27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAUAJI YA POLISI 8 SI UJAMBAZI WA KAWAIDA

Na WAANDISHI WETU

-KIBITI, DAR ES SALAAM

TUKIO la kuuawa kwa askari wanane waliokuwa wakitoka doria katika Kijiji cha Jaribu wilayani Kibiti, lina kila dalili kutekelezwa na watu wenye ujuzi na malengo mapana.

Tukio la sasa ambalo limechukua uhai wa Inspekta Peter Kigugu, F.3451 Koplo Francis, F.6990 PC Haruna, G.3247 PC Jackson, H.5503 PC Siwale, H.1872 PC Zacharia, H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub, ni mwendelezo wa matukio mengine saba ya aina hiyo yaliyotokea  katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja Mkoa wa Pwani.

Ingawa hadi sasa si Jeshi la Polisi wala mamlaka nyingine ambazo zimekwishaeleza kwa uwazi kiini cha kuwako kwa mfululizo wa matukio ya aina hiyo katika maeneo yale yale, lakini utekelezaji wake na aina ya watu wanaotekeleza unaelezwa kuwa na mwelekeo wa kigaidi.

Timu ya MTANZANIA Jumamosi ilifika katika eneo la tukio na baadaye Kituo cha Polisi Bungu iliposhuhudia gari aina ya Toyota Land cruiser lenye namba za usajili PT 3713, lililoshambuliwa na wahalifu likiwa lina jumla ya matundu 22 ya risasi.

Upande wa kioo cha mbele cha gari hilo lilikuwa na matundu tisa, wakati ubavu wa kushoto ukiwa na matundu mawili na upande wa kulia juu kulikuwa na tundu kubwa moja na upande wa nyuma kukiwa na matundu sita.

Mmoja wa askari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, alisema wauaji hao walikuwa wamejificha kwenye magema yaliyopo pembezoni mwa barabara ya Kilwa.

“Ilikuwa ni vigumu kubaini sehemu ile kama kuna watu wanatuchora ndio maana ukiona hata haya matundu ya risasi yanaonyesha yalipigwa kutoka juu.

“Inatia hasira sana jinsi wenzetu walivyouawa, yule kiongozi wa patroo alikuwa kavaa kofia ngumu, tulikuta kapigwa risasi nane kichwani yaani tulivyomvua tu kofia ubongo wote ukamwagika,” alisema.

Aliongeza kwamba, wahalifu hao wanaonekana kujipanga siku nyingi kutekeleza mauaji hayo.

“Tulipokagua eneo walipotekeleza shambulio hilo nyuma ya gema kwa upande wa kulia kama unatoka Dar es Salaam tumekuta mazingira yanayoonyesha walikuwapo eneo hilo kwa siku zaidi ya tatu, kwenye ile mikorosho kulionekana kuwapo kambi na kunaonesha walikuwa wanapika pale pale,” alisema.

Askari mwingine ambaye naye hakutaja jina lake, alisema tatizo kubwa lipo katika jamii ambapo wananchi hawatoi ushirikiano wa kufichua mtandao wa wahalifu.

“Tumekuwa na operesheni ya muda mrefu ya kuwasaka wahalifu wanaotekeleza mashambulizi haya, kwa wale tunaowakamata kwa kuwahoji hata ukiwashurutisha vipi watakwambia neno moja astakafirulah!

“Wengine tukiwabana sana wanasema hawako tayari kusema chochote bora wauawe. Nakumbuka kuna wachache tu wametuambia kuwa wamepata mafunzo ya kufanya aina hiyo ya uhalifu katika mataifa 11 ya Afrika Kaskazini na Arabuni,” alisema askari huyo.

Askari mwingine alisema hajalala kwa siku ya nne jana kwa sababu alikuwa kwenye doria porini.

“Nilikuwa kwenye doria ..hawa wahalifu wanajificha sana huko porini wanajifanya wanachoma mkaa, tulikuwa tunabomoa nyumba kule, unakutana na mtoto wa miaka mitano jeuri kweli na ukimuuliza wazazi wake wako wapi anakujibu wamekufa kumbe wamejificha.

“Hivi juzi tulifikia nyumba moja huko kijijini kabla ya kuvamia kuwakamata tukasikia mzee anatoa maelekezo kwa mwanawe kwamba hao mapolisi ni makafiri tu ukikutana nao waue, uanze na wao kisha uhamie kwa walimu,” alisema askari huyo.

