WASHINGTON, MAREKANI
HATIMAYE Ikulu ya Marekani imethibitisha kuwa Rais Donald Trump atakutana na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, wiki ijayo ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani (G20).
Itakuwa mkutano wa kwanza wa ana kwa ana baina ya viongozi hawa wawili. Mshauri wa masuala ya ulinzi wa Marekani, H.R. MacMaster, alisema bado hakuna mada maalumu uliopendekezwa.
Mapema msemaji wa Ikulu ya Kremlin alithibitisha kuwapo kwa  mkutano huo.
Viongozi hawa wawili wanakutana wakati ambapo Rais wa Marekani anaendelea kukabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia kuzuka kwa shutuma kwamba maofisa wake walitoa siri za ndani za Marekani kwa Urusi kabla ya kuchaguliwa kwake kuingoza Marekani mwaka uliopita.
Aidha, sakata hilo limesababisha kuanzishwa kwa timu ya uchunguzi dhidi ya Rais Trump mwenyewe pamoja na ofisa wake mwandamizi, Jared Kushner ambaye anadaiwa kuwa mtu wa katikati katika sakata hilo akishirikiana na Balozi wa Urusi nchini Marekani, Sergry Kslyak.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema huenda pia suala la vita dhidi ya ugaidi unaoendelea huko Syria likatarajiwa kuzungumzwa.
Nchi hizo zimekuwa zikitofautiana kwa kiwango kikubwa juu ya hatua za kuchukuliwa ili kukomesha mgogoro unaoendelea, ambapo Urusi inaamini Syria bila Rais Bashar Assad haiwezekani, huku Marekani ikitaka rais huyo ang’olewe.