Na Shermarx Ngahemera,
SERIKALI ina mipango mikubwa ya kuruhusu uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje kwa kuruhusu hisa za makampuni ya simu na migodi kununuliwa na yeyote aliyenacho na popote alipo ili kufanikisha mitaji inayotakikana na hata katika Toleo la mwanzo (IPO) kwa uwekezaji mkubwa nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, anashughulikia mabadiliko hayo kufuatia uwekezaji katika IPO ya Kampuni ya Vodacom Plc kuchukua muda mrefu usiotegemewa na kukosa maelezo ya kina hadi sasa.
Kampuni za Airtel na Tigo ambazo wanatakiwa kisheria kujiunga kwa sharti ikiwa itifaki na masharti yakizingatiwa, ziko kwenye mlolongo wa kwenda mbele kujiunga kwa sheria ila Tigo ina matatizo wakati Airtel njia nyeupe.
Ufunguzi wa milango ya uwekezaji kwa wote ni mabadiliko makubwa ya kisera na kiutendaji ili kufanikisha haraka mahitaji ya Taifa ya mitaji na kuongeza nguvu kuelekea uchumi wa viwanda.
Serikali imebadilisha msimamo wake huo wa kiuchumi ili kulifungua Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) litafute mitaji bila kikwazo kutoka ulimwengu mzima na hivyo kudai marekebisho mengi ya sheria na sera za fedha na uchumi nchini.
“Nia ni kupata wawekezaji kutoka Afrika Mashariki, Diaspora (ughaibuni) na masoko ya mitaji duniani kwenye matoleo ya awali (IPO) zaidi ya ilivyo sasa ikiwaruhusu wananchi tu,” alisema Waziri wa Fedha wakati wa kufunga hotuba ya mawasilisho ya bajeti bungeni.
Serikali itafanya mabadiliko katika Sheria ya Elektroniki, Posta na Mawasiliano (EPOCA) ya mwaka 2010 ili wawekezaji wa aina yote washiriki katika shughuli za uchumi hapa nchini hususani katika matoleo ya mwanzo ya hisa (IPOs). Mabadiliko hayo yanategemewa kufanywa kwenye Sheria ya Fedha ya 2017 ili iendane na uuzaji wa hisa za Airtel na Tigo kwa mafanikio.
Serikali imepanga kuwa na bajeti ya Sh trilioni 31.7 kwa mwaka 2017/18, ikiwa ni matumizi makubwa na ina mipango ya kutekeleza azma yake ya kufanya uchumi unamilikiwa na wananchi na hivyo migodi na shughuli za madini kuachia asilimia ya hisa zake kwa kiasi cha asilimia 25 kwa umma wa Tanzania walionazo kuwekeza DSE.
Watanzania walioko nje ya nchi sasa wanaweza kushiriki katika ununuzi wa hisa za awali wa kampuni za simu za Airtel Tanzania na Tigo ambazo ziko mbioni kujiorodhesha.
Mahitaji ya fedha za mitaji katika sekta za mawasiliano na madini ni makubwa na hivyo Serikali imeona ni bora ifungue milango kwa wote ili waweze kugharamia shughuli hizo.
Mabadiliko yanalenga kufanya mambo yaende haraka badala ya kusubiri Watanzania wa ndani pekee ambao wameonesha kukosa uwezo mkubwa.
Uzoefu kutoka Vodacom Tanzania Plc, IPO, hatima yake haijajulikana miezi miwili baada ya kufunga mauzo ya hisa.
Vodacom ilikuwa inahitaji uwekezaji wa Sh bilioni 476 kutokana na mauzo ya hisa milioni 560 na kila hisa ikiuzwa Sh 850 na kuna kila dalili kuwa mauzo hayakwenda vizuri hata baada ya kuongezewa muda wa mauzo.
Kuzuia mambo yasiende kombo imebidi Serikali ifanye mabadiliko makubwa kwa kuifungua nchi na kuachana na masharti ya uasilia wa mitaji.
Shauku iliyozimwa ya hisa za Vodacom ni kitendawili kikubwa cha kibiashara kwani kinaleta jakamoyo kwa masuala mengi ya uwekezaji hasa huo wa shuruti kwa kampuni ambazo kimsingi zenyewe hazikuhitaji bali zinatekeleza wajibu wa kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc, Ian Ferrao, alieleza kwa kifupi kuwa kampuni yake inasubiri tu kuruhusiwa kutoka Mamlaka ya Hisa, Dhamana na Mitaji (CMSA), kwani wawekezaji wapya zaidi ya 40,000 walijiunga nao kwenye IPO.
Juni 26, mwaka huu Baraza la Mawaziri lilifanya kikao Ikulu Dare Saalam na inasemekana suala hilo lilikuwa katika ajenda.
Dk. Mpango alieleza bungeni kuwa kama kampuni ikitoa toleo la mwanzo (IPO) na haikufanikiwa kupata kiasi kinachotakiwa, wizara ya sekta husika itahitajika kutoa maelezo na kutoa mwongozo kwa kampuni hiyo namna gani itapata fedha zinazohitajika kufikia hitaji hilo ili kuridhia mahitaji ya kisheria kabla ya kufikiria hatua ya kwenda mbele.
Airtel iko mbioni kwa mwendo kasi kujiorodhesha DSE baada ya wamiliki wake, Serikali na Bharti Airtel kukubali kila upande kuachia asilimia 12.5 ya hisa ili umma uzinunue.
Kampuni ya pili ya mawasiliano kwa ukubwa na umaarufu, Mic Tanzania Limited au Tigo, imekamilisha mipango ya kujiorodhesha ila ina kesi ya dawa ya umiliki mahakamani na hivi karibuni iliruka kihunzi cha kwanza baada ya majaji kung’ang’ania kuendelea kusikia kesi hiyo kinyume na mahitaji ya mdai.
Alipoulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu hatima ya usajili wa kampuni kwenye DSE, Mkuu wa Habari za Kiteknolojia wa Tigo, Jerome Albou, alisema suala hilo liko mahakamani na hawezi kusema litakwisha lini kwani kesi inahusu umiliki na hivyo ni vigumu kwao kwenda sokoni wakiwa na matatizo na hivyo watu wasubiri matokeo ya kesi hiyo.
Albou alieleza kuwa kampuni yake mwaka jana ilitumia dola milioni 75 kuboresha miundombinu yao na mtandao kwa kuanzisha huduma ya 4G kwenye miji 23 nchi nzima kama walivyopanga awali.
Wakati huo huo, Maxcom Africa maarufu kama MaxMalipo, imepata ruhusu na kibali cha CMSA kubadili jina lake na kutumia PLC wakati kampuni nyingine za mawasiliano ziko mguu sawa katika hatua mbalimbali za kujiorodhesha DSE kwa mujibu wa Sheria ya EPOCA ya mwaka 2010 na Marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2016.
Sheria inataka kampuni za simu zote kujiorodhesha DSE ili hisa zake kwa asilimia 25 ziuzwe kwenye soko hilo ili wananchi waweze kununua na kumiliki sehemu ya biashara hizo.
Toleo la IPO linaonesha kukwama kwani hisa hadi leo hazijapelekwa kwenye soko la upili licha ya IPO kufungwa muda mrefu na kuleta sintofahamu kwa wawekezaji wake na kutishia kuvuna haraka faida kwa wale waliokopa kununua hisa hizo na wale waliosogeza hela za taasisi ili watengeneze chochote kwa muda mfupi.
Airtel au Bharti Airtel inamilikwa na mfanyabiashara wa India, Mittal Ambani kwa asilimia 60 na Serikali ya Tanzania hisa asilimia 40. Taarifa zinasema wanahisa hao wamekubaliana kuwa kila mmoja aachie asilimia 12.5 kuuzwa DSE .
Ambali alikuja mwenyewe nchini na jina walikubaliana liwe Airtel Company Plc na limeshasajiliwa na BRELA na hivyo kukidhi haja ya ushiriki na kinachosubiriwa ni uchapishaji wa Matarajio ya Toleo (IPO Prospectus) ambayo inatayarishwa Airtel, yatapitishwa kwanza na DSE, halafu CMSA ambayo ndio itakayotoa kibali cha uuzaji na ununuzi wa hisa hizo sokoni .
Ni taratibu ndefu lakini ni kwa usalama wa wale wanaowekeza mitaji. Kampuni husika zinatakiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha faida ili wanahisa wapate gawio.
“Yote haya ni kumlinda mteja anayenunua hisa hizo kuhakikishiwa kupata faida ingawa biashara ina hatari (risks) nyingi kutokana na mwenendo wa soko husika,” anasema mtoa habari DSE.
Hali hiyo imetokea kwenye mauzo ya Hisa za Vodacom Plc ambayo pamoja na kusubiriwa kwa hamu kubwa na wawekezaji, matarajio ya kampuni hiyo hayakwenda vizuri hadi muda wa ziada ulipoongezwa.
Vodacom matarajio yake hayakufikiwa kirahisi kwenye Toleo la awali (IPO) ya Sh bilioni 476 sawa na $ milioni 213.
Hisa lulu za Vodacom
Ingawa picha kamili ilikuwa bado kutolewa hesabu na hatima ya mauzo hayo, kulijaa matumaini kwani vikwazo vya awali vilitolewa na wengi kupata uwezo wa kununua hisa hizo za kihistoria katika soko kwa ukubwa wa toleo la mauzo, kiwango na kiasi kilichosajiliwa kama bei ya awali ya hisa.
Isitoshe si kawaida kwa hisa za awali DSE kuongezewa muda wa mauzo yake kabla ya kuorodheshwa, tayari ishara zilionesha kwamba mambo si bambam.
Kwa mujibu wa waraka wa matarajio (prospectus), Vodacom Tanzania Plc ina thamani ya Sh trilioni 1.9.
Mkurugenzi Mtendaji wa Orbit Securities, ambao ni washauri wa uwekezaji na wasimamizi wakuu wa mauzo ya hisa za Vodacom, Laurean Malauri, alionyesha imani yake kufanikisha uuzaji huo ingawa imekuwa kwa mbinde.
Malauri amekubali kwamba ukubwa wa thamani ya hisa hizo pamoja na kukosekana kwa ukwasi miongoni mwa Watanzania ambao ndio waliolengwa kwenye mauzo hayo ni changamoto za msingi.
“Serikali ilitoa upendeleo pekee kwa Watanzania tu kunufaika na hisa za kampuni za simu katika matoleo ya msingi (primary market) na kuzuia wawekezaji kutoka nje ya nchi ambao wanachangia kiwango kikubwa kwenye biashara ya hisa DSE ikiwamo wale kutoka EAC na SADC,” alibainisha Malauri.
Hivyo, mpango huo mpya ulioghairi azma ya awali ya Serikali ni mwafaka kwani unatoa nafasi wawekezaji wa nje kugharamia maendeleo ya nchi badala ya kuwa wenyewe pekee.
Mabadiliko hayo ya sera za mitaji kama Dk. Mpango alivyosema yatazuia mkwamo, kwani bado kuna zaidi ya kampuni nyingine 8 za simu na mawasiliano pamoja na migodi mingi zinatakiwa kuuza hisa zake DSE. Swali muhimu ni kuwa fedha zitatoka wapi? Tusipende sana kujikaanga kwa mafuta yetu wenyewe.