28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MGOGORO CUF UTAFUTIWE UFUMBUZI WA KUDUMU HARAKA

MOSHI ambao umefukuta kwa muda mrefu ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF), sasa unakaribia kutoa moto, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa amani ya Taifa letu.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, CUF imekuwa  katikati ya mgogoro mkubwa wa kiuongozi, msingi wake ukiwa ni uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kuirudia nafasi yake ya uenyekiti aliyotangaza kuiacha wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Tukio lililofanywa na watu waliotajwa kuwa ni walinzi wa upande wa Profesa Lipumba wiki iliyopita la kuvamia mkutano na kujeruhi kwa silaha wa upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ndilo limetoa taswira kwamba mgogoro ndani ya chama hicho sasa umefika hatua mbaya.

Si hilo tu, kauli ya wabunge wa CUF wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanaomuunga mkono Maalim Seif kutangaza kwenda kufanya usafi siku ya Jumapili Makao Makuu ya chama hicho Buguruni, huku upande wa Profesa Lipumba wakionekana wanachama wakifanya mazoezi,  ni ishara tosha kwamba mgogoro ndani ya chama hicho sasa unatakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka kabla ya maafa zaidi kutokea.

Ukweli  ni kwamba, kwa muda wote tumeshuhudia Ofisi ya Msajili ikikibebesha CUF matumaini ya kutafuta haki na kurekebisha palipoharibika kwa njia ambazo tunadhani hazijafanya kazi.

Tunapotazama yanayotokea leo hii ndani ya CUF, tunadhani ni matokeo ya mizengwe ya muda mrefu ya kisiasa inayofanywa na vyama vinavyopambana kushika dola.

Historia si tu ya CUF, bali vyama vikubwa vya upinzani kufanyiwa mizengwe ipo wazi kila inapotokea kuonekana kuteteresha maslahi ya wapinzani wake.

Tangu miaka ya 1990, wakati wa kushamiri vuguvugu la kuanzishwa vyama vingi vya siasa, upo ushuhuda mwingi na malalamiko mengi kutoka kwa vyama vya upinzani kufanyiwa hujuma.

Hujuma zimetajwa hata katika chaguzi kuanzia katika zoezi la uandikishaji hadi kupiga kura.

Mwanasiasa mmoja wa Chama Cha Mapinduzi, Marehemu Asha Bakari, alipata kusema kwamba CUF kamwe haitashinda kupitia sanduku la kura, labda kwa mtutu.

Hii ni mifano michache tu kati ya malalamiko mengi ya vyama vya upinzani ambayo tunadhani bado Ofisi ya Msajili haijaweza kusimama sawasawa katika nafasi yake ili kuweza kushughulikia.

Kwa kushindwa kushughulikia vyema migogoro na malalamiko kutoka katika vyama vya upinzani, pengine kwa sababu ya upofu ama kutengeneza au uchanga wa kuhimili mitikisiko ya demokrasia, ipo siku tutajikuta tumetengeneza bomu hatari ambalo kulizuia kwake lisilipuke itakuwa ni shida.

Pengine sasa ni wakati mwafaka kwa mamlaka husika kubadili mwelekeo wa kushughulikia migogoro na malalamiko ya vyama vya upinzani ili kukwepa kuliweka Taifa katika mtego hatari wa kuingia kwenye machafuko yasiyo ya lazima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles