HARARE, ZIMBABWE
SERIKALI ya Zimbabwe itajenga chuo kwa gharama ya dola bilioni moja, kwa heshima ya mtu anayelaumiwa kuporomosha uchumi wa taifa hilo, Rais Robert Mugabe.
Waziri wa Elimu, Jonathan Moyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanachukua hatua hiyo kwa heshima ya Mugabe (93) kwa wajibu wake katika elimu na uongozi mzuri.
Haijulikani fedha hizo zitatoka wapi katika nchi ambayo ukosefu wa ajira na umasikini ni tatizo kubwa.
Mwaka uliopita zaidi ya watu milioni moja nchini Zimbabwe walikumbwa na ukosefu wa chakula kutokana na ukame.
Nchi hiyo kwa wakati fulani ilitajwa kuwa taila lenye neema lisilojua njaa barani Afrika.
Licha ya hilo, Baraza la Mawaziri limekubali kutumia dola milioni 800 kujenga chuo hicho kipya huko Mazowe, kilomita 35 nje ya mji wa Harare.
Fedha nyingine za dola milioni 200 zimetengwa kwa utafiti katika chuo hicho cha Robert Gabriel Mugabe, kitakachoangazia masuala ya sayansi na teknolojia.
Tangazo hilo limekosolewa na vyama vya upinzani ambavyo vimeungana na vina matumaini ya kuuondoa utawala wa miaka 37 wa Mugabe wakati wa uchaguzi wa mwakani.
Tayari Zimbabwe ina wakati mgumu kugharamia elimu na huduma za umma na miundo msingi kama barabara na hospitali.