29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU YA WATU KUFIKIA UAMUZI WA KUJIUA

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


MATUKIO ya watu kujiua yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini, ni matukio yanayoshtua na kuogopesha mno pindi tunapoyasikia.

Kwa sababu si jambo rahisi hata kidogo mtu kuamua na kukatisha uhai wake. Mara nyingi jamii huwa inabaki ikijiuliza maswali mengi.

Watu wanaposikia fulani kajiua hujiuliza imekuwaje hadi amefikia uamuzi huo ambao wengi hutafsiri kuwa ni mgumu.

Maswali hayo ndiyo yaliyolisukuma gazeti la MTANZANIA kufanya mahojiano na Msaikolojia Tiba wa Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Isack Lema.

Akizungumzia suala hilo anasema hali hiyo huweza kujitokeza iwapo mtu anakuwa ameugua ugonjwa uitwao kitaalamu sonona (depression) na akakosa mtu wa kumpa msaada unaostahili.

“Sonona ni miongoni mwa magonjwa ya akili, watu wengi wanapitia hali ya huu ugonjwa lakini si wote ambao wanatambua na kutafuta tiba sahihi kwa sababu hawajui,” anasema.

Anafafanua kwamba sonona ni ugonjwa wa akili ambao upo katika kundi la magonjwa ya hisia.

“Ni ugonjwa ambao hutokana na masuala mbalimbali ambayo tunayapitia kila siku ndani ya jamii,” anasema Lema ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa na Afya ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Anasema magonjwa mengi ya akili huanza kutoka kwenye vitu ambavyo ni vya kawaida kwenda kwenye vile vitu ambavyo si vya kawaida.

Anasema ugonjwa wa sonona huathiri utendaji kazi wa akili ya mtu, hisia za mgonjwa husika, mwitikio wa mwili na tabia yake kwa ujumla.

Dk. Lema anasema sonona ni ugonjwa ambao mara nyingi mtu anayeugua huishia kuumia lakini jamii inayomzunguka inaweza isielewe nini kinachoendelea katika maisha ya muhusika.

“Wakati mwingine hata mgonjwa mwenyewe anaweza asielewe kitu kinachoendelea katika maisha yake hivyo anakuwa akiumia mwenyewe moyoni mwake,” anasema.

 

Dalili

Anasema dalili za ugonjwa huu zimegawanyika katika makundi mbalimbali, ikiwamo za kiakili, kimwili, kihisia na kitabia.

“Tunapozungumzia akili tunamaanisha ni jinsi gani mtu anavyoweza kuzifanyia kazi zile taarifa anazozipata kila siku na jinsi gani anavyoweza kufikiria, kumbukumbu zake na jinsi anavyoweza kuchukua uamuzi.

“Sasa mtu anayeugua sonona, katika akili yake huwa ni mtu anayewaza mawazo hasi, huwa si mtu wa kuwaza mawazo chanya na anawaza hasi kutokana na yeye mwenye, mazingira aliyonayo na jinsi anavyoyatazama mazingira yajayo,” anasema na kuongeza;

“Mtu mwenye sonona huwa anawaza kwamba hana thamani au maisha si kitu, hayana maana yoyote au duniani si mahala pazuri pa kuishi.”

Anasema mtu anayeugua sonona hata akikutana na jambo ambalo ni chanya katika maisha yake mara nyingi huona limetokea tu kwa bahati mbaya.

“Anaweza kuwaza hivyo akichukulia kwamba limetokea kwa sababu watu hawampendi au kwa sababu maisha yake hayana maana yoyote ndiyo maana linapotokea jambo zuri yeye hachukulia kwamba ni ‘positive’ kwa upande wake,” anasema.

Dk. Lema anasema watu wanaougua sonona huwa wanapoteza kumbukumbu hata kwa jambo ambalo amezungumza na mwenzake muda mfupi uliopita.

“Hii ni dalili nyingine, mara nyingi huwa wasahaulifu, umakini wao katika vitu wanavyovifanya nao huwa unapungua  au unapotea kabisa. “Kwa mfano; iwapo ni mwanafunzi ambaye alikuwa anaouwezo wa kusoma ukurasa mmoja kwa dakika tano pekee kama anaugua sonona  unakuta hawezi tena kusoma kwa dakika hizo labda ukurasa mmoja atausoma kwa dakika kuanzia 20 na kuendelea,” anasema.

Anaongeza; “Kama ni mfanyakazi unaweza kukuta alikuwa na uwezo wa kufanya kazi zake kila siku kama kawaida lakini, akipata tatizo hili utakuta anashindwa kuzifanya kama ilivyokuwa awali.

“Au unakuta anatumia muda mrefu kufanya kitu kile kile ambacho alikuwa na uwezo wa kutumia muda mfupi kabla hajaugua,” anasema.

Anasema kwa sababu mtu anakuwa ametawaliwa na mawazo hasi akilini mwake hufikia hatua ya kuona maisha hayana thamani kwake na hivyo kuanza kupata mawazo ya kutaka kujidhuru.

“Ndipo hapo utakuta mtu anafikia uamuzi wa kujaribu kujiua na hadi inafikia hatua hiyo unaweza kukuta wale waliomzunguka wanakuwa bado hawajajua nini kinachoendelea, hizi zote ni dalili za kiakili,” anasema.

Anasema kwa kuwa sonona ni ugonjwa wa kihisia, hivyo mgonjwa huanza kupata dalili za awali za kihisia.

“Mara nyingi mtu mwenye sonona huwa na huzuni kupita kiasi, wakati mwingine huwa ni mtu wa hatia, anaweza akazungumzia jambo ambalo limetokea na akajilaumu kwa jambo hilo utadhani ni yeye amelitenda kumbe hajatenda,” anasema.

Anasema wengine huwa ni watu wenye jazba, kiasi kwamba wanapoulizwa jambo dogo hughafirika lakini baada ya muda hujikuta wakiomba msamaha.

“Wakati mwingine unakuta anarudi kuomba msamaha kwamba hakukusudia lakini baada ya muda ile hali inamtokea tena na anakuwa haelewi kwanini inamtokea,” anasema.

 

Dalili za kimwili

Anasema mtu mwenye sonona anakuwa anakosa usingizi au kupata ‘usumbufu wa usingizi.’

“Hali ya usumbufu wa usingizi imegawanyika katika makundi matatu, kundi la kwanza ni yule mtu ambaye anaenda kitandani lakini akijaribu kulala anakosa usingizi, anajikuta anakaa muda mrefu kabla ya kupata usingizi,” anasema.

Anafafanua kundi la pili kuwa ni yule mtu ambaye akienda kulala hupata usingizi lakini akishtuka usiku wa manane anakaa muda mrefu bila kuupata tena.

“Kwa sababu anakosa usingizi, unakuta anakaa muda mwingi akiwaza mambo mengi yanayomtokea katika maisha yake anakuwa hawezi kulala tena,” anasema.

Anataja kundi la tatu kuwa ni yule mtu ambaye hupata usingizi kwa muda mrefu kuliko kawaida yake.

“Yaani kwa mfano kama alizoea kulala saa tatu usiku na kuamka saa 12 alfajiri, ghafla anajikuta anashindwa kuamka katika muda ule aliozoea pengine anapitiliza hata hadi saa tatu na kuendelea,” anasema.

 

Kukosa hamu ya kula chakula

Daktari huyo anasema hii nayo ni dalili nyingine ambayo mtu anayeugua sonona huipata.

“Wapo ambao hujikuta hamu ya kula inapungua, kwa kuwa wanakula kiwango kidogo cha chakula matokeo yake uzito wa mwili wake hupungua, ingawa wapo wengine pia ambao hujikuta hamu ya kula chakula inaongezeka lakini wengi huwa inapungua,” anasema.

 

Uchovu wa mwili

“Hii nayo ni dalili nyingine mtu hupata uchovu wa mwili, wengi hulalamika kupata maumivu ya viungo vya mwili, maumivu ya kichwa, mgongo na sehemu zingine za mwili.

“Huwa wanadhani kuna tatizo kwenye miili yao na kwa kuwa huwa hawapati usingizi, mwishowe unakuta miili yao haipo ‘active’ katika kufanya kazi mbalimbali.

“Hufanya kazi kwa taratibu mno, tofauti na awali kiasi kwamba watu waliomzunguka humshangaa, pamoja na dalili hizo wakati mwingine huambatana pia na suala la homoni za mwili, wengine hupatwa na ile hali ya usumbufu na wapo ambao hamu ya kujamiiana hupungua.

“Sasa pata picha mgonjwa huyu ni mwanandoa na mwenzake anamuhitaji lakini yeye hamu hana tayari kunakuwa na usumbufu unaojitokeza, iwapo mtu anakuwa hajabaini kwamba hiyo ni dalili ya sonona anaweza kudhani mwenziye anamfanyia makusudi, kumbe ni mgonjwa,” anasema.

 

Dalili za kitabia

Dk. Lema anasema watu wanaougua sonona huwa wanatabia ya kujiondoa au kujitenga kwenye jamii, wanapenda kukaa maisha yao wenyewe.

“Inaweza kwenda hadi kwenye mawasiliano, unaweza kumpigia simu na asipokee, anakuwa hajisikii kabisa kupokea simu. Au kama alikuwa anapendelea kufanya vitu fulani mfano, kuangalia vipindi mbalimbali kwenye runinga anakuwa haangalii tena, anakuwa amejitenga na wakati mwingine huwa wanafanya vitu vingi kwa kujilazimisha,” anasema.

 

Tafiti

Anasema tafiti zinaonesha kuwa watu wengi wapo katika hatari ya kupata sonona kutokana na mambo waliyoyapitia katika maisha yao.

 

Mambo yanayochangia

Anasema yapo mengi mfano kufiwa na wapendwa au watu wa karibu au kupotelewa na kitu cha thamani maishani.

“Kuna wakati fulani mtu unajikuta unakuwa na migogoro ya nafsi katika nafsi yako, yaani mfano unatamani jambo fulani liende vile unavyotaka lakini inakuwa kinyume chake, kwa hiyo unakuwa unajiuliza maswali mengi, au unakuwa na migogoro na watu wengine.

“Kuna hali ya kutengwa na jamii pia, sasa mtu anapotengwa na matukio mengine kutokea katika maisha yanamfanya kuwa na ile hali ya huzuni (hapa inakuwa bado haijafikia kuwa ugonjwa).

“Kwa mfano, watu walikuwa kwenye uhusiano na ukavunjika, wakati ambapo hawa wawili hawajajiandaa kuondoka kwenye uhusiano, wanaweza kupata hali ya huzuni na kujiuliza kwanini uhusiano wao umevunjika.

“Na wakipitia hii hali ya huzuni wataanza kupata dalili nilizozitaja awali, kuvunja uhusiano si kitu kizuri, ila mtu kupitia zile dalili ni hali ya kawaida,” anasema na kuongeza:

“Lakini huyu mtu hawezi kuwa mgonjwa wa akili mpaka ile hali imeendelea si chini ya miezi mitatu.”

 

Sababu nyingine

“Wengine hupata sonona, labda kwa vile amezaliwa katika familia ambayo ina hali ya uhatarishi ya kupata sonona, kwa sababu ni miongoni mwa magonjwa yanayorithiwa katika familia,” anasema.

Anafafanua kuwa hawezi kuugua hadi atakapofikia kile kiwango cha juu cha msongo wa mawazo kinachoweza kumfanya augue.

 

Ni vigumu kumtambua mgonjwa

Anasema hiyo ni kwa sababu mara nyingi mtu anapokwenda huwa hajielezi kwamba anajisikia huzuni, ameachwa au amefukuzwa kazi.

“Wengi hujieleza kwamba wanajisikia maumivu ya kichwa, mwili, hawapati usingizi, sasa huyu mgonjwa akikutana na mtaalamu ambaye hafahamu dalili za magonjwa ya akili, anaishia kumpima magonjwa mengine kama malaria lakini mtu wa aina hii akitibiwa huwa haponi, kwa sababu anaugua sonona,” anasema.

 

Matibabu sahihi

Anasema mtu akigundua na kufika kwa wataalamu wa saikolojia humpa tiba sahihi na kupona kabisa.

“Huwa tunampa mgonjwa dawa tiba ambazo humsaidia kurejesha usingizi na kumrejesha katika hali yake ya kawaida, tunampa pia tiba za kisaikolojia ambazo humsaidia kwenye kufikiria na tunamtibu kwa njia ya kazi.

“Tiba za kisaikolojia zitamsaidia kumtoa katika hiyo hali, kisha tutamfanyia tiba ya kitabia na baadae atarudi katika hali yake ya kawaida kabisa,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles