RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka Watanzania wasigawanyike kwa masuala ya kidini na ukabila kwa kuwa wanaweza kuvuruga amani ya nchi.
Dk. Shein alitoa wito huo jana mjini Songea alipokuwa akizindua mbio za mwenge wa uhuru katika Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
“Kuna baadhi ya makundi yamekuwa yakifanya jitihada za kuwagawa Watanzania kwa kuingiza masuala ya udini na
wengine wanaanza kueneza ukabila.
“Mambo hayo tusiyaruhusu kabisa kwa sababu yanaweza kuvuruga amani ya nchi.
“Watanzania tukumbuke umuhimu mkubwa tulionao ni kulijenga taifa kwa kulinda amani na kuitetea na siyo kushabikia watu wanaofanya kazi ya kutaka kuligawa taifa kwa masilahi yao binafsi,” alisema Dk. Shein.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema lengo la uwepo wa mwenge huo wa uhuru ni kumulika nje ya mipaka na kuleta matumaini na amani kwa Watanzania.
Pia aliwahimiza Watanzania wafanye kila linalowezekana katika kupambana na rushwa kwa kuwa ni adui wa maendeleo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, alisema mwenge huo utakapokuwa ukikimbizwa mkoani humo, miradi mbalimbali ya maendeleo itazinduliwa.
Mbio hizo za mwenge zilizinduliwa jana huku kiongozi wake kitaifa akitajwa kuwa ni Juma Hatibu Chumu.