27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KIGEZO MUHIMU UNAPOTAFUTA MWENZI WA MAISHA

 

 

Na Christian Bwaya,

HIVI majuzi nilisikia mjadala mkali kuhusu usiri kwa wanandoa. Usiri uliojadiliwa ni kile kitendo cha mwanandoa kuficha ukweli wa mambo, kutoa habari zisizokamilika au hata kumnyima mwenzi wake taarifa za msingi ambazo angestahili kuzifahamu. Mume/mke anapoficha tarakimu halisi za kipato au matumizi yake, anapopanga na kutekeleza mipango bila kumshirikisha mwenzake maana yake anakuwa msiri.

Katika mjadala huo, zilikuwapo pande mbili zilizopingana kimtazamo. Upande wa kwanza uliamini kuwa uwazi na ukweli kwa mambo yote ndio sifa muhimu wanayoihitaji watu wawili walioamua kuaminiana na kupendana. Unapompenda mtu lazima uwe na ujasiri wa kumwambia siri zako. Kukosa ujasiri wa kushirikishana mambo ya msingi kunazorotesha uhusiano.

Upande unaounga mkono usiri ulisimamia kwenye hatari ya kuwa wazi kwa mtu asiyetabirika kesho anaweza kufanya nini. Kutokuaminika kwa baadhi ya watu kunafanya iwe muhimu kuchukua tahadhari kwa kuficha baadhi ya mambo. Ulitolewa mfano wa Samson, mtu mwenye nguvu tunayesoma habari zake kwenye biblia. Samson alifanya kosa la kutoboa siri ya nguvu zake kwa mke wake. Matokeo yake kitendo hicho cha kilichofanywa katika mazingira ya kimapenzi na kuaminiana, kilimgharimu Samson.

Mpaka mjadala huu unafikia tamati, washiriki hawakuwa wamekubaliana kwa hakika kipi cha kufanya. Hata hivyo, lengo hasa la mjadala huo halikuwa kumpata mshindi bali kubadilishana uzoefu. Nilitafakari suala hili kwa muda mrefu baada ya mjadala kumalizika. Nilijaribu kuzielewa hoja za pande hizo mbili. Nikajifunza mambo mawili makubwa.

Kwanza, kila ndoa ina uzoefu wake. Tunatofautiana. Kinachowezekana kwa watu fulani, si lazima kiwezekane kwa wengine. Kwa mfano, wapo wanandoa wasioaminiana. Kila mmoja anakuwa na wasiwasi na mwenzake hata kama hilo halizungumzwi wazi. Ili kukabiliana na wasiwasi huo, lazima kuchukua tahadhari za msingi katika jitihada za kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza.

Hatuwezi kupuuza ukweli kuwa wapo wanandoa walaghai wanaoweza ‘kujiibia’ kwa kufanya udanganyifu. Hata katika mazingira ambayo nia ya mmoja wapo ni njema, unaweza kuwapo wasiwasi wa namna ukweli huo utakavyotumika. Katika mukhtadha huu, usiri unakuwa sehemu ya suluhisho.

Somo la pili si kwa wanandoa wenyewe bali watu wanaojiandaa kuingia kwenye ndoa. Nilijifunza kuwa iko haja kubwa ya vijana wanaojiandaa kuingia kwenye ndoa kutafakari kwa kina vigezo wanavyovitumia kutafuta mwenzi wa maisha. Katika kutafakari vigezo hivyo, ni lazima kuelewa kuwa ndoa ni muunganiko wa watu wawili walioamua kuaminiana kwa dhati.

Msingi mkubwa wa ndoa ni watu wawili kuwa kitu kimoja. Ndoa ni kushirikiana mambo yanayowahusu kwa uwazi bila wasiwasi wa kuhujumiwa. Furaha na utoshelevu wa ndoa unategemea kwa kiasi kikubwa namna gani watu wawili wanavyoweza kushirikiana mambo yao bila hofu ya kutokueleweka, kuhukumiwa wala kuachwa. Hiyo ndiyo tofauti kubwa ya ndoa na urafiki mwingine wowote. Mtu aliyeoa maana yake anaishi na mtu anayemwamini kuliko watu wengine wote. Mke wa mtu huyu ndiye anayejua mambo yake ya ndani zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Kwa uelewa huo, kijana –wa kiume au wa kike –anayetafuta mwenzi wa ndoa lazima awe na vigezo vinavyomwongoza kuungana na mtu mwingine kwa karibu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. Kigezo kikubwa ni kuhakikisha kuwa anapata mtu anayeweza kumfanya ajisikie huru kumwambia vyote bila wasiwasi wa kutokueleweka.

Itaendelea…

Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles