Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
SERIKALI imeanza mkakati wa kupata mbinu mpya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini, hususani magonjwa ya mlipuko, yakiwamo Ebola na Chikungunya.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla wakati akifungua mkutano wa tano wa watafiti ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Alisema pia mkutano huo unalenga kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya afya ambazo ni pamoja na upatikanaji wa fedha za kulipia gharama za matibabu na uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto.
“Zipo changamoto nyingi ambazo hatuwezi kuzimaliza zote kwa pamoja, lakini changamoto kubwa tunazoziona ni magonjwa ya mlipuko, upatikanaji wa fedha na uboreshaji huduma za afya ya mama na mtoto ambapo tunalenga kupunguza idadi ya vifo, hasa vitokanavyo na uzazi,” alifafanua.
Alisema ili kutatua changamoto zilizopo, Serikali inahitaji kupata mbinu mpya na ushauri kutoka kwa wataalamu kupitia tafiti mbalimbali wanazofanya.
Dk. Kigwangalla alisema tafiti zinazofanywa na wataalamu zina umuhimu mkubwa kwani zinasaidia kuiongoza Serikali katika kutunga sera mbalimbali.
“Katika mkutano huu zitawasilishwa mada zipatazo 10 ambazo wataalamu wamezifanyia utafiti, zitajadiliwa na wataalamu watatoa mapendekezo ambayo yatawasilishwa wizarani.
“Sisi (wizarani) kupitia mapendekezo hayo yatakayowasilishwa tunahitaji kujua namna gani tutakavyoweza kupambana na changamoto hizi, nafurahi kwamba tafiti za Muhas zinasaidia mno kuboresha sekta ya afya,” alisema.
Mratibu wa mkutano huo, Profesa Twalib Ngoma, alisema uhaba wa maabara nao ni changamoto inayokabili sekta hiyo, hali inayowafanya wataalamu washindwe kubaini mapema magonjwa mengi.