25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI IPO NJIA PANDA?

 

 

Na MWANDISHI WETU,

MARAIS wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania, katika mkutano wao wa 18 kujadili mambo mbalimbali yanayoikabili Jumuiya hiyo.

Ajenda kuu ya mkutano huo itakuwa ni kujadili ushirikiano "tata wa kibiashara" kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya (EPA), lakini pia kutathmini mchakato wa kuwapo kwa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki na kuiingiza Somalia katika Jumuiya hiyo.

Aidha, mkutano huo ulioanza jana unaendelea kujadili masuala mengine ya namna ya kufadhili shughuli za jumuiya hiyo, utengenezaji wa magari katika Jumuiya hiyo na upigaji marufuku wa nguo za mitumba zinazoingizwa ndani ya Jumuiya.

Vilevile mkutano huo umezindua mfumo mmoja wa elimu ya juu katika vyuo vikuu kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa katika vyuo vikuu na utunzaji wa alama unafanana.

Viongozi waliohudhuria mkutano huu ni pamoja na Rais John Magufuli, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Naibu Rais wa Kenya William Ruto na wawakilishi wengine kutoka Serikali ya Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Rais Museveni amekabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa Rais Magufuli.

Mkutano wa EAC ulitakiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka huu, lakini uliahirishwa mara tatu kwa sababu mbalimbali. Kwa kawaida, mikutano mikuu ya viongozi wa nchi hufanyika mara mbili kwa mwaka, ambayo ni Aprili na Novemba.

Viongozi hao wamekutana wakati huu nchi wanachama kama Burundi na Sudan Kusini zikiendelea kukabiliana na mvutano wa kisiasa na kiusalama, hivyo kusababisha wimbi la wakimbizi kufurika katika nchi jirani.

Nchini Burundi, mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa chini ya Uenyekiti wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kati ya wapinzani na serikali hayajazaaa matunda. Haifahamiki ni lini pande hizo mbili zitakuja kuafikiana juu ya mustakabali wa amani na usalama wa nchi hiyo.

Nchini Sudan Kusini ambayo ni mwanachama mpya wa EAC, vita vimetawala na maelfu wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano kati ya waasi wanaoongozwa na Makamu wa Rais Riek Mechar na wanajeshi wa serikali wanaomtii Rais Salva Kiir.

Licha ya viongozi hao mara kwa mara kuendelea kusisitiza kuwa wana dhamira ya dhati ya kutekeleza malengo ya Jumuiya kwa manufaa ya wananchi, suala la mkataba wa kibiashara kati yao na Umoja wa Ulaya limeonekana kuwagawa viongozi hawa.

Abdulkarim Atiki, mtaalamu wa masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema kuwa Jumuiya hiyo kwa sasa ipo katika njiapanda, kutokana na baadhi ya mataifa kuendelea kukumbwa na changamoto za kiusalama, kisiasa na suala tata la mkataba wa masuala ya uchumi kati yao na Umoja wa Ulaya (EPA).

“Hali nchini Burundi siyo nzuri sana, demokrasia nchini Uganda ipo mashakani, Rwanda pia hali ni vivyo hivyo kisiasa, na hili ni tatizo,” amesema Atiki.

“Mkataba wa EPA umegawa viongozi wa nchi wanachama, na wameshindwa kuitafsiri kwa manufaa ya wananchi wetu,” ameongeza.

“Bado zinahitajika jitihada zaidi, kuimarisha umoja huu na kila mmoja kuzungumza kwa sauti moja,” amesisitiza Atiki akiwa jijini Dar es Salaam.

Inasubiriwa kuona ikiwa mkataba huo utapewa ufumbuzi katika mkutano huo. Mataifa pekee  yaliyoutia saini ni Kenya na Rwanda.

Uganda ilibadilisha uamuzi wake katika dakika za lala salama, huku Tanzania ikisema mpango wake wa kuwa na nchi za viwanda huenda ukaathirika pakubwa ikiwa itaingia katika mkataba huo.

Burundi nayo ilikataa kuukubali kwa sababu za kisiasa, baada ya Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo vya kiuchumi baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania urais kwa muhula wa tatu mwaka 2015.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukishinikiza mataifa yote ya Jumuiya  kutia saini mkataba huu ili kuondoa vikwazo vya kupata soko la bidhaa zake barani Ulaya, lakini pia bidhaa zake zipate soko la watu milioni 150 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mataifa mengi ya EAC hayana bidhaa nyingi za kusafirisha barani Ulaya, ukiondoa Kenya ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisafirisha maua katika soko la Ulaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles