Na Christian Bwaya
FIKIRIA una watoto wawili wanaotofautiana kitabia, mmoja kati yao hana nidhamu. Unapomwambia jambo haonekani kuzingatia. Mwingine ana tabia njema. Unapomshauri jambo ana utayari wa kukupa ushirikiano. Yupi unaweza kuonesha upendo wako kwake kirahisi kuliko mwingine? Ni wazi, utavutiwa na huyu wa pili mwenye usikivu na uelekevu. Ule usikivu wake, uzingativu wake utakuvutia kumlipa upendo na kumtendea yaliyo mema. Moyoni unafanya hivi kwa nia njema.
Lakini kwa yule wa kwanza, asiyesikia na pengine mkorofi, unaamua kumweka mbali na wewe. Humtumi, hushirikiana naye, humletei zawadi kama mwenzake wa pili na pengine hutataka husikia madai yoyote kutoka kwake. Nia yako unapoyafanya hayo ni kumfundisha atambue makosa yake. Hata hivyo, hali kama hii ya kumpendelea mtoto anayefanya vizuri kwa kumfanya awe tofauti na mwenzake asiyefikia matarajio yako kama mzazi inapozoeleka katika familia inaitwa ubaguzi.
Ubaguzi ni kumfanya mtoto ajione hana haki ya kuwa sawa na mwenzake kwa sababu ya upungufu wake kitabia au kiutendaji. Kwa mfano, unamhamisha mtoto aliyefeli kutoka kwenye shule bora yenye sifa kwenda kwenye shule asiyoipenda kama njia ya kumfundisha kufanya bidii kwenye masomo. Huu ni ubaguzi kwa sababu mwenzake anayefanya vizuri darasani unamwacha aendelee kubaki kwenye shule inayosifika kama motisha kwake ya kujituma.
Ingawa kwa mzazi hili linaweza lisiwe na maana yoyote mbaya, katika macho ya mtoto, huu unaweza kuwa mwanzo wa matatizo makubwa katika familia. Ndani ya mtoto uhamisho huo unaweza kuchukuliwa kama uonevu unaotokana na chuki ya mzazi kwake na si ufaulu mbaya kama anavyofikiri mzazi. Dhana kama hizi za kubaguliwa ni moja wapo ya adhabu mbaya kabisa unazoweza kumpa mtoto. Hisia za kubaguliwa zinajenga chuki kubwa ndani ya mtoto. Madhara yake, kama tulivyoona kwenye makala iliyopita, ni kuzorotesha mawasiliano katika familia.
Ili kuepusha mazingira kama haya yanayoweza kuibua misuguano ya chini chini kati yako na mtoto, ni busara wewe mzazi kufikiria matokeo ya adhabu unazowapa watoto. Jambo la kuzingatia ni kwamba adhabu isiyotolewa kwa uangalifu huweza kujenga dhana mbaya isiyokusudiwa na ikaaminika na mtoto. Dhana hii ikishajijenga ndani ya mtoto, itakuwa kazi ngumu kuing’oa baadae.
Kila inapowezekana, toa adhabu isiyomnyima mtoto huduma na haki zake za msingi anazostahili kama mtoto. Pamoja na matatizo yake, makosa yake, utovu wake wa nidhamu, mtoto wako anabaki kuwa mwanao. Kumpenda, kumtunza, kumhudumia mwanao si hisani bali wajibu. Ndio kusema, mtoto halazimiki kufanya vizuri ili umpe chakula, umtunze kulingana na uwezo wako, umpe huduma anazostahili kama mwanao. Hayo yote ni haki yake awe na nidhamu au la.
Kusema hayo haimaanishi sielewi kuwa wakati mwingine watoto wanaweza kufanya jambo zito linalokukasirisha mzazi. Najua yapo makosa yanaweza kukufedhehesha na kukusononesha mzazi unayetamani mwanao awe na tabia njema. Lakini pamoja na ukweli huo, naelewa pia sifa kubwa ya mzazi ni kuwa na fadhili kwa mtoto.
Kumfadhili mtoto ni kutambua kwamba hata akijisaidia kwenye kiganja, suluhu si kukikata. Fadhili ni kumpa mwanao haki sawa na wengine hata kama hastahili. Kwa kufanya hivyo, unamjenga kuwa sehemu kamili ya familia, hali inayoweza kumfanya ajirudi.