32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGAI AAGIZA WABUNGE WAPIGWE

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema ( BAVICHA), Patrobas Katambi, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana (hawapo pichani) kulaani kitendo cha Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, kutolewa kwa nguvu bungeni juzi. Kulia ni Katibu Mkuu wa baraza hilo, Julius Mwita. Picha na Jumanne Juma

 

 

RAMADHAN HASSAN NA AGATHA CHARLES-DODOMA/DAR

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amewapa maelekezo askari wa Bunge wampe kipigo mbunge yeyote atakayeagiza atolewe nje ya Bunge na kukaidi, ili iwe mfano kwa wabunge wengine.

Kauli hii imekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Ndugai kuagiza askari kumtoa kwa nguvu nje ya Bunge, Mbunge wa Kibamba ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika (Chadema) kwa madai kuwa alikuwa akileta vurugu.

Akizungumza juzi usiku bungeni wakati akiahirisha kikao cha Bunge mara baada ya wabunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2017-2018, Ndugai alisema hawezi kukaa kimya kwa yale wanayofanya baadhi ya wabunge.

Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, alisema kumekuwa na wabunge ambao wamekuwa hawaheshimu kiti.

 “Huu utaratibu wa mbunge unaambiwa utoke nje halafu mnaleta kasheshe humu ndani, yaani leo ndio mwisho, ninakwambia Sergeant at Army na ninarudia wabunge wanasikia.

“Askari wangu mliopo hapa kama hamtoshi itakuja seti nyingine, mbunge atakayegoma hapa ‘Demo’ ni hapa hapa ndani, hakuna Bunge la namna hiyo duniani.

“Katika ustaarabu wa kibunge, kiti kikikutaka utoke nje, mbunge yeyote yule unachukua vitu vyako kwa amani unatoka nje, ndivyo ilivyo. Inawezekana kabisa siku hiyo hukuamka vizuri au shetani amepita, huwa inatokea hivyo. Ukiombwa upishe basi unapisha kwa amani na salama,” alisema.

Ndugai alisema kama mbunge hajaridhika na jambo lolote, upo utaratibu wa kikanuni  wa kuweza kulalamika, huku akidai hivyo ndivyo mabunge yanavyotakiwa kufanya kazi.

Wakati Ndugai akiweka msimamo huo, msingi wa Mnyika kutolewa bungeni juzi ulikuwa ni hoja zilizokuwa zikitolewa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2017-2018 na kauli ya mbunge mmoja ambaye hajafahamika aliyemwita mwizi.

Lusinde alikuwa akihoji hotuba ya Mnyika na hasa mahali palipoandikwa “Rais makini kabla ya kufikiria makinikia angefikiria madini yanayochimbwa na kuchenjuliwa kwa ukamilifu hapa nchini lakini nchi haipati mapato yanayostahili.”

Akichangia katika hilo, Lusinde alisisitiza watu ambao si makini ni wapinzani ambao wanatetea wezi na si rais.

Ni wakati huo ndio ambao Mnyika alisimama na kuomba utaratibu na kusema kuwa si kweli kuwa upinzani wanatetea wezi na kwamba kama ni wizi umekuwa ukifanyika chini ya Serikali ya CCM na kwamba hata sasa pamoja na mchanga kuzuiwa, madini ikiwamo dhahabu yanaendelea kusafirishwa.

Wakati Mnyika anaendelea, mbunge mwingine wa CCM akawasha kipaza sauti na kusema “Mnyika mwizi”.

Ni kauli hiyo pia ndiyo ambayo ilimfanya Mnyika amwombe Spika amwelekeze mbunge huyo ama athibitishe au afute kauli.

Hata hivyo, Spika alisema hajasikia na hivyo Mnyika kuendelea kulalamika wakati kiongozi huyo wa Bunge akizungumza jambo ambalo lilimkasirisha na hivyo kuamuru askari wamtoe nje. 

Ndugai alisema jamii inachofahamu mbunge ni mtu mstaarabu, hivyo akipewa  maelekezo na kiti anatakiwa ayafuate kutokana na kuaminiwa na wananchi.

“Kama maelekezo unayopewa hujaridhika nayo, taratibu wewe mwenyewe unakwenda zako ‘canteen’ kwenda kunywa chai, unaenda kumpumzika ukirudi baadae ni mtu mpya lakini hii haiwezekani.

“Jumatatu tunaendelea na shughuli ile ambayo niliwaambia Kamati ya Maadili, niwahakikishieni wale ambao wanataka kucheza na kiti hilo jambo haliwezekani… haliwezekani.

“Sipendi kabisa twende hivyo, lakini sasa nafanyaje? Nyie mkinifikisha huko sasa mimi nafanyaje? Lazima nifanane na vilevile tunavyoenda,” alisema.

KIBANDA

Akichambua kile kilichotokea bungeni juzi, Mwenyekiti wa zamani wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, alisema Spika Ndugai aliyumba, alikosa hekima.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, inayochapisha magazeti ya MTANZANIA, Rai, Dimba na Bingwa, alisema Mnyika alikuwa na haki ya kutaka aliyemwita mwizi abainike na athibitishe.

“Kwa maoni yangu kitendo cha Ndugai kufumbia macho jambo lile ambalo limeshawagharimu wabunge wa upinzani ndiyo kosa lililozaa vurugu zote,” alisema.

Kwa upande wa Mnyika, alisema naye alikosa ustahimilivu japo alikuwa na kila sababu ya kutaka jina lake lisafishwe.

Hata hivyo, alisema Mnyika alifanya kosa kujaribu kumkabili Lusinde ambaye mkakati wake siku zote ni kutafuta lugha za maudhi na kuwavuruga wapinzani.

“Gharama ya kila mara kuwapoteza wabunge wa upinzani katika vikao vya Bunge kwa hoja za majibizano yasiyo na maana kama yale ya jana ni kubwa.

 “Wapinzani wanapaswa kujua namna ya kujinasua katika mitego ya namna hii,” alisema Kibanda na kuongeza:

“Ndugai anatumia madaraka yake vibaya. Nguvu iliyotumika dhidi ya Mnyika ni ya kudhalilisha hadhi ya mbunge, si Mnyika tu bali wabunge wote na Bunge lenyewe.”

BAVICHA

Kwa upande wake, Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) limelaani kitendo cha Ndugai kuamuru askari wamtoe nje ya Bunge Mnyika.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam.

Katambi alisema Mnyika alikuwa akijiandaa kutoka kistaarabu, lakini Spika aliwaagiza askari wa Bunge kumtoa nje kwa nguvu.

“Bavicha inalaani vikali kitendo cha askari wa Bunge kumsukuma Mnyika ilihali hakukaidi amri ya Spika katika jambo hilo.

“Tunalaani kitendo cha Spika kuwaagiza askari kumtoa nje kwa nguvu Mnyika, hata pale ambapo alikuwa anajiandaa kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge kistaarabu kwa hadhi yake kama mbunge,” alisema.

Katambi alisema uamuzi wa Spika ni batili na kwamba pengine alifanya hivyo kwa mamlaka, lakini hayapaswi kutumika vibaya.

“Kumwondoa Waziri Kivuli kwa siku saba ni kumfanya asitoe maoni yake. Spika akubali alikosea, arekebishe, arejee, atafakari. Ame-abuse na kukinajisi kiti cha Spika. Uongozi wa Bunge ukutane na Kambi ya Upinzani kulimaliza. Asipofanya maamuzi upya tutakutana, tutasema,” alisema.

Katambi pia alimtaka Spika Ndugai kufuatilia Hansard za Bunge ili kusikia sauti iliyosema ‘Mnyika ni mwizi’ ambayo kiongozi huyo wa Bunge alisema hakuisikia.

“Bavicha tumesikitishwa na tabia hii ya aibu na isiyo ya kiungozi aliyoionyesha  Spika wa Bunge ya kujifanya hakusikia kauli za Lusinde (Livingstone) na ile ya mbunge wa CCM dhidi ya Mnyika.

“Tunamtaka Spika afuatilie Hansard za Bunge, asikilize kipande hicho wakati Lusinde anachangia na aujulishe umma kama kweli hakusikia au ni kuendeleza upendeleo kwa wabunge wa CCM na uonevu kwa upinzani,” alisema Katambi.

Alisema suala la madini ni la Watanzania na si la Rais Dk. John Magufuli pekee, hivyo wanapaswa kuungana kufanikisha kuondoa ukakasi katika mikataba ya madini.

Kwa mujibu wa Katambi, hata wanasheria wa Serikali wastaafu akiwamo Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), wanapaswa kuitwa kwa kuwa walikuwapo na wanafahamu kuhusu mikataba.

Pamoja na hilo, alisema Bavicha wanalaani kauli ya Lusinde kuwa ‘upinzani ni wezi’ na kudai kuwa wizi unaofanywa nchini unatokana na wanachama au viongozi wa chama tawala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles