27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAZOEZI HUWASAIDIA WAGONJWA UTI WA MGONGO

 

Na Adrian Mgaya,

WAKONTA Kapunda ni binti aliyekuwa na ndoto nyingi katika maisha yake, lakini ndoto hizo zilikatishwa ghafla na ajali ya gari katika mahafali ya kumaliza kidato cha sita. Ajali hiyo  ilimsababishia ulemavu wa kudumu.

Baada ya kupata ulemavu, Wakonta alipamba mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari vilivyosheheni historia ya maisha yake.

Historia ya Wakonta inawagusa wengi hasa alipotumia ulimi kuandika baada ya kupooza kutoka shingoni kwenda chini, jambo lililosababishwa na ajali ya kugongwa na gari aliyoipata akiwa katika mahafali yake ya kumaliza kidato cha sita Shule ya Wasichana Korogwe.

Na hii inaotoa funzo kwamba hujafa hujaumbika, mambo mengi yakiwamo yanayoshabihiana na tukio lililompata Wakonta, yanaweza kusababisha matatizo katika uti wa mgongo, lakini pia kuna mambo mengine kama kutokuwa na muda wa mazoezi, aina ya shughuli unazofanya, mitindo ya maisha tunayoishi, kusogea kwa umri pamoja na kuzaa.

Tatizo la uti wa mgongo kwa kiasi kikubwa linaweza kusababisha baadhi ya watu kupata  ulemavu.

Tafiti zinaonesha kuwa matatizo katika uti wa mgongo huweza kuathiri asilimia 40 katika moja ya hatua za waathirika.

Ugonjwa wa uti wa mgongo huweza  kumuathiri  binadamu yeyote yule endapo sehemu ya uti wa mgongo  ambayo ina kazi ya kushika mifupa yote kwa pamoja kuanzia fuvu hadi mbavu na mifupa ya chini kama itaathiriwa na maradhi au ajali.

Ni ukweli usiopingika kuwa matatizo ya uti wa mgongo yanakua kwa kasi kutokana na kadhia mbalimbali zinazotokea katika maisha ya watu ikiwamo ajali, huku baadhi ya watu wakibaki na fumbo juu ya uti wa mgongo.

Daktari Haleluya Moshi ni mtaalamu kutoka Hospitali ya Rufaa KCMC (Physiotherapist) anayeshughulikia matatizo ya uti wa mgongo, anasema;

“tatizo la uti wa mgongo linajitokeza pale ambapo mishipa ya fahamu iliyopo katika pingili za mifupa ya mgongo inapokatika.”

Anaongeza; “tatizo hili huanzia sehemu ambayo mishipa hiyo ya fahamu inayopeleka taarifa katika ubongo ilipokatika kushuka sehemu ya mwili wa binadamu, hivyo kusababisha mgonjwa kutohisi mguso katika maeneo yaliyoathirika.”

Dk. Moshi anasema endapo tatizo kwa mgonjwa litaanzia sehemu ya shingo basi hata mikono itashindwa kufanya kazi.

Inawezekana umekutana na watu wenye viungo vyote vya mwili lakini wapo katika viti vyenye magurudumu?  Si watu wote waliopo katika viti vyenye magurudumu wamezaliwa na ulemavu, wengine hawakuzaliwa na ulemavu wowote lakini wakajikuta wapo hivyo, na wanawakilisha maelfu ya Watanzania wenye ulemavu.

Kila mmoja akidai kuwa ilitokea ghafla na maisha yakabadilika, wengine ni kutokana na ajali za barabarani zilizowajeruhi uti wa mgongo na matokeo yake  ni ulemavu.

Mohamed Tega ni miongoni mwa waathirika wa matatizo ya ugonjwa wa uti wa mgongo anasema chanzo cha yeye kuwa miongoni mwa watu wanaotegemea viti vya magurudumu ni ajali ya gari.

“Ilitokea tu, nilipata ajali, nikanusurika lakini nikajikuta katika hali hii. Madaktari wameniambia kwa kuwa nina shinikizo la damu, sitakiwi kula nyama na chumvi ili kupunguza ukubwa wa tatizo.

 “Huwa tunafanyishwa mazoezi katika hospitali ya mifupa (MOI), kule kuna wataalamu wanaotusaidia kutufanyisha mazoezi ili kuepuka matatizo yanayoweza kusababishwa na mwili kukaa sehemu moja tu,” anasema Tega.

Wataalamu wa masuala ya afya huona mazoezi kama muarobaini kwa watu  waliopata  matatizo kwenye  uti wa mgongo, huku wakizidi kutoa elimu kwa wagonjwa kufanya mazoezi kama anavyoeleza  Dk. Moshi.

“Mazoezi yanasaidia maungio ya mwili kuweza kujikunja pamoja na kujinyoosha hasa kwa wale walioumia kwa kiwango kidogo, huweza kuwasaidia kurejesha nguvu zao taratibu, na kwa walioumia shingo hushindwa kupumua vizuri, hivyo mazoezi ya kupumua huwasaidia,” anasema Dk. Moshi.

Anafafanua kuwa wanawafundisha wagonjwa kuweza kuhama kutoka katika kiti mwendo kwenda katika vitanda vyao hatimaye kuweza kuishi vizuri katika maisha ya kawaida.

Matatizo ya uti wa mgongo kwa namna moja  ama nyingine yameharibu ndoto za watu wengi na wengine kupoteza maisha kwa haraka kutokana kukata tamaa na kutojikubali.

Lakini wapo waliojikubali na wengine kuweza kutimiza ndoto zao ilhali wamepata ulemavu japokuwa hawakuzaliwa nao, hivi ni nani leo hii  asiyelijua jina la Wakonta aliyeandikwa mno na vyombo vya habari  kwa kadhia ya ajali  iliyomkuta  na kumsababishia ulemavu?

Inawezekana ingekua kwa mwingine  isingekuwa rahisi kujikubali na kuruhusu maisha yaendelee, lakini kwa Wakonta imewezakana na tunaweza kusema ni mfano wa kuigwa kwani katika maisha hakuna aijuaye kesho.

Mara kadhaa tunaona  kuwa watu waliopatwa na matatizo ya uti wa mgongo hususan kwa walemavu wengi wao huvimba miguu.

Hili linawezekana likawa fumbo kwa watu wengi na kutaka kufahamu kuna siri gani kwa wale walemavu wanaoshindwa kutembea na kuvimba miguu. 

Dk. Fanuel Bellet ni mtaalamu wa matatizo ya uti wa mgongo kutoka KCMC anasema watu ambao hawawezi kutembea, misuli yao hukosa uwezo wa kusukuma maji kutoka kwenye miguu na kwenda sehemu nyingine ya mwili, jambo linalofanya maji kubaki kwenye miguu na hivyo kusababisha miguu kuvimba.

Anasema tatizo hili si kwa wagonjwa wa uti wa mgongo pekee bali pia huwapata wale wenye saratani.

Anasema ili kuepuka tatizo hili mgonjwa anapaswa kutumia mashine ambayo hushtua misuli kidogo ili kuwa mikakamavu, lakini pia mazoezi hufanya misuli kuisaidia mishipa ya maji kufanya kazi.

Ukifuatilia historia za watu wengi wenye ulemavu walikuwa wazima, mabadiliko yote hutokea kutokana na aina ya maisha watu wanayopitia  ikiwamo ajali, vipigo na kuumizwa katika matukio tofauti ambayo mengine yanaweza kuepukika.

Uelewa wa watu

Teddy Gumbo, mkazi wa Chang’ombe jijini Dar es Salaam anasema hafahamu matatizo katika uti wa mgongo yanasababishwa na nini lakini ameshuhudia watu wengi wakilalamika juu ya maumivu ya mgongo.

Naye Ramadhani Masudi anasema; “nafahamu kuwa ni athari fulani zinazotokana na matatizo katika maungio ya mgongo na athari hizi zinaweza kusababishwa kutokana na mazingira yanayomzunguka mtu.”

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (B. A in Journalism).

0656110670 au barua pepe [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles