NA OSCAR ASSENGA, TANGA
ASILIMIA kubwa ya wanaume waliomo kwenye ndoa mkoani Tanga ni waoga kuandika wosia wa mali walizonazo kwa hofu ya kujichulia kifo.
Imeelezwa kwa hatua hiyo wanapofariki dunia huziacha familia katika migogoro na wakati mgumu hususan kwa wanaume wenye wake zaidi ya mmoja.
Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa Chama cha Wanasheria wanawake Tanzania Mkoa wa Tanga (TAWLA), Latifa Mwabondo kwenye mdahalo na wadau wa masuala ya ardhi.
Alisema suala la wosia bado ni changamoto kubwa kwa jamii.
Latifa alisema suala la wanandoa kuandika wosia wa mali zao limekuwa na vikwazo vikubwa kutokana na baadhi yao kudhani iwapo wataandika mapema itakuwa ni njia ya kutaka kufariki dunia mapema.
“Pamoja na sisi TAWLA kuhamasisha jamii kuandika wosia kulinda mali zao lakini mpaka sasa zaidi ya wosia 200 zimeandikwa.
“Kati ya hizo, 26 zimendikwa na wanawake katika mikoa tunayofanya kazi lakini kwa Tanga bado ni changamoto kubwa.”alisema Latifa.
Alisema kitendo cha wanaume kushindwa kuandika wosia mapema kinasababisha matatizo makubwa hususan kwa familia zenye wanawake zaidi ya mmoja ambako kila upande huhitaji kunufaika zaidi na mali za marehemu.
Awali, akifungua mdahalo huo, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanasha Tumbo aliwataka wenye ndoa zaidi ya mwanamke mmoja kuwawekea wanawake utaratibu mzuri ambao unaweza kusaidia kuondoa changamoto hizo kwenye jamii.
Mwanasheria wa TAWLA mkoani Tanga, Adolphina Mbekenga alisema imekuwapo changamoto kwa wanawake wanaopigania
haki zao ambao huitwa wenye tamaa ya mali za marehemu.