27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA AWATETEA MASHEIKH UAMSHO

Na ARODIA PETER

-DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemtaka Rais Dk. John Magufuli, kutafakari hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki) maarufu ‘Uamsho’ wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.

Masheikh hao ambao wamefunguliwa kesi ya ugaidi, awali kesi yao ilikuwa ikiendeshwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na baadaye kuhamishiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam inakoendelea hadi sasa.

Lowassa, alisema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini muda mrefu kiasi hicho bila kesi kusikilizwa mahakamani.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyasema hayo juzi  alipokuwa akizungumza kwenye futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Alisema kama masheikh hao wamefanya makosa wapelekwe mahakamani ili haki itendeke lakini kuendelea kuwashikilia ni fedheha kubwa kwa Taifa.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli, ametekeleza ahadi ya vyama Vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuunda Tume  mbili za kushughulikia madini ya dhahabu, hana budi kutekeleza na ahadi yake (Lowassa) kuwatoa kizuizini masheikh hao wa Uamsho.

“Nilipokuwa nagombea urais, nilizunguka nchi nzima nikiahidi kuunda tume ya kuchunguza madini ya dhahabu, bahati mbaya kura zetu walizihesabu vibaya na kutunyima kura zetu, sasa niliposikia bwana mkubwa kaunda tume nikasema naam… Rais ameanza kutekeleza ahadi yetu ya Ukawa.

“Sasa nimwombe aangalie na hili la masheikh wetu, sisemi kwamba hawana makosa, lakini kuwaweka ndani miaka minne bila kesi kuamuliwa ni fedheha kwetu na kwa Serikali pia.

“Nchi gani hii, ina uhuru wa miaka 50, watu wako tena waumini wa dini wanawekwa ndani bila kesi, kwa sababu ya tofauti ya kiitikadi, tuwaombee masheikh wetu wale watoke, lakini na nyinyi masheikh mliopo hapa zungumzeni mfanye nini, msiwe baridi sana, pengine kuna lugha watakayoweza kuwasikia,” alisema Lowassa.

Akizungumzia suala la kuenzi amani ya nchi  aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu wanapotafakari mambo mbalimbali kupitia mwezi Mtukufu wa Ramadhan wakemee jambo hilo ambalo alisema linavurugwa na chuki zikiwamo za kisiasa.

Awali Imamu Mkuu wa Msikiti wa Gongolamboto na Amiri wa Shura ya Maimamu Wilaya ya Ilala, , Sheikh Hassan Abbas,  alimwomba Mbunge Waitara kupeleka kilio chao bungeni kuhusu viongozi hao wa dini wanaosota gerezani bila kesi yao kuamuliwa.

“Nimshukuru Mbunge kwa kutambua katika eneo lake kuna kada mbalimbali za viongozi kujumuika pamoja kuelekea sikuu zetu hizi baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Lakini kuna jambo linatuuma sisi waislam, wakati tunaelekea kula sikuu wenzetu wako mahabusu, kwakweli jambo hili linatuuma sana na tunaomba utufikishie kero hii huko bungeni,” alisema Sheikh Abbas.

Kwa upande wake, Waitara alisema juzi ilikuwa siku maalum ya kujumuika pamoja kula futari na kwamba baada ya kumaliza vikao vya Bunge Julai 2, mwaka huu atakaa nao na kujadili kwa undani kero mbalimbali za wananchi.

“Tunatarajia kumaliza Bunge la Bajeti kati ya Julai 2 au 3, kimsingi nina mambo mengi nitakuja tujadiliane, kuna sheria ambayo imepitishwa juzi bungeni, faini ya utupaji taka ovyo imepanda kutoka 50,000 za awali hadi 200,000 na milioni 1,000,000.

“ Na kwa wenzetu washereheshaji (MC’s) na mama lishe kuanzia sasa wataanza kulipa kodi. Haya mambo muwe nayo makini,” alisema Waitara.

Uamsho

Mwaka 2011 viongozi hao wa Uamsho wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) walikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kusababisha uharibifu wa mali za watu na Serikali na kuhatarisha usalama wa taifa.

Mara kadhaa wamekuwa wakifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto wakishitakiwa kwa ugaidi.

Mbali na kina Farid, kesi za ugaidi zaidi ya 20, zinaendelea mahakamani zikiwahusisha  washtakiwa zaidi ya 60.

Viongozi hao walioshtakiwa ni Masheikh Farid Hadi Ahmed (41), Msellem Ali Msellem (52), Mussa Juma Issa (37), Azzan Khalid Hamdan (48) na Suleiman Juma Suleiman (66).

Wengine ni Khamis Ali Suleiman (59), Hassan Bakar Suleiman (39), Gharib Ahmad Omar (39), Abdallah Said Ali (48) na Fikirini Majaliwa Fikirini (48) wakazi wa mjini Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles