa dini waliokuwa wamekwenda kutoa rambirambi kwa wazazi waliopoteza watoto wao katika ajali ya basi la shule ya Lucky Vincent, ambapo viongozi hao walikamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
“Tunawaona polisi wakitekeleza maagizo tunajiuliza maagizo haya wanasema ni amri ya DC au RC, namtaka IGP Sirro alielekeze Jeshi lake lifanye kazi kwa weledi, siyo kila amri itakuwa na afya katika Taifa hili, siyo kila amri itakuwa na maana katika Taifa hili, maana leo DC akisema mbunge apigwe risasi kabla ya saa 12 jioni tutapigwa risasi.
“… najiuliza wako wapi Usalama wa Taifa, ninajiuliza sana na ninafahamu Mkuu wa Idara hiyo Dk. Kapilimba ni mcha Mungu tena ni Mchungaji anaingia ibada kila Jumapili, sidhani kama matendo haya wanayaona wanaendelea kukaa kimya, wanaitakia nini nchi haya mambo ni hatari maana leo siwezi kuhutubia mkutano Arumeru Magharibi au Mashariki, waishauri Serikali juu jambo hili,” alisema
Lema aliwashauri viongozi na watendaji wa serikali nchini kuiga mfano wa Rais Uhuru Kenyata wa Kenya ambaye aliruhusu maandamano ya kumpinga wiki iliyopita.
“Rais Kenyata aliruhusu mkutano na maandamano ya kumpinga, yaliyoandaliwa na wapinzani nchini humo wakishutumu chama chake kimeiba kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo, akawapa na polisi wakalinde. Hii ndiyo demokrasia ni mfano wa kuigwa hasa ikizingatiwa limetokea katika nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema.
Mwisho