Timu ya MTANZANIA Jumamosi ilikutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba katika eneo la tukio ambaye ameelezea shambulio hilo kuwa ni la kuvizia na lilipangwa.

Mwigulu alitoa kauli hiyo jana baada ya kutembelea eneo ambalo shambulio hilo lilifanyika, akisema tukio hilo linachukiza hivyo Serikali haitashindwa vita hiyo.

Aliongeza kwamba tukio hilo limechochea zaidi nguvu ya kupambana na uhalifu wa aina yoyote hapa nchini.

“Nimekuja kuwapa pole askari wetu, tukio hili linaonekana lilipangwa na si bahati mbaya. Nawaomba Watanzania watulie sisi tumejipanga vizuri kupambana na uhalifu wa aina hii na tutazirudisha silaha zote ambazo wameziiba,” alisema Mwigulu.

Alisema kutokana na hatari ya eneo husika, ameagiza kuongezwa kwa askari pamoja na vifaa vya kutosha hususani magari makubwa.

“Sikutegemea kuona eneo lenye hatari kama hili kuwa na askari wachache pamoja na vifaa vichache,” alisema Mwigulu.

Wakati Mwigulu akisema hayo, kwa upande wake Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam jana, alisema alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuungana kupambana na majambazi walioua askari hao.

 

Akielezea tukio hilo, Mssanzya alisema lilitokea katika Kijiji cha Jaribu Mpakani kilichopo Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani, ambapo askari tisa walikuwa wanatoka lindo na kurudi kambini.

Alisema askari hao wakiwa kwenye gari la wazi walivamiwa na majambazi ambao walimrushia risasi dereva hali iliyosababisha gari hilo kuyumba na kuanguka.

“Mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, majambazi hao walivamia gari hilo na kuanza kuwapiga risasi askari waliokuwa ndani ya gari na askari wanane walifariki na mmoja alijeruhiwa mkononi,” alisema Mssanzya.

Aliongeza kuwa mara baada ya kuua polisi hao majambazi hao waliiba silaha saba, nne zikiwa SMG na tatu ni Long range ambazo zilikuwa zinatumiwa na polisi hao wakati walipokuwa lindo.

Alisema wakati majambazi hao wanakimbia, kulikuwa na askari wengine waliokuwa kwenye maeneo hayo ambao walianza mashambulizi na kufanikisha kuua majambazi wanne kati ya wale waliofanya tukio hilo na kuokoa silaha nne, mbili zikiwa za polisi waliouawa na mbili zinatumiwa na wao kwenye matukio mbalimbali.

Alisema matukio ya mauaji katika maeneo hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara jambo linaloonyesha wazi kuna vikundi vya majambazi vimejificha kwenye misitu iliyopo eneo hilo na hivyo kuhitaji nguvu ya ziada ili kuhakikisha wanavisambaratisha.

 “Hatuwezi kuvumilia kuendelea kwa vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara katika maeneo hayo, sasa inatosha, dawa ya moto ni moto,” alisema Mssanzya.

Alisema hadi sasa zaidi ya polisi 10 wameuawa kwa vipindi tofauti katika maeneo hayo, mbali na baadhi ya watendaji wa Serikali ya kijiji.

“Imefika wakati sasa wa kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.”

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kipindi hiki cha msako wa watu hao ili wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.

Tukio hilo limemsikitisha na kumshtua Rais Dk. John Magufuli ambaye  amesema analaani matukio yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali zao.

Rais Magufuli ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo.

 “Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu wanane ambao  wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.

“Namwomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu,” alisema Rais Dk. Magufuli kupitia taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Kumekuwapo na mlolongo wa matukio ya mauaji katika wilaya ya Kibiti na Mkuranga na kinachozua maswali ni kitendo cha wauaji kutochukua mali yoyote.

Tukio la sasa la kuuawa kwa askari wanane limetokea ikiwa ni siku chache baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliokuwa wamevalia buibui za kike.

Wanaume hao ambao walikuwa na pikipiki mbili, walikuwa wakijaribu kukwepa vihunzi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika Daraja la Mkapa.

 

Februari mwaka huu, watu watatu akiwemo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.

Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi/mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.

Mei, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa kwa risasi.

Oktoba, 2016 Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho hicho, Aly Milandu, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanne.

Novemba, 2016 wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho, waliuawa kwa kupigwa risasi.

Januari, 2017 watu ambao Jeshi la Polisi hadi sasa halijawafahamu walimuua mfanyabiashara, Oswald Mrope kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake.

Februari 3, 2017 watu wasiojulikana walivamia nyumba ya mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles