27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Bomani ajitosa suluhu ya CCM, Ukawa

Jaji Mstaafu, Mark Bomani
Jaji Mstaafu, Mark Bomani

NA ESTHER MBUSSI, DAR ES SALAAM

JAJI mstaafu, Mark Bomani, amewataka Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kurejea bungeni kujadili Rasimu ya Katiba Mpya.

Jaji Bomani pia amewashauri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuweka kando suala la idadi ya Serikali na kujadili masuala mengine yaliyomo kwenye rasimu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Jaji Bomani alisema yuko tayari kukutana na Ukawa na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) ili kujadili muafaka wa Katiba Mpya ambayo inaonekana kupoteza matumaini ya kupatikana kama ilivyopangwa.

Jaji Bomani alikiri kuwa ni moja ya Watanzania wanaoamini katika muundo wa Serikali tatu lakini hakusita kuonyesha wasiwasi wake wa kupatikana kwa muafaka au maridhiano pindi Bunge Maalumu la Katiba litakapokutana Agosti mwaka huu.

“Binafsi malumbano yaliyotokea na yanayoendelea yananihuzunisha sana, nijuavyo mimi msingi wa Katiba nzuri ni maridhiano, katiba nzuri haiwezi kupatikana kwa wingi wa kura au kwa hoja ya nguvu tu bali inatakiwa ikubalike na walio wengi (consensus).

“Zimejitokeza tofauti kubwa za kimtizamo au kiitikadi bila kusahau maslahi binafsi ambayo hayanipi matumaini, kwamba muafaka au maridhiano yatapatikana hasa juu ya suala la idadi ya Serikali, nina mashaka pia kama kuna utashi wa kutosha wa baadhi ya viongozi wa nchi,” alisema.

Alisema si sawa mchakato mzima wa Katiba kukwamishwa na suala la muundo wa Serikali wakati kuna mengi ya kujadiliwa kama Tunu za Taifa, Uwakilishi sawa wa jinsia yaani asilimia 50 kwa 50 kwenye vyombo vya uwakilishi muundo wa tume huru ya uchaguzi, mawaziri kutokuwa wabunge na suala la mgombea binafsi.

“Hayo ni baadhi tu ya masuala ambayo yangeweza kujadiliwa na kupatiwa muafaka na kuingizwa kwenye Katiba iliyopo bila ya kukwamishwa na suala la idadi ya Serikali.

“Ninachomaanisha hapa ni kwamba kama uwezekano wa kukubaliana juu ya idadi ya Serikali haupo, si sawa kuwamisha masuala mengine yote kama hilo haliwezekani kwa nini tusiliweke kiporo hadi wakati muafaka.

“Iliwachukua wenzetu Wakenya miaka 10 kukubaliana juu ya Katiba Mpya, mimi binafsi na kitaaluma ningependa sana tupate Katiba Mpya tena ni mshabiki wa Serikali tatu lakini si kwa gharama yoyote,” alisema Jaji Bomani.

Alisema wajumbe wakilazimisha uamuzi juu ya suala la idadi ya Serikali, nchi itaingia kwenye tafrani ambayo matokeo yake ni kuvuruga amani na hata kuvunja Muungano.

Aidha, Jaji Bomani alisema suala la idadi ya Serikali ni vyema likawekwa kwenye ilani za uchaguzi za vyama mbalimbali na Serikali iahirishe suala hilo hadi baada ya uchaguzi mkuu mwakani.

Akizungumzia kuhusu lugha chafu bungeni hususan vurugu zilizotokea bungeni kati ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredrick Werema alisema Jaji Werema, alikosea kupandisha jazba.

“Tukio hilo halikuwa na taswira nzuri kabisa, yaani wabunge wanatukanana halafu mbaya zaidi mmoja ni mtumishi wa Serikali, Werema alitakiwa asipandishe jazba kiasi kile.

“Viongozi wanatakiwa kuchunga ndimi zao popote wanapokuwa si bungeni tu hata kwenye mikutano ya hadhara, wanatakiwa kuwa wavumilivu si lazima kujibu kila hoja unayotuhumiwa nayo,” alisema Jaji Bomani.

Kuhusu Serikali kushindwa katika kesi nyingi inazofungua hususan kwa viongozi wake katika mahakama mbalimbali, alisema kuna udhaifu katika uwasilishwaji wa mashtaka na upelelezi.

Alisema mara nyingi kwenye upelelezi wanakuwa hawajajiandaa vizuri ambapo kesi inapofika mahakamani ushahidi unakuwa hautoshi.

“Lakini pia mahakimu nao wanachangia kwa sababu hakimu anaweza kuwa ana hasira zake labda mtuhumiwa ni mtu wake, lakini cha msingi wote ni kuzingatia taaluma zao,” alisema Jaji Bomani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles