Na CLARA MATIMO
PAROKIA ya Kung’ara Bwana wetu Yesu Kristo Mabatini Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mwanza, inakabiliwa na changamoto ya waumini wake kuendelea kuamini ushirikina.
Hayo yalielezwa na Katibu wa Halmashauri ya Walei wa Parokia ya Mabatini, Lawrence Mayunga, wakati akisoma risala katika sherehe ya kutimiza miaka 13 ya parokia hiyo kanisani hapo.
Alisema baadhi ya waumini wa parokia hiyo ambao wanatenda matendo ya ushirikina bado wameghubikwa na imani kwamba wakitenda hivyo watapata utajiri wa haraka na kuishi maisha bora.
“Mheshimiwa mgeni rasmi wapo baadhi ya waumini ambao walikabidhiwa mikoba ya ushirikina kutoka kwa wazazi, bibi au babu zao na wakati wanakabidhiwa walitishwa kwamba endapo wakiacha na kumtumikia Yesu watapata majanga makubwa.
“Hivyo wanaamua kuwatumikia mabwana wawili wakati Yesu Kristo alisema ukitaka kumfuata lazima ujikane,” alisema Mayunga.
Alisema kanisa linatatua changamoto hiyo kwa kuwapa semina, mfungo na maombezi ya mara kwa mara waachane na imani za zamani waweze kumpokea Yesu katika roho ikiwa ni pamoja na kutenda matendo mema ambayo aliyafundisha.
Mgeni rasmi katika sherehe hiyo ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Sala Ibanda Ziwani Parokia ya Mabatini Jimbo kuu la Mwanza, Padri, Jeme Ebo, aliwataka watu wote kujenga moyo wa upendo.
Alisema upendo wa moyoni unajenga uhusiano mzuri kati ya Mungu na mwanadamu.
Aliwasisitiza wakristo wote waliompokea Yesu kuachana na imani za ushirikina kwa sababu kumchanganya na shetani ni sawa na kuweka mafuta na maji ambavyo havichanganyiki.
“Achaneni na dhambi ndugu zangu maana ni mbaya ng’areni kama ambavyo jina la parokia yenu lilivyo.
“Pia tatueni changamoto zinazowakabili bila kutegemea wafadhili naamini mkiungana mnao uwezo wa kufanya maboresho makubwa katika parokia yenu.
“Mlikotoka ni mbali na mmepiga hatua katika maendeleo, wekezeni fedha zenu kwa Mungu ukimtolea naye atakuzidishia,”alisema Padri Ebo.