LONDON, UINGEREZA
WAZIRI Mkuu wa Uingereza Theresa May ametia saini barua ambayo itaanzisha rasmi mchakato wa kuiondoa Uingereza kutoka kwa Umoja wa Ulaya (EU).
Barua hiyo inatoa taarifa rasmi ya kujiondoa kutoka umoja huo kwa kutumia Kifungu 50 cha Mkataba wa Lisbon.
Iliwasilishwa kwa Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk jana mchana na Balozi wa Uingereza katika EU, Sir Tim Barrow.
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kura ya maoni iliyofanyika Juni mwaka jana, ambapo wapiga kura waliunga mkono kujiondoa kutoka EU.
May aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri jana asubuhi kabla ya kutoa taarifa rasmi kwa wabunge kuthibitisha kwamba mchakato wa Uingereza kujiondoa EU umeanza.
May aliwaambia wabunge kuwa hatua hiyo inaashiria wakati wa taifa kuungana pamoja.
Aliahidi kuwakilisha kila mtu katika Uingereza yote wakati wa mazungumzo ya kujiondia ikiwamo hatima ya raia wa EU wanaoishi Uingereza, ambao wamekuwa na wasiwasi.
“Nimejitolea kuhakikisha tunapata mkataba bora zaidi kwa kila mtu katika nchi hii,” May alisema.