25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

PRESHA YAZIDI KUPANDA VIGOGO ESCROW

Na MWANDISHI WETU,

WAKATI majaji wawili wa Mahakama Kuu waliopata mgawo wa fedha zilizochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow wakijiuzulu nyadhifa zao, hatua hiyo sasa huenda ikawa imehamishia joto kwa wanasiasa, viongozi wa dini na watumishi wa umma ambao nao walinufaika.

Majaji waliojiuzulu ni Profesa John Ruhangisa, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye juzi Ikulu ilitoa taarifa kwa umma ikisema Rais Dk. John Magufuli ameridhia kujiuzulu kwake na Jaji Aloysis Mujulizi pia wa mahakama hiyo, ambaye alijiuzulu Mei 16, mwaka huu.

Baada ya kutajwa kwenye kashfa hiyo, waliokuwa kwenye nyadhifa za kisiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge, waliitwa Baraza la Maadili ya Utumishi wa Umma, ambako baadhi walihojiwa, ingawa hatua zilizochukuliwa hazijawekwa wazi.

Kwa viongozi wa umma, baadhi walifikishwa mahakamani, ingawa wengine kesi zilifutwa zikiwa kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji.

Homa ya walionufaika na mgawo huo wa fedha za Escrow, ilianza kupanda baada ya Serikali kuamua kufufua sakata hilo, lililodhaniwa kuwa limekwisha kwa kuwafikisha mahakamani hivi karibuni vinara wawili.

Vinara hao ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, aliyekuwa pia mwanahisa wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), iliyoletwa nchini miaka 23 iliyopita, James Rugemalira na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Pan African Power (PAP), Habinder Sethi Sigh, waliofikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 19 na kusomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Julai 3, vigogo hao walifikishwa tena kwenye mahakama hiyo na kuongezewa mashtaka sita, yakiwamo ya utakatishaji fedha.

Kwa jumla wake mashtaka 12 waliyosomewa Rugemalira na Sethi Julai 3, ni pamoja na kutakatisha fedha na kuisababisha hasara Serikali ya USD 22, 198,544.60 (Sh 309,461,300,158.27).

Kutokana na hali hiyo, na hatua ya majaji wawili kuamua kuachia nyadhifa zao, ni wazi walionufaika na fedha hizo presha zao zitakuwa zinapanda na kushuka, kutokana na kutojua hatima yao ya ama kuunganishwa au kutounganishwa kwenye kesi inayoendelea mahakamani.

Miongoni mwa viongozi wa kisiasa na umma ambao wakati fedha hizo zinatolewa walikuwa madarakani, ama kwa namna moja ama nyingine walihusika kuiingiza IPTL nchini, huenda sasa wakawa kwenye wakati mgumu zaidi.

Hii ni kwa sababu baada ya kutajwa kwenye kashfa hiyo, waliishia kwenye Baraza la Maadili na wengine kesi zao zikifutwa baada ya kufika mahakamani.

Novemba 2014, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliwataja vigogo wa Serikali, wanasiasa na viongozi wa dini watatu walionufaika na Akaunti Tegeta Escrow, huku ikishindwa kuweka wazi walionufaika na sehemu ya fedha zilizodaiwa kuchotwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilipokuwa akaunti hiyo na kupelekwa Benki ya Stanbic.

PAC wakati ikisema Rugemalira aliwagawia baadhi ya watu fedha kupitia akaunti zao walizofungua kwenye Benki ya Mkombozi, ilisema sehemu ya fedha nyingine iliwekwa Stanbic, ambako watu walizichota kwa mifuko ya plastiki, maarufu kama sandarusi.

 WALIONUFAIKA NA MGAWO WA RUGEMALIRA

Akisoma maoni ya PAC, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye wakati huo alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, aliwataja waliochukua fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, kiwango walichopokea katika mabano kuwa ni Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (Sh bilioni 1.6) na Mbunge wa Muleba ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Sh bilioni 1.6).

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh milioni 40.4), aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh milioni 40.4), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga, Paul Kimiti (Sh milioni 40.4) na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk. Enos Bukuku (Sh milioni 161.7).

Kwa upande wa majaji, ni Jaji Profesa Ruhangisa (Sh milioni 404.25) na Jaji Mujulizi (Sh milioni 40.4).

Kwa upande wa watumishi wa umma, Zitto alisema aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko, alipewa Sh milioni 40.4, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel ole Naiko (Sh milioni 40.4) na Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh milioni 80.8).

“Kwa upande wa viongozi wa dini ambao waliingiziwa fedha na Benki ya Mkombozi, ni Askofu Methodius Kilaini (Sh milioni 80.9), Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh milioni 40.4) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh milioni 40.4),” alisema Zitto.

Alisema Rugemalira alipata mgawo wa Dola za Marekani milioni 75 kutoka katika fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na kuzigawa kwa watu mbalimbali.

Rugemalira, ambaye alikuwa na hisa 3 kati ya 10 za kampuni ya IPTL, alichukua kiasi hicho cha fedha na kukipeleka katika Benki ya Mkombozi, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki.

 KUHUSU MAJAJI

Mwaka jana katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, alinukuliwa na gazeti hili akisema dawa ya kumaliza mambo ni kuwa wazi.

“Suala la majaji waliohusishwa katika Escrow limeshaletwa katika tume, lipo na taratibu zinaendelea,” alisema Katanga.

Naye Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Enzeel Mtei, alinukuliwa katika maadhimisho hayo ya Wiki ya Sheria akisema tume hiyo iliundwa na wajumbe sita.

Alisema ilikuwa na jukumu la kumshauri rais juu ya uteuzi wa Jaji Kiongozi au majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu na kutokuwa na uwezo kwa watendaji hao.

Majukumu mengine ni kuchambua malalamiko dhidi ya majaji hao na kuchukua hatua za utawala dhidi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi au Jaji na hatua zilizoainishwa katika Katiba.

Alisema kwa majaji wanaokwenda kinyume na maadili, tume huchunguza madai hayo na kupeleka mapendekezo kwa rais kwa ajili ya uamuzi.

 VIONGOZI WA KISIASA

Machi 2015, Ngeleja alidai mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwamba msaada aliopewa na Rugemalira hauna tofauti na  mingine aliyowahi kupokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kama vile Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa na Yusuf Manji.

“Msaada niliopewa na Rugemalira hauna tofauti na misaada mingine wanayopewa wabunge wenzangu au misaada mingine niliyowahi kupokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kama vile akina Mengi, Bakhresa, Yusuf Manji, mashirika ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF, PSPF, NHC, NHIF na benki ya CRDB na NBC,” alisema.

“Sijawahi kuomba wala kupokea fadhila za kiuchumi kutoka kwa Rugemalira, isipokuwa kama Mbunge wa Sengerema kwa nyakati tofauti kama wabunge wengine wanavyofanya, niliomba misaada ya kiuchumi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa jimbo langu na Watanzania kwa ujumla,” alisisitiza.

 CHENGE

Kwa upande wake, Chenge, alidai mbele ya baraza hilo kuwa amri ya Mahakama Kuu inazuia mamlaka zozote kujadili au kulifanyia kazi suala lolote linalohusu kashfa ya akaunti hiyo.

Kutokana na hali hiyo, hakuhojiwa na baraza likatenga siku moja kuipitia amri ya zuio hilo la mahakama kabla ya kutoa uamuzi juu ya pingamizi hilo.
Baada ya kuipitia, mwenyekiti wa baraza hilo aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, Jaji mstaafu Hamisi Msumi, alisema zuio hilo la mahakama halilihusu wala kulizuia baraza kufanya kazi yake, isipokuwa Bunge, wasaidizi wa sheria au mawakala wanaofanya kazi za kisheria.

Baada ya Jaji Msumi kutoa uamuzi huo, Chenge hakukubaliana nao na kusema anakata rufaa kwenda Mahakama Kuu kuomba mwongozo juu ya kuendelea kujadiliwa suala hilo au la.“Sitaki kubishana na maamuzi yaliyotolewa na baraza, lakini nafikiri wanasheria wa baraza hili wangejaribu kwenda masjala kusoma zaidi, naamini wangeelewa hili ninalozungumza. Ninakubaliana na maamuzi, lakini naomba nikate rufaa, niende Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata mwongozo zaidi juu ya suala hili,” alisema Chenge.

 TIBAIJUKA

Kwa upande wake, Profesa Tibaijuka alikiri kuomba fedha hizo, lakini si kwa masilahi yake binafsi, bali ni kwa ajili ya Taasisi ya Barbro Johannson Girls Trust.
Alipoulizwa sababu ya kutoa fedha hizo kwenye akaunti yake katika Benki ya Mkombozi na kuzitumia katika kazi zake binafsi, alisema fedha hizo ziliingizwa tarehe 12 mwaka 2014 na kuanza kufanya miamala binafsi tarehe 14, ambapo Sh milioni mbili alizitumia kununua hisa Makongo Parish.

Profesa Tibaijuka alisema baada ya hapo alitoa Sh 400,000 na kununua hisa Kijiwe Parish na siku hiyohiyo alitoa Sh milioni 10 ambazo hazina maelezo sahihi.
“Sh milioni 10 nilitoa kwa ajili ya kununua mboga kwa sababu fedha hizo ni zangu.

“Nashangaa kuambiwa nimevunja maadili, kwanza fedha hizi ni ndogo japo ni hela, lakini mimi sina shida na fedha hizi.

“Mimi ni mstaafu wa miaka mingi, nina pensheni ya kila mwezi, sina shida na fedha hizo, ndiyo maana hata hizo fedha zilizobaki kwenye akaunti hiyo sijaenda kuziangalia kwa sababu sina shida za hivyo,” alisema.

 VIONGOZI WA DINI

Hadi sasa haijulikani kama kuna hatua zozote zimechukuliwa kwa viongozi wa dini waliotajwa kwenye sakata hilo.

 VIONGOZI WA UMMA

Baadhi ya wafanyakazi wa umma, wakiwamo wa  Mamlaka ya Mapato (TRA), Msajili wa Vizazi na Vifo (Rita), na Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kesi zao zinaendelea, huku wengine zikiwa zimefutwa ama kumalizika.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Sina uhakika kama mmoja ya kazi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kufanyia mapitio ya mara kwa mara sheria za nchi (hasa zile za jinai) na kutoa mapendekezo ya kuzirekebisha pale anapobaini mapungufu.
    Nasema haya kwa sababu ya mchezo ambao Mheshimiwa Chenge, pamoja na wengine (i.e. Lema, Lisu, Kubenea, Mdee, Manyika, n.k.) wamekuwa wakiufanya katika kujitenga na tuhuma dhidi yao juu ya masuala mbalimbali.
    Sijui!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles