WASHINGTON, MAREKANI
RAIS wa Marekani, Donald Trump anatarajiwa kutimiza siku 100 tangu alipoapishwa Januari 20, mwaka huu kuliongoza Taifa hilo kubwa duniani kiuchumi na kijeshi. Trump alitimiza siku 100 za kuliongoza Taifa hilo Aprili 29, mwaka huu yaani jana.
Katika siku yake ya 100 madarakani, Rais Donald Trump alitarajiwa kuzungumzia masuala ya biashara katika moja ya majimbo yaliyochangia ushindi wake usiotarajiwa, ambapo alisaini amri ya rais kutathmini upya mikataba ya biashara ya Taifa hilo.
Ni moja ya amri mbili ambazo rais huyo alizitia saini akiwa kwenye Kiwanda cha Koleo katika kaunti ya Cumberland jimboni Pennsylvania. Hilo ni jimbo lililosukuma mbele ushindi wake wa kushangaza.
Wiki iliyopita ilishuhudia mhemuko mkubwa katika Ikulu ya White House wakati Trump na timu yake wakijaribu kuorodhesha mafanikio na kutimiza ahadi kabla ya kufika siku ya kibiashara ya 100.
Pamoja na ziara ya kiwanda cha zana cha Ames, ambacho kimekuwa kikitengeneza Koleo tangu 1774, Rais Trump alifanya mkutano aina ya ile alioifanya wakati wa kampeni kuhitimisha siku hiyo. Ni kama kurudi kwenye kanuni kwa rais ambaye katika siku za karibuni, amekuwa akitoa matamshi yanayoashiria kutoridhika na mafanikio yake mpaka sasa.
Amri nyingi zaidi za rais
Mapema wiki hii, Trump alitangaza azma yake ya kuujadili upya mkataba wa biashara huria wa mataifa ya Amerika Kaskazini (NAFTA). Alisema pia angeanza kujadili upya makubaliano ya biashara huria na Korea Kusini ambayo kwake Marekani ina nakisi kubwa ya kibiashara.
“Hakuna siku inayopita bila rais kuzungumzia suala la biashara," alisema Waziri wa biashara, Wilbur Ross juzi akiwa Ilkulu.
Amri za rais zilizosainiwa jana zitakuwa za 31 na 32 tangu alipoingia madarakani, idadi ambayo ndiyo kubwa zaidi kuwahi kusainiwa na rais katika siku 100 za kwanza madarakani tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia.
Ni hali tofauti kabisa na matamshi ya Trump aliyoyatoa wakati wa kampeni, alipomkosoa mtangulizi wake kwa kutumia njia hiyo, ambayo ina faida ya kutohitaji idhini ya Bunge.
Amri muhimu zaidi kati ya mbili itaipa Wizara ya Biashara na mwakilishi wa biashara wa Marekani siku 180 kubaini ukiukaji na matumizi mabaya chini ya mikataba ya biashara ya Taifa hilo na kupendekeza hatua za kuchukuliwa. Waziri Ross alisema Shirika la Biashara duniani (WTO) lina ukiritimba mwingi na limepitwa na wakati na linahitaji kufanyiwa mageuzi.
Waziri huyo wa biashara alipuuza uwezekano wa Marekani kujiondoa kwenye shirika hilo la usuluhishi wa sheria za biashara duniani lenye makao yake mjini Geneva nchini Uswisi, lakini hakuondoa uwezekano huo.
"Kama ilivyo kwa shirika lolote la kimatifa, huwa kuna uwezekano wa kufanya marekebisho," alisema.
Aumizwa kichwa na China
Utawala wa Trump unahoji kuwa ushindani usio wa haki na China na washirika wengine wa kibiashara umefuta mamilioni ya ajira za viwandani nchini Marekani. Ross alisema kutoridhishwa na sera ya kibiasahra ndiyo moja ya sababu wapigakura walimgeukia Trump katika uchaguzi.
"Wamechoka kuona ajira zao zinahamia nje ya nchi. Wamechoshwa na baadhi ya matendo yanayoharibu. Hivyo, kimsingi Taifa lilisema katika uchaguzi uliopita: Ni wakati wa kurekebisha mambo. Na rais alisikia ujumbe huo,” alisema Ross.
Trump ambaye aliahidi kuishughulikia China na washirika wengine wa kibiashara, ametangaza hatua kadhaa nyingine katika wiki za karibuni.
Ameiagiza wizara ya biashara kuchunguza sababu za nakisi kubwa katika bidhaa za kibiashara za Marekani iliyofikia Dola bilioni 734 kwa mwaka uliopita, Dola bilioni 347 zikiwa katika biashara na China pekee.
Utawala huo pia unaanza kuziwekea ushuru bidhaa za mbao laini kutoka Canada na unachunguza iwapo bidhaa za nje za chuma na aluminium zinasababisha kitisho kwa usalama wa Taifa.
Robert Lighthizer, Wakili wa Biashara ambaye Trump amemteua kuwa mwakilishi wake wa biashara, ameukosoa uamuzi wa mwaka 2001 wa kuiruhusu China kujiunga na Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Malalamiko dhidi ya WTO
Serikali ya Trump ilichukulia kwa kutojua kwamba China ilikuwa ‘mfano tu wa nje wa Canada’, Wakili Lighthiner aliwahi kuthibitisha na kwamba ingejifunza kuishi ndani ya sheria za WTO na kufungua soko lake kwa bidhaa za Marekani; badala yake China imedhibiti ushindani wa nje, kuchezea thamani ya sarafu yake na kuwapatia ruzuku wafanyabiashara wake wa nje.
Ross alisema kuwa WTO imejielekeza zaidi kuhusu kudhibiti ushuru wa desturi ya kodi kwenye bidhaa za nje na halifanyi vya kutosha kukabiliana na vikwazo visivyo vya kidesturi vya biashara au kuzuia ukiukaji wa haki za umiliki.
Trump anashinikiza kuwepo na uhuru wa makubaliano ya kibiashara ya kutendeana, ambamo Marekani inaweza kupandisha au kushusha ushuru kwa bidhaa za Taifa kulingana na namna nchi hiyo inavyoitendea Marekani.