25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Chadema, ACT jino kwa jino

mtanzaniadaily 21 april .inddBAKARI KIMWANGA NA SHOMARI BINDA, MUSOMA

NI dhahiri sasa vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vimeanza kuumana jino kwa jino kutokana na kupishana kwenye mikutano ya kisiasa inayoendelea mikoani.
Wakati vyama hivyo vikiendelea kuchuana na kujaza mamia ya wananchi kwenye mikutano yao, viongozi wake wamekuwa wakituhumiana kwa mambo mbalimbali.
Vyama hivyo vimekuwa vikipishana katika kanda tangu vilipoanza ziara za mikoani hivi karibuni. Wakati Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika akiwa mkoani Mtwara, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alikuwa mkoani Ruvuma na timu yake.
Baada ya Mnyika kumalizia ziara hiyo, alirejea Dar es Salaam kabla ya kuanza mikutano yake Kanda ya Ziwa, ambako ACT nao walikwenda.
Akiwa mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki, Mnyika akihutubia mamia ya wananchi kwenye viwanja vya Furahisha, alisema Chadema haiko tayari kuwakaribisha ACT-Wazalendo kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Lakini siku moja baada ya Mnyika kuondoka Mwanza, Zitto na msafara wake nao waliwasili mkoani humo.
Baada ya kuwasili, Zitto alifanya mkutano wa hadhara kwenye viwanja hivyo hivyo na kusema ACT-Wazalendo wamejipanga kurudisha uzalendo.
Baada ya mkutano huo, jana Zitto aliwasili mkoani Mara ambako alifanya mkutano mkubwa wa hadhara.
Alisema kamwe hatorudi nyuma kwa maneno ya watu, kwani safari ya mapambano imeanza.
Zitto alisema hivi sasa kuna kundi la watu waliojivika upinzani dhidi ya ACT-Wazalendo, ambao wamekuwa wakikesha ili waone chama hicho kinapotea katika siasa za nchi hii.
Akizungumza katika mkutano huo kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo mjini Musoma, Zitto alisema ameamua kuingia kwenye jahazi la ACT, huku akitambua namna ambavyo anapigwa kila aina ya mishale na watu wasiomtakia mema kwenye siasa.
Alisema anashangazwa na madai ya watu hao kueneza kila aina ya propaganda zenye lengo la kukiua chama cha ACT-Wazalendo, ikiwamo kukihusisha na mipango ya kuwaandalia nafasi baadhi ya makada kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili wagombee urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, baada ya kutemwa.
“Mimi ndugu yenu nimepigwa mishale mingi kweli ndani na nje – huko nilikotoka, ikafika mahali unajitahidi kueleza kile unachojua, wenzako hawakutaki, mngekuwa ninyi mngefanyaje?
“Tumeanza ziara hii baada ya kuona moto wa ACT-Wazalendo umekuwa mkali na hauwezi kuzimika, wamegeuka na kuanza kusema eti tunawaandalia akina Edward Lowassa kuja kugombea urais… jamani hilo halipo.
“Hao ambao wamekuwa wakipita kila kona kueneza propaganda za kipuuzi wajue sasa safari imeanza ya kujenga demokrasia imara na yenye matumaini mapya kwa upinzani, ACT tunahitaji kujenga taifa imara ambalo lina misingi ya maadili kwa viongozi wake,” alisema Zitto.
Akizungumzia ni wapi chama hicho kinapata fedha za kuendesha shughuli zake, Zitto alisema wanaotakiwa kujibu swali hilo ni wale wanaoeneza propaganda chafu dhidi yake.
“Waulizwe akina Ediwn Mtei (mwasisi wa Chadema) na Freeman Mbowe (mwenyekiti) walitoa wapi fedha za kujenga Chadema kabla ya sisi kuingia na kukijenga hadi kupata ruzuku. Huko walikopata wao ndio njia hizo hizo napita kuijenga ACT.
“Nimekuwa mbunge miaka 10, nimejenga watu wanaoamini siasa zangu ndani na nje ya nchi. Sisi ziara yetu mkoa mmoja ni shilingi milioni 3.6 tu. Je, Zitto anakosa watu 11 wa kila mtu kuchangia mkoa mmoja?” alihoji huku akishangiliwa.
Zitto alitumia mkutano huo kueleza namna ACT-Wazalendo ilivyojipanga kuhakikisha inaweka misingi ya nchi na si kuzungumzia siasa zilizopita.
Akizungumzia idadi ya wanachama waliojiunga na chama hicho hadi sasa, Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa, alisema hadi sasa wamefanikiwa kuvuna wanachama wapya 4,610.
“Jana (juzi) tukiwa Mwanza tumefanikiwa kupata wanachama wapya 742, ingawa mpaka sasa Mkoa wa Tabora unaongoza kwa kuwa na wanachama 815.
“Dodoma 649, Shinyanga 1,104, Singida 594, Ruvuma 528, Njombe 26, Mambako 228, Iringa 471 na Morogoro 1,401,” alisema Mtemelwa.
MNYIKA
Naye Mnyika akihutubia wakazi wa mji wa Musoma kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo juzi, aliwataka wapenda mabadiliko kumpuuza Zitto kwa kile alichokidai kuwa ni msaliti na hana uzalendo.
Mnyika alisema Zitto ndiye aliyekuwa akiratibu majimbo ambayo CCM ilipita bila ya kupingwa kwa kula njama za kuwaondoa wagombea mwaka 2010.
Alisema miongoni mwa majimbo hayo ni pamoja na Mlale linaloongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Bumbuli linaloongozwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Musoma Vijijini linaloongozwa na Nimrod Mkono.
Mnyika alisema Zitto alifanya usaliti wa kuwaondoa wagombea ili wagombea wa CCM wapiti bila kupingwa.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania waendelee kuiamini Chadema na Ukawa ili kupata mabadiliko ya kweli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles