25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

NGO’S ZINAZOTETEA WANAFUNZI WAJAWAZITO KUFUTWA

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA



SERIKALI imesema haitasita kuifutia usajili taasisi yoyote isiyokuwa ya kiserikali (NGO’s) itakayopingana na maagizo ya Rais Dk. John Magufuli, kuhusiana na wanafunzi waliopewa mimba kurudi shuleni.
Pamoja na hali hiyo pia imetangaza msimamo mkali kwa taasisi zinazotetea na kuhamasisha vitendo vya ushoga nchini.

Akizungumza jana mjini hapa wakati wa uzinduzi wa harambee ya ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Bikira Maria Parokia ya Kisasa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema Serikali haitaomba ushauri wala maoni kuhusu suala la ujauzito kwa wanafunzi kwani Rais Dk. Magufuli ameshatoa maagizo ya Serikali.

Katika harambee hiyo Mwigulu alimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambapo alisema mjadala kwa wanafunzi wanaopata ujauzito kwa sasa umefungwa na taasisi yoyote itakayopingana au kubeza agizo hilo la Rais haitasita kufutiwa usajili wake.

“Wakati Rais Magufuli anazungumzia masuala ya mimba (ujauzito) Bagamoyo kuna watu wanaibuka wanapenda sana (mjadala), basi hata maelekezo tunadhania ni Debate wengine wanaosema hivyo ni waumini na wengine wanaopigia kampeni ni waumini lakini nyinyi waumini ni biblia gani inayosema hayo.

“…kwa imani yangu na maandiko ninayopitia yote kwanza yanazuia mimba nje ya ndoa na yote yanazuia ndoa za utotoni, waumini wenzetu ambao wanatokea wanaona mimba zihalalishwe kwa wanafunzi wanasoma ni kitabu kipi na wengine ni kina mama hayo malezi tunatoyataka kuruhusu wanafunzi wafanye mambo hayo msingi wake unatokana na nini,’’ alisema na kuhoji Mwigulu

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema kuwa anaunga mkono kauli ya Rais Dk. John Magufuli kwa asilimia 100 huku akiwataka Watanzania nao wafanye hivyo kwani Serikali imetoa haki kwa kila mtoto kupata elimu bure na atayekosa asikose kisingizie kingine.

“Ameongelea mambo makubwa mawili alipokuwa Bagamoyo la kwanza likiwa na mimba na la pili likiwa la ushoga hili la ushoga linaletwa kwa kivuli cha haki na hili la mimba linataka liletwe kwa kivuli cha haki.

“Hawa wanaotaka haki za mashoga watafute nchi yao inayoruhusu mambo hayo lakini si hapa Tanzania na kama kuna taasisi imesajili katika nchi yetu tukagundua inafanya kampeni hiyo tutaifuta mara moja,” alisema Mwigulu.
Kuhusu mimba kwa wanafunzi alisema. “Serikali haiwezi kuwa na utaratibu huo wa likizo ya uzazi, kwa mimi ninayesimamia idara ya utekelezaji wa maelekezo nizionye taasisi zote zilizokuwa zikifanya kazi ya kutetea watafute shughuli zingine za kufanya.

“Na wale wanaodhani maelekezo ya Rais yalikuwa ni ajenda ya kuzua mjadala atazifutia usajili taasisi hizo. Maelekezo na sio ajenda ya mjadala na kwenye hilo hatukusanyi ushauri, huo ndiyo msimamo wa Serikali hakuna ushoga hakuna mimba kwa wanafunzi.

“Hakuna likizo ya uzazi kwa wanafunzi na wanaosema haki kwa kila mtoto ndiyo maana Serikali imetoa haki kwa kila mtoto Rais Magufuli anasomesha bure ili kila mtoto apate haki hiyo.

“Hakuna kisingizo cha ada wala cha aina yoyote ni bure hakuna ‘Tuition Fee’ ni bure, Serikali imetoa haki kwa watoto atakayeamua kuiacha haki hiyo asipeleke lawama kwa Serikali,” alisema Mwigulu.

Wiki iliyopita Rais Dk. John Magufuli alitoa msimamo wake kuhusu katazo la watakaopata mimba katika utawala wake kutopata haki ya kurudi shuleni jambo ambalo liliibua mjadala mpana mitandaoni.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo mjini Bagamoyo wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Pwani ambako alizindua viwanda saba na barabara ya Bagamoyo-Msata ya kilometa 64 iliyogharimu Sh bilioni 183.

“Serikali inatoa mabilioni ya hela kwa ajili ya elimu bure, halafu zinakuja NGOs zinasema eti anayepata mimba akishazaa aruhusiwe kurudi shuleni… hizi NGOs zikafungue shule za wazazi siyo zilazimishe serikali kusomesha wazazi. Mwisho utakuta darasa la kwanza wote wanawahi kwenda kunyonyesha,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles