30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MARAGA ASHIKILIA URAIS WA KENYATTA

NAIROBI, KENYA

WIKI mbili baada ya kuapishwa kuwa Jaji Mkuu mnamo Oktoba mwaka 2016, David Maraga, alifanya mazungumzo na kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika Mahakama ya Rufani kwa muda wa saa moja na nusu.

Ulikuwa mpango wake kama rais mpya wa Mahakama ya Rufani kuzungumza na wanasiasa waandamizi, ambapo awali alianza kufanya kikao cha kwanza na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kukutana na Raila.

 

 

sasa Jaji Maraga anakabiliwa na kibarua kizito katika kusimamia na kutoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na muungano wa Upinzani NASA dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Isiyo na Mipaka na Chama cha Jubilee kupinga matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.

 

Akiambatana na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka na kiongozi mwingine wa NASA, Moses Wetang’ula, Odinga ameripotiwa kusema Jaji Maraga yuko kwenye mioyo ya Wakenya na amebeba heshima ya mhimili wa mahakama na imani ya wananchi wote.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, Jaji Maraga alisema kesi hiyo dhidi ya IEBC na Jubilee ni kipimo cha uwajibikaji na heshima ya Mahakama ya Rufani ambapo uamuzi wake ni wa mwisho katika ngazi zote za kisheria.

Taarifa zinasema kuwa katika kipindi ambacho alikutana na wanasiasa wakubwa nchini humo, Jaji huyo aliwahakikishia uwazi wa hukumu za kesi zote.

“Napenda kuwahakikishia wananchi, Mahakama ipo tayari na inamudu kusikiliza mapingamizi yote yatakayotokea mwakani (uchaguzi wa mwaka 2017),” alisema Jaji Maraga alipokuwa akizungumza na Odinga na wafuasi wake, ikiwa ni njia ya kujenga imani kwa mhimili huo.Aidha, Jaji Maraga amesisitiza Mahakama ipo tayari kupokea na kusikiliza pingamizi lolote tangu siku ya kwanza alipoapishwa na sasa anakabiliwa na jukumu zito la kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8, mwaka huu.

MAJAJI 7

Wakati Mahakama ya Rufani ikisikiliza na kuandaa hukumu ya kesi hiyo, itasikilizwa na majaji 7 wa mahakama hiyo wakiongozwa na Jaji Maraga ambaye macho na masikio yote yapo kwake.

 

Jaji Maraga akiwa katika nafasi ya rais wa mahakama atakuwa sehemu ya kusikiliza kesi na dhahiri hii ni kesi kubwa kwake.

 

Aidha, Jaji Maraga atakuwa mwenyekiti na majaji wengine sita katika kesi hiyo kuhusu kura za urais. Majaji wengine ni  Jaji Mohamed Ibrahim, Profesa Jackton Ojwang’, Dk. Smokin Wanjala na Jaji Njoki Ndung’u ambaye amewahi kusikiliza kesi kama hiyo ya matokeo ya uchaguzi mwaka 2013.

KANISANI

 Taarifa zinasema kuwa tayari Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Jaji Isaac Lenaola, wameshakula kiapo. Katika kusikiliza kesi majaji wote wanakuwa na uhuru wa kusikiliza na kuamua kulingana na jinsi wanavyoona wao, inaelezwa kuwa hapo ndipo kuna hukumu ya Mahakama.

Jaji Maraga ni muumini wa Kanisa la Adventisti ambalo hufanya ibada siku ya Jumamosi. Jaji huyo ni miongoni mwa wazee wa kanisa hilo hali ambayo inatajwa kumuwia vigumu kusikiliza kesi hadi siku ya Jumamosi, ambapo siku za karibuni amewakosoa wanasiasa wanaoushambulia mhimili wa mahakama.

“Litakuwa jambo gumu kwangu kuketi mezani siku ya Jumamosi na kusikiliza kesi yoyote,” Jaji Maraga aliiambia kamati ya Huduma ya Mahakama.

Jaji Maraga anatajwa kushikilia imani yake ya Kikristo hivyo hataweza kufanya kazi za mahakama siku ya Jumamosi.

 

MAHAKAMA YAONGEZA MUDA

 

Mahakama ya rufani jana ilitangaza kuruhusu kesi iliyofunguliwa na NASA kusikilizwa hadi usiku. Mahakama hiyo iliamua kusikiliza kesi hiyo kuanzia saa moja asubuhi hadi usiku ili kutoa muda wa kutosha kuwasilisha nyaraka za kupinga matokeo ya uchaguzi.

 

Msajili wa kesi katika Mahakama ya Rufani, Esther Nyaiyaki, amesema timu ya utetezi kutoka upande wa Rais Uhuru Kenyatta, wanapaswa kujibu mashtaka.

 

Kwa mujibu wa sheria ya kupinga matokeo ya urais, mlalamikaji anatakiwa kuzishtaki pande mbili, ambazo kwa sasa ni Rais Kenyatta na Tume ya Uchaguzi. Katiba inasema kesi ya kupinga matokeo inatakiwa kufunguliwa siku 7 baada ya kutangazwa kwa matokeo. Pia Katiba inasema Mahakama ya Rufani itasikiliza shauri hilo ndani ya siku 14 tangu kufunguliwa.

 

Hiyo ina maana kesi iliyofunguliwa na NASA itasikilizwa kabla ya Septemba 1 mwaka huu licha ya awali kutangaza kutofungua kesi yoyote dhidi ya matokeo ya urais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles