29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kudhibiti usafirishaji fedha mipakani

 

Na Benny Mwaipaja- WFM, Dar es Salaam

WIZARA ya Fedha na Mipango imeandaa kanuni za taarifa za usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na kwenda nje ya nchi ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na wasafiri wote wanaotoka au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha taslimu wanazosafirisha ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola za Marekani 10,000.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa kanuni hizo, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Onesmo Makombe, alisema utekelezaji wa kanuni hizi pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.

“Takwimu hizo zitasaidia pamoja na mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na kuhakikisha kuwa tunapunguza kama si kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha zitokanazo na uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi,” alisema Makombe.

Alisema kanuni hizo zimeweka adhabu zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha zinazolingana au zinazozidi kiwango kilichowekwa bila kutoa taarifa au watakaotoa taarifa za uongo.

Alizitaja adhabu hizo kuwa ni pamoja na kukamatwa kwa fedha taslimu walizonazo na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria kama vile kufunguliwa mashtaka.

“Wahalifu pamoja na mambo mengine, wanapenda kusafiri na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia benki kutuma fedha kutokana na umakini unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza kuwepo mipakani,” alisema.

Kamishna huyo amewaasa washiriki wa warsha hiyo kutekeleza jukumu hilo  kwa uadilifu na uaminifu mkubwa  ili kuziba mianya yote ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kutimiza kusudi lao ovu na kuhatarisha usalama wa nchi.

Kutokana na umuhimu wa ushiriki wa wadau mbalimbali katika utekelezaji wa kanuni hizo, warsha hiyo imejumuisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali wengi wao wakiwa ni maofisa forodha.

Washiriki hao wametoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kikanda, Mamlaka ya Mapato Tanzania na vikosi vya ulinzi na usalama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles