Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WADAU wa Bandari wamelalamikia itifaki iliyofanywa na uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kutothamini mchango wao na kushindwa kuwatambulisha kwa Rais Dk John Magufuli alipoweka jiwe la msingi kwa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Wakizungumza jana, walisema walitarajia ziara ya rais ilikuwa ya kutambua umuhimu wao na namna wanavyochangia uchumi wa nchi.
Mmoja wa wadau hao, John Mfaume, alisema walishangaa kutotambuliwa mahali popote na hotuba ya TPA iliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu, Deusdedit Kakoko.
Alisema wadau hao ni pamoja na Freight Forwarders Association (TAFFA), Tanzania Shipping Agents Association(TASAA), Tanzania Truck Owners Association (TATOA), Dry ports Association (ICDS), Tanzania Shippers Council na wengineo.
“Tumesikitika sana katika hotuba yote ya Mkurugenzi Mkuu mbele ya Rais, hakuna mahali alipoeleza kwa kina mchango wetu wala kututaja kwamba tupo kwenye tukio hilo.
“Hata alipotoa heshima ya meza, wakati anaanza hotuba yake kwa Rais, Kakoko hakututambua kwa kututaja kama wadau muhimu wa bandari.
“Sijui kama alitusahau lakini moja kwa moja ni kutothamini mchango wetu kwa sekta hiyo muhimu.
“Sisi ndiyo wadau muhimu tunaofanya kazi kila siku na TPA, inapokuja shughuli kama hiyo, tunashindwa hata kutambuliwa kuwapo kwetu kwa kututaja tu kwenye hotuba yake Rais wetu naye atambue kwamba na sisi tupo na tunatoa mchango kwa sekta hii muhimu, inatuvunja moyo,”alieleza mmoja wa wadau hao kutoka TAFFA.
Mdau huyo alisema mafanikio yote ya bandari likiwamo hili la upanuzi linaloendelea misingi yake imeanzia mwaka 2009 ambako wadau hao wameshiriki kuasisi na kutoa mapendekezo ya maboresho mengi ya bandari likiwamo la upanuzi.