31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KAMPUNI YA ACACIA YATINGA KORTINI

KAMPUNI ya Acacia imewasilisha notisi ya kimahakama kuiita Serikali ya Tanzania kwenye Baraza la Usuluhishi ambalo lina nguvu sawa na Mahakama ya Kimataifa.

Taarifa iliyotolewa jana na Acacia, ilieleza notisi hiyo imewasilishwa kwa niaba ya Bulyanhulu Gold Mine Limited (BGML), ambayo ni mmiliki wa mgodi wa Bulyanhulu na Minerals Limited (PML), mmiliki wa mgodi wa Buzwagi.

Acacia imesema kuwa imetoa notisi hiyo kulingana na mchakato wa utatuzi wa migogoro uliokubaliwa baina ya Serikali ya Tanzania, BGML na PML kwa mujibu wa masharti ya mikataba yao.

Notisi hiyo inahusu mgogoro unaoendelea kati Serikali na Acacia.

Katika taarifa hiyo walieleza kuwa wito huo unalenga kulinda masilahi yao, jambo linaonyeshaka kwamba hawana imani ya mazungumzo yaliyotangazwa.

Taarifa hiyo imesema pamoja na kutolewa kwa notisi hizo, wanabakia na mtazamo kwamba azimio kwa njia ya mazungumzo ni mwafaka bora kwa migogoro iliyopo sasa na kwamba migodi yote mitatu itaendelea kufanya uchimbaji.

“Serikali ya Tanzania imeliarifu Shirika la Barrick Gold (Barrick) kwamba katika wakati huu ingependa kuendelea na majadiliano yao na kwa hivyo Acacia haitashiriki moja kwa moja katika majadiliano haya pindi yatakapoanza.

“Azimio lolote ambalo linaweza kufikiwa kama matokeo ya majadiliano hayo litapaswa kupata idhini ya Acacia na kampuni itafanya kazi na Barrick kama inavyohitajika kuunga mkono majadiliano hayo.

“Migodi yetu yote mitatu inaendelea kufanya kazi kulingana na taarifa zetu za awali na tutatoa taarifa zaidi juu ya maendeleo yoyote, ikiwa ni pamoja na sheria iliyopendekezwa ya madini, pindi mchakato wa sheria utakapokamilika,” ilieleza taarifa hiyo.

Hatua hiyo ya Acacia imekuja huku suluhu ikisakwa kwa njia ya mazungumzo kumaliza mzozo wa mchanga wenye madini (makinikia), baina ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold Corporation kupitia mshirika wake Acacia.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa mazunguzo hayo yanaweza kuwa si tu magumu, bali yakachukua muda mrefu kupata suluhisho.

Mazingira hayo yanatokana na uzoefu wa kampuni hiyo katika historia ya kimataifa kuonyesha kwamba inatumia umakini wa hali ya juu kulinda masilahi yake pale panapotokea nafasi ya mazungumzo ya kutafuta suluhisho la jambo lolote linalohusu uwekezaji wake katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa kutambua changamoto mbalimbali za kiuwekezaji, kampuni hiyo ina bodi maalumu inayohusika na ushauri wa kimataifa, ambayo inaundwa na watu wenye ubobezi katika maeneo mbalimbali, hasa ya kisiasa na jiografia.

MTANZANIA ilichunguza mwenendo wa kampuni hiyo kuhusu aina ya makubaliano yake ya kiuwekezaji na nchi mbalimbali na kubaini kuwa imekumbana na misukosuko mikubwa ya uwekezaji wa madini.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kupitia vyombo vya habari vya kimataifa na  kwenye mtandao wa intaneti, umebaini kuwa hata ule mgogoro wake wa mkataba wa uchimbaji wa madini  na taifa la Dominica lenye takribani watu milioni 10, mazungumzo ya kutafuta mapatano yalidumu kwa miezi minane.

Inaelezwa kuwa Serikali ya Dominica iliipa mkataba Kampuni ya Barrick Gold Cooperation wa kuchimba madini kwa miaka 30 katika mgodi wa Pueblo Viejo, ambao ni moja ya migodi mikubwa ya dhahabu duniani.

Katika uwekezaji huo, kampuni ya Barrick Gold Cooperation inamiliki asilimia 60 na Goldcorp asilimia 40. Kampuni zote mbili zinatoka nchini Canada.

Msingi wa mgogoro baina ya Serikali ya Dominica na Barrick ni mkataba ambao ulielekeza kuwa nchi hiyo ingenufaika kwa asilimia tatu tu ya faida ya dhahabu inayochimbwa.

Juni 16, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John Thornton, ilibainika kuwa nchi hizo zilipita njia kama hii hii inayopitia Tanzania kwa sasa.

Siku chache baada ya mazungumzo hayo, Acacia Mining Plc, ilisema kuwa Mwenyekiti wa Barrick, Profesa Thornton ambaye alifanya mazungumzo na Rais Magufuli, Ikulu Dar es Salaam hakusema kama watalipa malimbikizo ya kodi.

Acacia ilitoa ufafanuzi huo katika mkutano wa wanahisa baada ya mwanahisa mmoja kutaka kujua kama ni kweli kampuni hiyo ilitoa ahadi ya kulipa malimbikizo ya kodi za nyuma ambazo haikulipa kwa Serikali ya Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, aliwaambia wanahisa kupitia mkutano kwa njia ya simu kutokea makao makuu ya kampuni hiyo London, Uingereza kuwa mwenyekiti huyo hakuzungumza chochote kuhusu kulipa kodi.

Machi mwaka huu, Serikali ilizuia makontena zaidi ya 200 kwenye Bandari ya Dar es Salaam kuchunguza mchanga wa madini (makinikia) ambao ulikuwa unasafirishwa nje ya nchi kwenda kuchenjuliwa.

Mchanga huo ulikuwa ni mali ya ya Acacia, ambayo ni kampuni mshirika wa Barrick.

Baada ya zuio la mchanga huo, Rais Magufuli aliteua kamati mbili kuchunguza makinikia hayo, ambapo kamati ya kwanza iliyokuwa inaundwa na wanasayansi ilibaini kiasi kikubwa cha madini ambayo yangeibwa kupitia mchanga huo.

Kutokana na hali hiyo, Acacia ilieleza kusikitishwa na kushangazwa na matokeo ya ripoti ya pili ya mchanga wa madini iliyowasilisha kwa Rais Magufuli.

Taarifa iliyotolewa na Acacia kupitia tovuti yake, saa chache baada ya ripoti hiyo kusomwa na Mwenyekiti wa kamati, Profesa Nehemiah Osoro, ilisema kampuni hiyo imesikitishwa na ripoti ya kamati ambayo matokeo ya uchunguzi wake ni historia katika uchumi wa nchi hii na mambo ya sheria ya kusafirisha mchanga wa madini.

Kwa mujibu Acacia, ripoti ya pili imejikita katika matokeo ya ripoti ya kwanza iliyotolewa Mei 24, mwaka huu ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiipinga vikali.

Taarifa hiyo inasema ripoti hiyo ilihusisha matokeo ya sampuli za makotena 44.

 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles