PATRICIA KIMELEMETA Na NORA DAMIAN
MAWAKILI wanaomtetea mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, wameiomba Mahakama Kuu kuingilia kati kutokana na kukamatwa na kushikiliwa isivyo halali kwa mfanyabiashara huyo na wenzake.
Manji na wenzake, Deogratius Kisinda na Thobias Fwere wanashikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam tangu walipokamatwa wiki iliyopita.
Mawakili hao waliwasilisha maombi kwa hati ya dharura wakiomba mahakama hiyo itoe amri ya kuwataka walalamikiwa wapelekwe mahakamani aweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Katika hati ya kiapo ya kuunga mkono maombi hayo, Wakili Hudson Ndusyepo, alidai walalamikaji walikamatwa na kushikiliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO) kwa nyakati tofauti.
Alidai, Kisinda alikamatwa Juni 30, mwaka huu, saa 10 jioni wakati Manji na Fwere walikamatwa Julai Mosi, mwaka huu saa 5 asubuhi katika jengo la Quality Centre na tangu siku hiyo wanaendelea kushikiliwa.
Wakili hiyo alidai alifahamishwa na ZCO kwamba walalamikaji walikamatwa na kushikiliwa kwa tuhuma za kutenda kosa linalohusiana na sare za jeshi ambazo zilikutwa kwenye ghala la Quality Motors Limited.
Alidai kukamatwa kwa wateja wake si halali kwa sababu kosa lililosababisha kukamatwa na kushikiliwa kwao linahusiana na Kampuni ya Quality Motors ambayo inaongozwa na wakurugenzi wengine na si wateja wake.
Alidai hata baada ya Manji na wenzake kukamatwa, aliomba dhamana lakini alikataliwa kwa sababu ambazo hazijajulikana.
Wakili alidai kuwa tangu wakamatwe hadi sasa zaidi ya saa 48 zimepita na ZCO amekataa kuwapa dhamana.
Alisema kwa uelewa wake wa sheria, kitendo cha wateja wake kushikiliwa kwa zaidi ya saa 24 na kunyimwa dhamana ni kinyume cha sheria na si sahihi.
Wakili Ndusyepo alidai kama mahakama haitayakubali maombi yao wateja wao wataendelea kuingiliwa uhuru wao bila sababu za msingi.
Aliiomba kuingilia kati na kutoa maelekezo kama inavyostahili.
Maombi hayo yamepangwa kusikilizwa kwa Jaji Lugano Mwandambo ingawa siku haijapangwa.
Katika hatua nyingine, taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata jana zilisema Manji alikimbizwa juzi jioni na kulazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, baada ya kujisikia vibaya.
“Wakati akiwa pale kituoni akiendelea na mahojiano, aliwaambia askari wetu anajisikia vibaya na kuomba apelekwe hospitali…ndiyo akapelekwa Taasisi ya Kikwete ambako yupo mpaka sasa.
“Hatuwezi kujua tatizo linalomsumbua sasa, maana hiyo ni siri ya daktari na mgonjwa wake,” kilisema chanzo chetu.
Juhudi za kumpata Kaimu Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa kwa vile simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Mwisho.