Na Fredy Azzah, Tabora
WIZARA ya Maji na Umwagiliaji imesaini mkataba na wakandarasi watatu kutandaza bomba la maji kutoka Shinyanga hadi Tabora utakaogharimu Dola milioni 268.35 za Marekani (zaidi ya Sh bilioni 600).
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo iliyofanyikia Tabora Mjini jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo, alisema mradi huo wa kusafirisha maji ya Ziwa Victoria, unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ya nchi hiyo.
Kitila alisema mradi huo utaotarajiwa kuanza Mei, mwaka huu na kukamilika ndani ya miezi 30, utafanywa na wakandarasi watatu tofauti na alimtaja wa kwanza kuwa ni Megha Engineering Infrastructures wa India na ataanzia katika Kijiji cha Solwa kilichopo Shinyanga Vijijini hadi Nzega Mjini.
Alimtaja mkandarasi wa pili kuwa ni Kampuni ya L & T ikishirikiana na Kampuni ya Shriram zote za India ambazo zitasambaza mtandao wa bomba kutoka Nzega Mjini hadi Manispaa ya Tabora kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.
Alisema ujenzi wa bomba hilo kutoka Nzega Mjini hadi Igunga utafanywa na Kampuni ya Afcons ikishirikiana na SMC ambazo zote za India.
Kitila alisema kukamilika kwa mradi huo ndani ya miaka miwili na nusu, utafanya zaidi ya wakazi milioni 1.1 wa miji ya Tabora, Igunga, Uyui, Nzega na baadhi ya maeneo ya Shinyanga Vijijini kupata maji safi kwa asilimia 100.
Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, aliwaagiza wakandarasi hao kumaliza kumaliza kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa na kwamba hatowaongezea hata siku moja.
Aliwataka pia wananchi kuwapa ushirikiano wakandarasi hao na kutohujumu kwa namna yoyote ile mradi huo ili ukamilike kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alisema mradi huo ukishafika katika Mji wa Nzega, halmashauri itatumia mapato yake ya ndani kusambaza maji kwenye vitongoji.
Pia aliitaka wizara kuanzisha Mamlaka ya Maji Vijijini ili kurahisisha usambazaji wa bidhaa hiyo aliyosema ndiyo kila kitu ndani ya maisha ya mwanadamu.
Alitaka wakandarasi wasaidizi wapewe wazawa wa maeneo husika ili kukuza uchumi wao pamoja na maeneo yao.