Na MWANDISHI WETU
MWANAMUZIKI wa Nigeria, David Adeleke ‘Davido’ ameteka akili za mashabiki wa soka duniani baada ya kumtaja mchezaji wa timu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano Ronaldo, kwenye wimbo wake mpya wa ‘Fall’.
Tangu video ya wimbo huo ulipowekwa kwenye mitandao ya kijamii imepakuliwa mara nyingi, huku wengi wakitaka kusikia alipotajwa na namna alivyotajwa mcheza soka Cristiano Ronaldo, ambaye hivi karibuni ameshinda ubingwa wa Ulaya akiwa na timu ya Real Madrid.
Wimbo huo umejizolea idadi kubwa ya watu, huku ukionyesha kutazamwa na kupakuliwa na zaidi ya watu milioni moja. Wimbo huo ni baada ya wimbo wake uliotangulia wa ‘If’ ambao nao ulijizolea mashabiki wengi ndani na nje ya Nigeria.
Katika kipande alichomtaja Cristiano Ronaldo, Davido ameimba kwamba hataki tena kuigiza kwa sababu mpenzi wake anamuita Cristiano, Mr Ronaldo, huku kiitikio cha wimbo huo kikimueleza Davido anavyolalamika namna ambavyo mpenzi wake anafuatiliwa na vitu vingi kwa sababu tu yeye anampenda.