Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru Salma Juma na wenzake wawili wanaodaiwa kukutwa na magunia ya bangi na kuamuru wasikamatwe tena na kushtakiwa katika mahakama hiyo.
Uamuzi huo ulitolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respius Mwijage kwa kuzingatia malalamiko ya washtakiwa na Jamhuri kushindwa kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu.
“Naamini mahakama iko kwa ajili ya kutenda haki, wanachofanya Jamhuri si kuendesha kesi bali kuwanyanyasa washtakiwa, kesi ya jinai si mchezo wa kuchezea, tunawezaje kupambana kupiga vita dawa za kulevya kwa kutokamilisha upelelezi kwa miaka mitatu na miezi minane.
“Nimezingatia malalamiko ya washtakiwa, maelezo ya upelelezi kwamba haujakamilika kwa siku 1,335 bila sababu za msingi, kwa nia ya kutenda haki na kwa kuepuka kukiuka taratibu za uendeshaji wa kesi mahakamani, nafuta mashtaka dhidi ya washtakiwa na mahakama inaamuru washtakiwa wote waachiwe huru.
“Naamuru washtakiwa wasikamatwe na kufunguliwa shtaka linalofanana na hili katika mahakama hii labda kwa maelekezo ya Mahakama Kuu ya Tanzania,” alisema Mwijage.
Akitoa uamuzi huo, Mwijage alisema washtakiwa walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Agosti 26 mwaka 2013, kesi yao ilipita mikononi mwa mahakimu tofauti tofauti ikiwa namba 154 ya mwaka 2013 hadi ilipofutwa na washtakiwa kukamatwa tena Juni 14 mwaka 2016 na kushtakiwa tena mbele yake.
Alisema waliposhtakiwa kwa mara ya kwanza walikuwa wakituhumiwa kuwa Agosti 14 mwaka 2013 walikutwa wakiwa na kilo 920 za bangi maeneo ya Kawe Ukwamani, Dar es Salaam, yenye thamani ya Sh milioni 138.
“Walipofunguliwa upya mashtaka, thamani na uzito wa dawa hizo vilipungua, walishtakiwa kwa kukutwa na gramu 169,500 za bangi zenye thamani ya Sh milioni 25.
“Tangu waliposomewa upya Juni 14 mwaka 2016 hadi Aprili 5, mwaka huu, upelelezi haujawahi kukamilika na washtakiwa walikosa dhamana, wako mahabusu,” alisema.