Na  Walter  Mguluchuma-Katavi .
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Sumbawanga, imemhukumu  Yustine  Robarti (32)mkazi wa  Kijiji cha   Majimoto  Wilaya ya Mlele  Mkoa wa  Katavi kunyongwa hadi kufa,  baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la  kumuua   mke wake na  watoto wake wawili, kisha kuwatumbukiza ndani ya kisima cha maji .
Hukumu  hiyo ilitolewa wiki iliyopita na  Jaji wa mahakama hiyo, Adam Mambi katika vikao vinavyoendelea kufanyika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.
Mtuhumiwa alitiwa hatiani, baada ya mahakama kuridhika na     ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Achiles Mulisi.
Awali katika kesi hiyo,Mulisi alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 23,2015 saa 7 usiku baada ya kutokea ugomvi na mke wake, wakati wakiwa wamelala chumbani na watoto wao wadogo ambao aliuawa.
Ilidaiwa siku ya tukio, Yustini alimpiga mke wake, Monica Lwiche (25), kisha baada ya kumuua alimtupa ndani ya kisima cha maji.
Baadae aliwauwa watoto wake, Eliza Robert (4) na Frank Robart (6) kwa lengo la kuvuruga ushahidi kwakuwa wakati akifanya kitendo hicho watoto walikuwa wakishuhudia
Kabla ya kufanya tukio hilo, mshtakiwa alikuwa ametoa kauli za vitisho endapo mke wake atarudi nyumbani atafanya jambo litakalokuwa la kihistoria na ambalo halitasahaulika kwa wakazi wa kata hiyo.
Mshtakiwa katika kesi hiyo, alikuwa anatetewa na wakili Patrick Mwakyusa ambapo upande huo wa utetezi ulikuwa na mashahidi wawili, mshtakiwa mwenyewe na baba yake mzazi.
Katika utetezi huo, waliiomba mahakama imwachie huru kwani upande wa mashtaka umeshindwa kudhibitisha kama kweli alitenda kosa hilo.
Pia walidai upande wa mashtaka, umeshindwa kudhibitisha kuwa wakati anafanya mauaji hayo, hakuna mtu yoyote aliyeshuhudia tendo hilo la kumuua mke wake na watoto.
Utetezi huo ulipingwa vikali na Mulisi kwa kile alichodai wa katika ugomvi unatokea mwanzoni, mama mwenye nyumba alikokuwa amepanga mshtakiwa alishuhudia ugomvi huo na ushahidi wa maneno ya vitisho aliyoyatoa mshtakiwa ni ushahidi tosha ndiye aliyetekeleza mauaji hayo.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Adam Mambi aliiambia mahakama  kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka na utetezi mahakama, lazima iangalie mambo matatu ambayo ni ushahidi wa mazingira,je upande wa mashtaka unadhibitisha na kama kweli mshtakiwa amehusika au la.
Hivyo aliieleza mahamakama kuwa kutokana na maswali hayo,mahakama ilihoji na kujilisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Kutokana na ushahidi huo, mahakama ilimtia Robert kwa kosa la kifungu cha sheria namna 196 na 197 cha kanuni ya adhabu na alitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kabla ya kusoma hukumu.
Naye Mwasheria wa Serikali, aliiomba mahakama itoe adhabu kali li iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo na hasa wanaowaua watu wasiokuwa na hatia.
Baada ya maelezo hayo,Mambi ali alimhukumu kunyongwa hadi kufa.