NA RAMADHANI HASSAN,
MBUNGE wa Kibiti, Ally Ungando (CCM), ameiomba Serikali kutokana na mauaji yanayoendelea kutokea jimboni humo ipeleke umeme kwani kwa sasa ni giza.
Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, Ungado alidai kutokana na mauaji yanayoendelea katika jimbo lake, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka umeme katika Jimbo hilo kwakuwa usiku kunakuwa na giza.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medad Kalemani, alisema Serikali itapeleka umeme wa Rea katika vijiji vyote vikiwemo vijiji vilivyopo katika Jimbo la Kibiti.
Katika swali la Msingi, Mbunge wa Mbogwe, Augustino Masele, aliuliza ni lini Serikali itaongeza usambazaji wa huduma za miradi ya Electricty V na Rea kwa wananchi wengi walio tayari kulipa gharama za kufungiwa umeme katika nyumba zao hususan katika Mji wa Lulembele na Masumbwe?
Akijibu swali hilo, Dk Kalemani alisema utekelezaji wa mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza kwa nchi nzima tangu Machi mwaka huu.
Dk. Kalemani alisema mradi huo utajumuisha vipengele vitatu ambavyo ni Densification, Grid Extension na Off-Grid Renewable ambayo inalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme, ikiwa ni pamoja na vitongoji, taasisi za umma, mashine za maji visiwa.
Alisema Miji ya Lulembela na Masumbwa imewekwa katika utekelezaji wa Mradi wa Rea Awamu ya Tatu utakaokamilika mwaka 2020-2021.
“Kazi ya kupeleka umeme katika miji ya Masumbwe unajumuisha vijiji vya Budoda, Ilangale, Nyakasaluma na Shenda na Lulembela unajumuisha vijiji vya Bugomba, Kabanga, Kashelo na Nyikonge na maeneo mengine itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa Kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 38.7,” alisema.