27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 7, 2022

Contact us: [email protected]

MDEE: WAZAZI NENDENI MAHAKAMANI

MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, amewataka wazazi ambao watoto wao waliopata mimba watanyimwa fursa ya kuendelea kusoma, waishtaki Seikali kwa sababu Katiba inawalinda.

Kauli hiyo ya Mdee imekuja ikiwa ni wiki chache tangu Rais Dk. John Magufuli, alipoagiza kuwa katika utawala wake hakuna mwanafunzi ambaye atapata mimba akarudi shuleni kuendelea na masomo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mdee alisema kauli hiyo ya Rais Magufuli ni ya kushangaza kwa sababu Tanzania iliridhia mikataba mbalimbali ikiwepo haki ya kupata elimu.

“Kama kuna mzazi ananyimwa haki ya kumrudisha mtoto wake shule baada ya kupata mimba, anayo haki ya kuishtaki Serikali na akashinda kwa sababu Katiba inawalinda.

“Nafahamu Rais ana mfumo dume hii imeonesha kwenye uteuzi wake, ila sikujua kama anawachukia hadi wasichana yaani msichana akipata mimba shule, ndoto zake zinazimwa wakati wengine walibakwa.

“Na kama Rais anataka hizo kauli zake anazotoa ni sheria, apeleke bungeni ili iwe sheria lakini mikataba inayotetea hilo ipo na imeshasambaa,”alisema.

Alisema hata katika hotuba yao ya kambi ya upinzani bungeni walisisitiza sera ya kurudisha watoto shule baada ya kupata mimba.

“Hata katika vikao vyetu vya Wabunge Wanawake (TWPG), tulielewana hii sera ya watoto kurudi shule baada ya kupata mimba, sasa huwezi kujua kauli iliyotoka juu kwa sababu tuligawanyika tena na baadaye Waziri wa Afya akasema mjadala umefungwa.

“Sasa sisi hatuwezi kufungwa midomo kwa sababu hatukubaliani na kauli hizi kwa sababu si sheria. Lazima tukemee tabia ya hii, haiwezekani kauli ya Rais iwe sheria kwa sababu hii nchi inaongozwa na Katiba. Kama nchi tumeingia kwenye mikataba ambayo baadaye inaingizwa kwenye Katiba,”alisema Mdee.

Pamoja na mambo mengine, alisema Tanzania iliingia Mkataba wa Uondoshaji wa aina zote za ubaguzi mwaka 1979.

‘Ibara ya 10 (F) ya mkataba huo inazitaka nchi wanachama kuhakikisha, inachukua hatua dhidi ya walioacha shule na kuwarudisha shule na mkataba huu ulisainiwa mwaka 1981.

Alisema inawezekana Rais aliteleza hivyo si dhambi akijirudi kwa kuwa ametoa kauli hiyo kama vile watoto wanaopata mimba wamefanya makosa ya kijinai.

“Kuna petition imeanza kusainiwa Watanzania tuungane na wanaharakati ambao wanatetea sera hiyo ya watoto kurudi shule baada ya kupata mimba waingie kwenye mtandao wa www.change.org wasaini na ikishaungwa mkono kuna mkakati wa kuishtaki Serikali,”alisema Mdee.

Alizitaka halmashauri zote zinazoongozwa na Chadema zihakikishe zinawasaidia waliopata mimba shuleni kuendelea na masomo.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Watanzania tuwe macho kwa wanawake wapotoshaji kama alivyo huyu Dada Halima mdee. Akiwa mbunge tulitegemea awe na busara na ethics za utanzania, lakini bahati mbaya hayuko hivyo. Huo mkataba anaoutaja kama kweli upo na uko hivyo, basi ni mmoja kati ya mikataba mibovu ambayo ni vizuri ibadilishwe na au ibatilishwe kabisaa. Kama yeye anataka watoto wake wawe hivyo, awafundishe wafanye hivyo, hatumkatazi, ila ajuwe wazazi na waalimu Shuleni wawafundishe watoto wote wa kiume na wa kike maadili mema. Tena ingefaa msichana atakayepata mimba wakati yuko shule, akiisha jifungua naye apelekwe Jela angalau nusu ya miaka aliyohukumiwa mvulana aliyempa mimba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,662FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles