NA SHARIFA MMASI -DAR ES SALAAM
KOCHA wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 16,Bahati Mgunda na mchezaji Jesker Ngaisaise, wamerejea nchini juzi wakitokea Afrika Kusini, kuendesha zoezi la kusaka vipaji vya makinda watakaojiunga na akademi ya watoto ijulikanayo kwa jina la ‘NBA Junior ’.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mgunda alisema safari hiyo ilikuwa nzuri, kutokana na kujifunza mambo mbalimbali yenye manufaa kwake na Taifa zima.
“Namshukuru Mungu tumerudi salama mimi na mchezaji wangu Jesker ambaye yeye alipata nafasi ya kuwakilisha nchi katika semina maalumu ya wachezaji iliyomalizika Afrika Kusini.
“Binafsi nimejifunza mambo mengi sana ambayo nitayatumia katika ufundishaji wa watoto katika mchezo huu, ambapo pia wakiyazingatia watanufaika nayo siku zote za maisha yao wakiwa bado ni wachezaji,” alisema Mgunda.
Mbali na hilo, Mgunda alisema watajipanga kuandaa semina ya muda mfupi kwa ajili ya mchezaji Jesker, atoe elimu ya kile alichojifunza ughaibuni kwa wachezaji wenzake wa kike.
“Tunafikiria jambo moja muhimu sana la kumpa nafasi mwakilishi wetu wa Afrika Kusini ili apate muda wa kuzungumza na vijana wenzake juu ya kile alichojifunza ughaibuni,” alisema.